Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote na mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge na mimi kutoa maoni yangu juu ya Taarifa tatu za Kamati zilizowasilishwa katika Bunge lako hili.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kudumisha utulivu, amani lakini pia kwa kujituma na kuhakikisha tunapata fedha za miradi ya maeneleo zinakuja kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kwa maana ya CAG pamoja na ofisi yake kwa uzalendo wake mkuu na namna ambavyo anawajibika kuhakikisha angalau anadumisha na kurudisha uzalendo na uimara katika fedha za Serikali kwenye miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, tunakubaliana kwamba Ofisi ya CAG kama Mdhibiti wa Hesabu za Serikali ametimiza wajibu wake. Mbele yetu sisi tunao mtego, sisi kama Bunge la watunga sheria ambao kimsingi yanayokwenda kukaguliwa na CAG na yanayotekelezwa na watumishi mbalimbali yanaendana na sheria mbalimbali ambazo zimetungwa ndani ya Bunge hili na sisi ndiyo watungaji wa sheria hizi.

Mheshimiwa Spika, mtego ulioko mbele yetu ni pale ambapo taarifa hizi zinakuja na baadhi yetu wataalam na watumishi mbalimbali wamekiuka sheria na taratibu mbalimbali ambazo zinatungwa ndani ya Bunge na sisi kama Wabunge tunaingia mjadala wa kuweza kuzijadili.

Mheshimiwa Spika, kwa kuendelea kutoa maoni ya Taarifa ya CAG ningetamani tutakapopata nafasi ya Waheshimiwa Mawaziri mimi ningependa sana nitoe ushauri, watakaposimama kwanza tupitie mapendekezo ya Bunge hili ya Taarifa ya CAG ya miaka miwili au mitatu iliyopita kabla hatujaanza kupitia mapendekezo ya mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, kwa kufanya vile tutakuwa moja; tunadhibiti na kuimarisha maelekezo ya Bunge hili kwamba Bunge linapotoa mapendekezo ya kwenda kufanyiwa kazi basi uimara wa taarifa huo uweze kufanyika. Kwa mfano, wakati tunajadili mwaka jana Taarifa ya CAG ilionekana kwenye fedha za mikopo peke yake, mikopo ya vijana, wanawake na walemavu, taarifa ya mwaka jana kwa maana ya 2020/2021 zaidi ya shilingi bilioni 47 zilikuwa zimekwenda mahali ambapo kuna utata hazieleweki. Mwaka huu Taarifa ya CAG inazungumza zaidi ya shilingi bilioni 88 kwa maana hiyo zimeongezeka zaidi ya mara mbili na kwenyewe matumizi yake hayaeleweki.

Mheshimiwa Spika, kwenda kujadili shilingi bilioni 88 peke yake tukaacha kupata maelekezo ya Serikali na Wizara husika hatua walizochukua kwa Wakurugenzi, Maafisa Maendeleo na Wakuu wa Idara mbalimbali waliosababisha hasara ya shilingi bilioni 47 tunakoenda kujadili shilingi bilioni 88 maana yake tunaacha kiporo huku nyuma na inawezekana mwakani tukarudi tena kujadili zaidi ya shilingi bilioni 88. Kwa hiyo, uendelevu huu ni lazima tuhakikishe kwamba sisi tunausimamia.

Mheshimiwa Spika, la pili, kwenye Bunge hili tumetunga Sheria kwamba mwananchi akinunua chochote, akihitaji mahitaji yoyote au bidhaa yoyote ni lazima aombe risiti. Sheria hiyo tumekwenda kutengeneza Kanuni kwamba asipoomba risiti mwananchi mnyonge wa kule kijijini anatakiwa kulipa shilingi milioni tatu kwa ile risiti ambayo hakuomba. Hili limekuwa likifanywa na TRA na wenzetu na linasimamiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, sasa tujiulize sisi Serikali imefanya malipo ya zaidi ya shilingi bilioni 10 na hawajaomba risiti ya eletroniki, lakini wamelipa fedha. Sasa tunataka tujue nani anayewajibika hapa na ndiyo maana ninasema Waheshimiwa Mawaziri sisi inawezekana hatuna ubaya na ninyi tunataka tujue mtakavyokuwa mnatoa majibu hasa Waziri husika. Wakurugenzi wa hizi Halmashauri wote waliotoa risiti ambao kimsingi mmeshindwa kuwaomba ile shilingi milioni tatu ambayo mwananchi wa kawaida anatoa. Ukisimama kutoa majibu…(Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi jana Mawaziri walikuwa wanatoa taarifa sana kwa Waheshimiwa Wabunge, naomba na sisi uturuhusu leo Waziri atakapokuwa anatoa majibu ambayo hayaridhishi kwenye kipengele ambacho tunahitaji majibu tupe nafasi tumpige taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ningetamani Waziri husika aniambie Wakurugenzi waliolipa fedha hizi bila risiti za elektroniki wako wapi na asiniambie wahewahamisha kutoka kituo “A” kwenda kituo “B.” Nataka aseme hadharani wamefukuzwa, wako kwa mujibu wa sheria mahakamani au wako wapi. Ukiniambia umewatoa sehemu “A” kwenda sehemu “B” nitaomba unipe nafasi ya kum-correct Mheshimiwa Waziri huyo ili angalau twende sawasawa. Kwa kufanya hivyo tutakuwa angalau tunakwenda kama vile inavyotakiwa.

Mheshimiwa Spika, la pili, Mheshimiwa Waziri husika atakaposimama leo atuambie leo ndani ya Bunge fedha ya POS ambayo imekusanywa shilingi bilioni 11 hazikupelekwa benki, hizi fedha hawa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara wamezipeleka wapi? Aseme yeye yaani natamani jibu liwepo kwamba hawa Wakurugenzi wa hizi Halmashauri waliosababisha upotevu wa fedha hizi leo watatu wako mahakamani, wanne wako sehemu fulani na usiniambie umewahamisha kutoka sehemu “A” kwenda sehemu “B.”

Mheshimiwa Spika, inauma sana na naamini wote tutakubaliana, ni sawa na mtu una duka lako umemuweka kijana asimamie mauzo ya duka lako, halafu yule kijana anakuibia fedha ya kwako wewe mfukoni. Anachokiuza anakipeleka mfukoni hapeleki benki wala hakupi wewe eti kwa kujifurahisha na kuchukua hatua unamhamisha kutoka kwenye duka “A” unampeleka kwenye duka “B” halafu unapiga makofi kwa kujipongeza kwamba nimechukua hatua zinazostahili, hii si sawa.

Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba kama wewe una uchungu na yule kijana aliyekuibia fedha yako maana yake utachukua hatua stahiki. Tunataka tuone Waheshimiwa Mawaziri mtakapokuwa mmesimama kutoa taarifa hapa mtuambie hawa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara mmechukua hatua gani za kinidhamu? Hili nadhani litaongeza umaarufu.

Mheshimiwa Spika, pia natamani nitoe ushauri kwa Mheshimiwa Waziri na kwa Serikali kwa ujumla wake. Haya yote yanafanyika kwa sababu ya sheria zilizopo, Sheria ya Utumishi wa Umma, sheria mbalimbali za usimamizi wa manunuzi na sheria zote zinazoendesha miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri aone namna ya kurekebisha hizi sheria. Kwa mfano, leo kijana analipwa mshahara wa shilingi 800,000 mpaka shilingi 1,000,000, afisa wa kawaida. Shilingi milioni moja au laki nane kwa mwezi kwa mwaka maana yake anachukua milioni kumi huyu kijana. Kwa miaka mitano ukizidisha shilingi milioni kumi maana yake ana shilingi milioni hamsini peke yake, kwa miaka kumi ndiyo ana shilingi milioni 100. Amekutana na deal la shilingi bilioni mbili mezani kwake ambayo akifanya kazi ya utumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 30 hata 50 mpaka anastaafu hawezi kupata ile shilingi bilioni mbili maana yake atakupiga shilingi bilioni mbili na akikupiga shilingi bilioni mbili anajua sheria yenyewe iko weak. Kwa sababu sheria yenyewe ni kwamba utamsimamisha, utamchukua utampeleka TAKUKURU, utampa barua ya kujieleza, ndivyo zinavyozungumza maana yake huyu hawezi kuogopa kuiba fedha za umma.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nikaishauri Serikali ifanye mabadiliko ya sheria na ndiyo maana jana tulisema hapa ikibidi iseme mtu wa aina hii kama siyo kunyongwa basi itamke kitu ambacho kinaweza kikafanya watu wote wakaweza kuogopa kuchezea fedha za umma.

Mheshimiwa Spika, lingine ni TAKUKURU; nataka nijue ni chombo gani kinachowasomamia TAKUKURU? Leo Mkuu wa Wilaya akienda kukagua miradi akikuta kuna ubadhirifu utasikia anasema hili liende TAKUKURU. Mkuu wa Mkoa hivyo hivyo akija Waziri hivyo hivyo, akija Waziri Mkuu hivyo hivyo; najiuliza TAKUKURU ukiacha haya ambayo yametajwa humu kwenye Taarifa ya CAG haya ambayo yanatolewa matamko na viongozi wa kisiasa na viongozi wa Serikali TAKUKURU anayo mangapi?

Mheshimiwa Spika, nani anaki-regulate kile chombo kuhakikisha haya maelekezo, hizi kesi mbalimbali TAKUKURU anazipeleka mahakamani na zinafanyiwa kazi? Nani anaye-regulate? Ndiyo maana ukiangalia hii Taarifa ya Kamati wanasema TAKUKURU ni kichaka cha taarifa mbalimbali kwa sababu hakuna chombo na kama kipo maana yake kimeshindwa kusimamia TAKUKURU kuhakikisha kesi mbalimbali zinakwenda mahakamani.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana tunashauri kiwepo chombo maalum ambacho kinafuatilia kesi mbalimbali zote na matamko ya wanasiasa ambayo TAKUKURU wanapewa jukumu lake ili angalau kila mwezi kwa miezi mitatu tupate taarifa kwamba wanachukua hatua gani juu ya utekelezaji wake.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Jafari Chege kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

TAARIFA

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nilitaka kumpa taarifa kwamba baada ya Wilaya ya Bunda kupokea kesi zaidi ya 40 za TAKUKURU nilipoenda kwa TAKUKURU Wilaya akasema yeye hana uwezo wa kupeleka hao watu mahakamani mpaka apate idhini ya TAKUKURU Mkoa, kwa hiyo ni process. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Jafari Chege unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa ndiyo maana nikashauri kwamba kiwepo chombo ambacho kinawa-regulate, kinawa-control hawa watu. Kwa sababu TAKUKURU ukiacha kesi ambazo zimetajwa kwenye taarifa wewe ni shahidi haiwezi kupita mwezi hujasikia viongozi wa kisiasa au Kiserikali kusema jambo hili, kama imetokea mradi wowote wa wananchi, jambo hili TAKUKURU chukua ukalifanyie kazi. Nani anayeyafuatilia yale mambo kama yanafanyiwa kazi sawa sawa ili mwishoni angalau Wabunge au Serikali au wananchi wote tupate taarifa sahihi kwamba kesi hizi zinakwenda inavyotakiwa. (Makofi)

SPIKA: Haya ahsante sana kengele ya pili ilikuwa imeshagonga.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika nakushukuru sana. Naunga mkono hoja, ahsante sana.