Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Omar Ali Omar

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Wete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii adhimu. Kwanza, sina budi kumshukuru Allah Kareem aliyeumba mbingu na ardhi na vilivyomo vyote tukapata uhai huu ambao tumo katika siku ya Jumamosi tukiwa sote tuko wazima.

Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa na ufahari mkubwa leo nimesimama katika Bunge lako Tukufu ukiwa wewe ndiye Rais wa Mabunge ya Dunia. Kwa kweli nakupongeza sana na nina imani kwamba, Wabunge wote wataunga mkono hili la kukupongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kwa heshima na taadhima, naomba uniruhusu kidogo nitoe ushairi ambao mtaalam wa Lugha ya Kiswahili kule Zanzibar ndugu yangu Haji Gora aliutoa katika kitabu chake cha kimbunga. Katika kitabu cha kimbunga ndugu yangu Haji Gora alizungumza maneno yafuatayo; katika ushairi wake alisema kwamba: “Chura kakausha mto, maji yakamalizika, Pwani kuliwaka moto, mawimbi yaliyowaka usufi nusu kipeto, rikama likavunjika, nyoyo zikafadhaika.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana ya ushairi huu ni kwamba sote Wabunge tuliomo humu, tumefadhaika sana na Ripoti ya CAG na tumefadhaika kwa sababu ya hali ya upepo wa fedha za walipakodi wa nchi hii zinavyotafunwa, zinatafunwa mkono wa kulia wa kushoto haupati. Zinatiwa kwenye pua ya upande wa mkono wa kulia wa kushoto haupati, matokeo yake hali ya uchumi inadorora na matokeo yake Wananchi wetu wanabaki katika umaskini uliokithiri.

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze kuhusu Wazabuni na Wakandarasi ambao imezungumzwa katika ripoti zetu hizi tatu kwenye ukurasa wa 44. Taasisi 259 zinadaiwa na Wazabuni, zinadaiwa na Wazabuni ambapo Serikali inadaiwa jumla ya trilioni 4.82 kwa kweli hili ni jambo la kusikitisha sana, lakini wazabuni pekee wanadaiwa fedha trilioni 3.40 sawa na asilimia 83, hilo ni deni la wazabuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri nina documents ninataka nitaje baadhi ya taasisi za Serikali ambazo zinadaiwa madeni makubwa. Kwa mfano, kuna Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania inadaiwa bilioni 60. Wakala wa Ufundi wa Umeme (TEMESA) bilioni 49, Wakala wa Huduma ya Ununuzi wa Serikali (GPSA) inadaiwa bilioni 13. Kwa kweli hicho ni kimbunga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, SUMA JKT Kampuni ya Ujenzi inaidai Serikali, wazabuni hao jumla ya bilioni 10. Mfuko wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) bilioni 90. Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) bilioni 41. Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Dar es Salaam bilioni 137. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa angalia kimbunga hiki, Mamlaka ya Mapato Tanzania ambao ndiyo Taasisi Mama inayokusanya mapato inadaiwa bilioni 224, hawa ni wazabuni ambao wanaidai Serikali kwa kipindi kirefu sasa. Sasa nenda basi ukaangalie katika hospitali zetu. Ukienda Benjamin Mkapa, wazabuni hawa wanapima pressure kipimo kinasoma juu moja kwa moja. Ukienda Hospitali ya Mirembe, ambako huko ndipo wagonjwa wanaoshikwa na matatizo ya akili, napo huko wapo wazabuni ambao tayari wameshakwenda kule, kwa sababu akili hazifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matokeo yake watanzania hawa ndiyo wale ambao sasa hivi waliokuwa sasa hawana uchumi tena, nyumba zao zimepigwa mnada na mabenki, viwanja vyao walivyokuwa navyo vimeuzwa, magari yao waliokuwa wakitembelea waliokuwa wakifanya kazi nayo yamepigwa mnada, matokeo yake ni kwamba hawa wamekuwa masikini. Hii ni kuionesha kwamba Serikali haijawa makini katika kulishughulikia suala la hawa wazabuni.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika hii paper niliyonayo, mpaka Wizara zote zimo humu, Wizara zote zinadaiwa na wazabuni! sasa hii tunakwenda wapi? tunafika wapi ikiwa Serikali inadaiwa namna hii na deni kubwa kama hili, je tunafanyaje? Mawazo yangu mimi, maana yake najua kwamba wasimamizi wa Serikali ni Mawaziri, lakini kuna watendaji wao. Hao watendaji ndio wanastahiki sasa wawajibishwe, kwa sababu hizi fedha nina imani kwamba zinakwenda, Mheshimiwa Waziri wa Fedha anatoa Fedha na anazipeleka, kwa sababu tunampitishia fedha kwenye bajeti lakini matokeo yake fedha hizi zinaliwa na watu wachache.

Mheshimiwa Spika, mawazo yangu mimi, wenznagu wengi walisema kwamba wanyongwe lakini ukinyongwa ndio umeshakufa, utakuwa huonekani wala hupati uchungu, kwanza wezi hawa tuanze kuwakata mkono, wakiona mkono mmoja hawana watajua kwamba kweli waliiba pesa za watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia wafungwe jela wawekewe daftari maalum la uzalishaji, kwamba ikiwa umezalisha kule mali ya 10,000 na ionekane deni letu lile tulilokuwa tunawadai tayari 10,000 imetoka, mpaka muda wao umeisha. La tatu na mwisho, wafilisiwe mali zao hadharani na kila mtanzania ajue kwamba mali hii inafilisiwa kwa sababu ya kuibia Serikali mali ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maneno hayo mafupi mimi naunga mkono hoja asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)