Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja zilizoko mezani.

Mheshimiwa Spika, kwanza, nianze kwa kukupongeza wewe mwenyewe kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, hongera sana. Hii siyo kwa sababu ya jambo jingine unao uwezo mkubwa na umetuheshimisha sana. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazozifanya kwa ajili ya nchi yetu na nimefurahi sana juzi wananchi wa Hai walikuwa barabarani, umeme ulizimika sasa tumewekewa pale taa za barabarani Bomang’ombe barabara kama nne, wanasema wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu. Hapa niseme kidogo, Mheshimiwa Waziri Mkuu anafanya kazi kubwa, tunaona anavyohangaika haya majizi tunayosema huko, siyo tu kwamba wanatudanganya sisi, hata Waziri Mkuu akienda huko mnaona wanavyomjibu. Mheshimiwa Waziri Mkuu nikupe pole sana hao ndiyo watumishi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa kuaminiwa na kupewa dhamana kubwa, mimi nimwambie tu Watanzania wanataka umeme na mafuta ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na issue ya KADCO imezungumzwa hapa. Mimi niwaambie Waheshimiwa Wabunge pamoja na investment kubwa inayofanyika, sasa hivi Serikali imetoa bilioni 11 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi waliokuwa kwenye eneo lile la Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro watoke na wamekubali. Mimi nashangaa tumepitisha hapa tuambiwe kiwanja kile kisimamiwe na Mamlaka ambayo ni ya Serikali mpaka leo halijafanyika.

Mheshimiwa Spika, jambo hili linaudhi na mimi niwaambie nipo kule site, likichelewa jambo hili tutazungumza lugha nyingine baadae, siyo vyema. Ninaomba sana Serikali ifikie mwisho ichukue maamuzi.
Mheshimiwa Spika, naungana na Mheshimiwa Ole-Sendeka kwamba tuunde Kamati Teule iende awamu tatu taarifa ya CAG, tuone CAG aliagiza nini, nini kimefanyika na kwa nini na hatua gani zinapaswa kuchukuliwa?

Mheshimiwa Spika, tusipofanya hivi, tutakuwa tunazungumza hapa kila mwaka tunajaa gesi hapa mambo yanaendelea vilevile. Waheshimiwa Wabunge sote tunafahamu Utumishi wa Umma kuna shida. Kuna shida kubwa hawa watu wameshakuwa sugu, hivi nawaambia wengine wako mule, hawa wanasema majamaa wanapiga stori wataondoka, business as usual! wako pale wanatusikiliza, wanajua kabisa hakuna kitakachofanyika. Mheshimiwa Waziri Mkuu wanakusikiliza pale! Wanajua hawa wataongea wataendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niwaambieni tumepita Kamati ya TAMISEMI huko Halmashauri, tunawasilikiza wakija kwenye Kamati, anakuja Mkurugenzi pale unamsikiliza huyu mtu hata kujumlisha hesabu zinawashinda, unamuuliza swali mtu mwepesi kabisa. Hapa kwenye Taarifa ya Kamati ya LAAC wameandika naomba nimnukuu “Kamati imefanya uchambuzi wa kina na kujiridhisha kutokuwepo kwa ufanisi wa utendaji wa Wakurugenzi”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kama watu hawana ufanisi Mheshimiwa Waziri Mkuu wameshindwa kazi hawa watu. Tunaenda mahali pale Iringa ni aibu, tukaenda kuangalia soko lile ni kilio. Mheshimiwa Waziri Mkuu utembelee pale. Nadhani awamu hii utawapiga makofi, kwa sababu ni aibu! Ni vitu ambavyo havifai. Mheshimiwa Waziri Mkuu hebu tufikirie Mheshimiwa Rais wetu amefanya kazi kubwa, ametupatia fedha, mtu anapewa trilioni 1.2 nenda kajenge madarasa kwa mradi wa SEQUIP, pesa umepewa cash, tengeneza ramani wewe, tengeneza mpago wa ujenzi wewe, tengeneza feasibility wewe, unaenda kujenga madarasa hayakamiliki, kama siyo maksudi, kama siyo hila, kama siyo mpango mbaya wa kumuhujumu Mheshimiwa Rais, ni kitu gani? Kwa sababu siyo pesa ya mkopo, pesa ipo cash. Unaenda pale darasa halijakamilika havieleweki vitu vinavyofanyika, haya ni maksudi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niseme tubadilishe mazungumzo namna ya kuzungumza na hawa watumishi. Mheshimiwa Jenista Mhagama hapa Mama yangu ameongea kwa uchungu sana na mimi nikamuonea huruma, lakini Mheshimiwa Waziri tumkamate nani zaidi ya ninyi? Sisi tuwabane na ninyi mkawabane wale. Ninyi ndiyo size yetu. Tunafahamu mnafanya kazi nzuri sana, lakini hawa majizi mnayo humo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Bashe ana majizi yake kwenye Ushirika kibao ya kutosha, Mheshimiwa Kaka yangu hapa Mchengerwa una majizi yako kule TAMISEMI ya kutosha na unayajua, nenda kayatoe, ukiyatoa sisi tutakuja hapa tutapongezana, kwa sababu hivi vitu vinafanyika ni maksudi kabisa! Haya majizi ya Ushirika Mheshimiwa Bashe anayajua, kila mwaka tunazungumza anayo mule ndani, sasa mnataka tukamwambie nani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa TAMISEMI unafahamu majizi unayo, Wakurugenzi ambao hawaeleweki wanafanya miradi ya hovyo, unafahamu na wewe upo kwenye Kamati yetu! Sasa usipochukua hatua unataka tukamwambie nani? Hawa watu wanamhujumu Mheshimiwa Rais na sisi ndiyo kazi yetu kusema hapa. Hizi fedha hizi hebu fikiri…(Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam.

TAARIFA

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Saashisha. Ndugu yetu Waziri wa Ujenzi, nyumbani kwao kwa Mama yake Sengerema kuna kituo kinajengwa cha afya na yeye alikuwa ni Waziri wa TAMISEMI. Imepelekwa pesa imeliwa na madarasa hayajaisha. Karibu sana Mchengerwa Sengerema. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, unapokea taarifa hiyo?

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, naipokea na bahati nzuri tulienda Mwanza, tuliona hilo jambo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kweli nilikuwa nasema hizi fedha ifike mahali tumuonee huruma huyu Mama, anayo dhamira ya dhati ukimsikiliza unaona huyu Mama anatamani mabadiliko, anatamani watu wapate huduma. Hivi hawa watu wanaomsaidia mbona hawafanani na huyu Rais wetu, mnataka tufanyaje?

Mheshimiwa Spika, unajua tunafikia mahali watu wanafikiri, mimi tukiwa pale Mbeya kwa kweli nilijikuta nimesema tu, hivi kwa nini hawa watu wasipigwe risasi? Inafika mahali unaona ni hujuma fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka nizungumze tu kwenye elimu, TAMISEMI wamepewa trilioni 1.2 kwa ajili ya SEQUIP, wamepewa pesa za BOOST bilioni 1.15, wamepewa fedha kwa ajili ya vyoo bilioni 230 haijawahi kutokea! Hawa watu wamechanganyikiwa wanafikiri hela ni za kwao hizi, Mheshimiwa Mchengerwa usipochukua hatua wanadhani ni zao. Hawa watu hawako na mama tukuambie hapa uelewe, nendeni mkachukue hatua kwenye utumishi wa umma kuna jambo la kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ndio mahiri wa kusema aah, wanasiasa ndio wanaharibu nchi, Wabunge; wanatusema sisi wakati wao ndio wanaoharibu vitu, wao ndio hawafanyi kazi. Mheshimiwa Ndejembi tumeendanaye ziara, ni aibu tupu. Anasimama Mkurugenzi, unajiuliza, huyu mtu katokea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami niseme jamani, turudi kwenye utaratibu. Kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma, namna ya upatikanaji wa Wakurugenzi, imeelezwa. Sheria za utumishi zipo wazi, awe amefanya kazi miaka 12, awe na uzoefu. Wakati mwingine ni sawa hatujadili kuhusu namna ya uteuzi, lakini tunashauri, turudi kwenye sheria kwa sababu, Mkurugenzi anaenda pale Halmashauri ni mpya, katokea kwenye taasisi nyingine, hajui chochote. Anakuta Wajumbe, wale Wakuu wa Idara, ni magwiji yako pale miaka na miaka. Mkurugenzi anakuja maskini wa Mungu ni mwepesi, hajui kinachoendelea, wale ndio wanamtengenezea ramani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unajikuta Mkurugenzi yuko pale, hajui kinachoendelea kabisa, haijui Halmashauri. Ndiyo maana akija hapa kila ukimwuliza swali…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Muda wako umekwisha.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Dah!

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja zote za Kamati. (Makofi)