Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi asubuhi hii, lakini nikupongeze kama alivyotangulia kusema ndugu yangu hapa Mheshimiwa Getere kwamba nafasi uliyonayo ni kubwa sana na naamini dunia inafuatilia Bunge letu la Tanzania na nikuombe sana utengeneze historia kwenye Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utatutendea haki sana endapo utaelekeza sasa sisi kama Wabunge tukae na kupitia maazimio yote yaliyotolewa na Bunge kwenye Ripoti za CAG kwa miaka mitatu nyuma ili wote waliohusika wawajibishwe ndani ya Bunge letu, kwa sababu hiki ndicho wanachokisubiri wananchi huko nje kuona sisi tumefanya nini.

Mheshimiwa Spika, ukifuatilia kwenye mitandao binafsi unapongezwa sana na Wabunge wengi wanaochangia wanapongezwa sana. Ndugu zetu Mawaziri kwa namna fulani wanalaumiwa na wanakuwa less popular maeneo mengi hasa zaidi wanapotaka kutoa taarifa za kuwa-distract watu kwenye mjadala mzito kama huu unaohusu Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuombe pamoja na kwamba kanuni zinaruhusu kufanya hayo mambo Waheshimiwa Mawaziri mtuache tuishauri Serikali, lakini pia tujaribu kuielekeza kwa sababu naamini Bunge hili linafuatiliwa wapi kwenye matobo kwenye maeneo sisi tunakotokea kwa maana ya lutaka kulisaidia taifa letu. Kwa hiyo, mtuache tufanye kazi yetu ya kuishauri Serikali, lakini na kuwashauri na ninyi ili mkachukue hatua mtakaporudi kwenye ofisi zenu.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi wameongea na kama ulivyosema hapo kwamba hata muda wenyewe sasa tunapunguza kwa sababu tunaelekea kwenye kuhitimisha. Nimekuja hapa kwa ajili ya kutoa ushauri.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa kwanza kuhusu kubadilisha kanuni ili Ripoti ya CAG inapokuja mwezi Machi ikiwezekana Wabunge tukubaliane tuendelee kuijadili kwa kubadilisha kanuni zetu ili tunapokwenda mwezi Julai kwenda kufanya allocation za pesa nyingine kwa ajili ya bajeti inayofuata na haya tuwe tumepata majibu yake, kwa maana ya kwamba taarifa hii tuwe tumeijadili. Kwa hiyo, tuone namna ya kubadilisha kanuni kwenye hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine Mheshimiwa Simbachawene jana alijibu kwamba sisi Wabunge ni sehemu ya Kamati za Fedha kwenye Halmashauri zetu. Hakuna Mbunge hapa ambaye hafahamu kwamba ratiba zinatofautiana sana. Sisi tuko hapa Bungeni tunajadili masuala haya, lakini na huko kwenye Halmashauri zetu vikao vya Halmashauri vinaendelea, Kamati za Fedha zinakaa, Mabaraza yanakaa. Kwa hiyo, tuone namna ya kubadilisha kanuni ili tuweze kuhudhuria kwenye hivi vikao na tuweze kuzishauri Halmashauri zetu vizuri namna ya matumizi bora ya hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumejadiliwa hapa suala la Mfuko wa Usalama wa Raia SACCOS na kwamba taarifa zimekuja kuna upotevu. Mheshimiwa Bulaya jana hapa alisema vizuri tuombe basi kama kweli tuna nia ya kutaka kuwawajibisha hawa watu na Mheshimiwa Naibu Waziri jana alijibu kwamba kuna watu wako mahakamani. Nataka nimkumbushe amemsahau Mheshimiwa Afande Sirro ambaye alikuwa IGP wakati haya mengine yanatokea basi wafanye utaratibu wamrudishe ili naye aunganishwe na hawa watu walioko mahakamani kwa sababu ametwambia kwamba hili jambo liko mahakamani. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, tukaangalie pia na suala la Mfuko huu wa Kufa na Kuzikana lakini tukaangalie na SACCOS…

SPIKA: Mheshimiwa Cecil Mwambe kuna tarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Bulaya.

TAARIFA

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nampa taarifa, siyo Sirro peke yake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili ametajwa kwenye taarifa baada ya taarifa akapata uteuzi wa Naibu Katibu wa Maliasili na Utalii. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Cecil Mwambe unaipokea taarifa hiyo?

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, naipokea hiyo taarifa nadhani namuongezea Mheshimwa Waziri hapa wigo mpana wa kutimiza wajibu wake.

Mheshimiwa Spika, pia kuna suala la Mfuko huu wa Usalama wa Raia SACCOS, askari wetu wamekuwa na malalamiko makubwa sana, Mheshimiwa Waziri yuko hapa kwamba kila mara wanakatwa, hawapati taarifa zinazohusiana na makato yao, lakini hata hivyo kunakuwa na marejesho ama faida inayopatikana hawajawahi kushirikishwa.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni mishahara imeogezwa, ukiangalia kiasi cha mshahara kilichoongezwa na makato waliyoongezewa polisi kwenye huu mfuko wao havifanani. Kwa hiyo, niwaombe nao wakajaribu kujadiliana na wakubwa wa polisi kwa sababu askari hawa wadogo wanakatwa pesa hizi, lakini wao wanaamini kwa sababu ya utii wanaotakiwa kuwa nao mambo mengine wanashindwa kuyapinga, wanayaleta kwetu sisi kama Wabunge tuseme hapa yasikike ili wakubwa waone namna ya ku-review kwenye haya mambo.

Mheshimiwa Spika, ushauri mwingine lakini hili pia ni ombi na nimemuona hapa rafiki yangu Bwana Ndejembi kwamba tumesoma hizi taarifa zote, tumesikia madudu mengi yanayofanyika kwenye halmashauri zetu. Mimi niko hapa kuomba ukaguzi maalum kwa ajili ya Halmashauri ya Masasi DC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mchungahela hapa jana wakati anasema, wakati anamalizia kwenye dakika ya tisa alitoa maelekezo kwamba hata kwenye Halmashauri yetu kuna ubadhirifu. Nataka nikuongezee, maeneo ambayo natamani kabisa mkayakague la kwanza kabisa ni eneo ambalo Mheshimiwa Rais alitoa pesa kwa ajili ya madawati, eneo hili halijafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ujenzi wa sekondari Shule ya Mpeta, ujenzi ule umekuwa unalalamikiwa sana, lakini pia kuna ujenzi wa ghala letu la Halmashauri ya Wilaya ya Masasi DC, ujenzi huu umekuwa unalalamikiwa sana. Pia tunayo hospitali yetu Mheshimiwa Rais alitoa pesa nyingi za kwenda kukamilisha Hospitali ya Tarafa ya Chikundi, sasa hivi ni karibu mwaka wa pili, tunaelekea mwaka wa tatu pesa zimekwisha, ujenzi wake haujakamilika.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tunalo jengo letu ya Masasi DC ambalo Mheshimiwa Rais alikwenda kulifungua hili jengo mwezi mmoja miezi miwili iliyopita wakatoi wa ziara yake. Wakati Rais anakwenda nataka nikuchekeshe kitu kimoja hapa, palifanyika utaratibu wa kuondoa simenti kwenye Shule ya Sekondari ya Kata ya Chikunja ili kwenda kufanya marekebisho kwenye hili jengo Rais atakapopita aone pale mambo ni safi, naomba mambo yote haya yakakaguliwe na tupate taarifa maalum.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine limejitokeza karibuni pesa za likizo za walimu zaidi ya 120 wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi DC nazo zimetumika kwenye matumizi tofauti, walimu hawa hawajalipwa wameshindwa kwenda likizo. Kwa hiyo, nimeombwa na walimu na ili lenyewe nililete hapa niliseme.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema kwamba mjadala huu umekuwepo hapa kwa siku tatu na sisi tunatokea maeneo hayo, na nakumbuka Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa aje kufanya ziara kwenye Wilaya yetu ya Masasi DC, tulitamani haya mambo yote tumuoneshe tumwambie kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu kuna haya mambo yanayotokea kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo bado niikumbushe Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba sasa waratibu hiyo ziara ya kuja Halmashauri ya Masasi DC, lakini kabla ya hapo ninyi kama watu wa TAMISEMI nendeni mkaangalie haya maeneo niliyowaambia kwa sababu tuna Mkurugenzi mpya, tunae pale DC wetu mpya ambaye ameripoti hivi karibuni, lakini wao wamerithi mambo ambayo wao hawawezi kuyamaliza pale, wameyakuta haya madudu.

Mheshimiwa Spika, pia niishauri Serikali kama inawezekana kila tunapopeleka Mkurugenzi mpya, Mkuu wa Wilaya kwenye maeneo haya ikafanyike kwanza special audit ili wakabidhiwe halmashauri ikiwa clear.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine tunapokaa muda mrefu na hizi taarifa kwa mfano Taarifa ya CAG tunaijadili leo hapa baada ya LAAC kwenda kufanya huko ukaguzi na vitu vingine, kimsingi tumebakisha taarifa mbili, maamuzi ya taarifa zetu tatu za huko nyuma hatujafanyia kazi. Walau sisi tuna historia tulipoingia Bunge la mwaka 2020 lakini tayari haya mambo tulishajadili kati ya 2015 mpaka 2020 tutawaachia kiporo Bunge lijalo kwa sababu tunaacha hivi vitu ambavyo sisi tumeviharibu, tumeshindwa kuviweka sawa sawa tunacha kwa ajili ya Bunge lijalo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe taarifa hizi za CAG zikija mwezi Machi tuzijadili kwa sababu kama hapa anatuambia tunapunguza muda wa majadiliano. Taarifa ambayo imekaa miezi sita/saba na sisi leo tunaijadili kwa dakika nane kwa dakika kumi, kwa dakika 15 tunajadili kwa siku tatu kuna mambo mengi ambayo kimsingi tunahitaji kuyachambua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nisisitize bado tuombe kubadilisha kanuni ili ikiwezekana taarifa hizi zije mapema tuzijadili kwa ajili ya kusaidia Taifa letu, kwa ajili ya kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipatia. (Makofi)