Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/2023. Nami kama walivyosema Wabunge wenzangu hapa, napenda kuendelea kuwapongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha bajeti hii vizuri kabisa na kuwasilisha kazi inayoendelea ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Nawashukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, kaka yetu Emmanuel Tutuba ambaye kwa kweli ni Katibu Mkuu msikivu sana na usikivu wake sisi tumeuona katika ufuatiliaji wa Barabara yetu ya Ifakara – Kidatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema kwenye bajeti hii kuna mazuri mengi sana, nikisema tutumie muda hapa wa kuyasema hayo mazuri tutamaliza dakika zetu, lakini tunaenda kutaja mazuri huku tukichangia.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, mimi kama Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuna mambo ambayo tunataka tuyapongeze na tuiombe Wizara ihakikishe kwamba, bajeti hii inafanikiwa na mambo haya yanafanyika, ili Serikali zetu za mitaa ziweze kufanya vizuri zaidi. Jambo la kwanza, nimemsikia Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti yake na nimesoma, anasema kuhusu uboreshaji wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani hasa katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, sisi katika Kamati ya LAAC maeneo mengi tumepita tumekuta kwamba, kitengo hiki ni kama kimekufa. Ni kwamba, ni kitengo tegemezi kwa Mkurugenzi ambaye wanamkagua na kumshauri. Sasa kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni wazi kwamba, kinaenda kuboreshwa Kitengo hiki cha Ukaguzi wa Ndani na kitakuwa indicator kubwa kwa CAG anavyoenda kukagua katika halmashauri zetu. Hilo ni jambo la msingi sana na tunamwomba Mheshimiwa Waziri kwa kweli kiboreshwe kama alivyosema, watafute fedha katika bajeti hii wahakikishe wanamwezesha CAG, kama walivyosema wamempa asilimia mia ya bajeti yake, basi na Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kwa Taifa na katika halmashauri kiende vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukomo wa bei. Sisi katika hesabu za Serikali za Mitaa huko, tenda na mambo mbalimbali, tumeona kwa kweli kama kuna sehemu hela zinapigwa basi ni katika tenda mbalimbali hizi za halmashauri zetu. Tumemsikia Mheshimiwa Waziri kasema kwamba, utaratibu wa ununuzi utakuwa na ukomo wa bei usiotofautiana sana na soko; basi tunashukuru na tunapongeza hatua hii itaokoa sana fedha za Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, mengine wamesema katika TEHAMA, mimi bado nasema TEHAMA ni muhimu sana katika dunia ya sasa ya sisi vijana. Hatuwezi kwa kweli, kuendelea kuogopa TEHAMA, tufanye mikutano, Mabaraza ya Madiwani, imeshindikana Waheshimiwa Wabunge kushiriki vikao vyote vya Mabaraza ya Madiwani. Pamoja na maelekezo mbalimbali ya Serikali kwamba, lazima tushiriki kama Wabunge katika vikao hivyo, lakini imeshindikana kwa sababu lazima vitaingiliana na ratiba za halmashauri, vitaingilina na ratiba za Bunge. Kwa hiyo, kwa kutumia hiyo TEHAMA itatusaidia sisi kushiriki, kwa hiyo, mimi naunga mkono jambo hilo lifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa tuliona matatizo makubwa ya kurejeshwa fedha katika miradi. Ikishafika 30 Juni, Wakurugenzi wa Halmashauri wanakuwa wanahangaika, wanahaha kuhakikisha kwamba, wanawahi hata saa nyingine kulipa bila utaratibu kwa sababu, fedha zitarudi kwenye mfumo. Tumemsikia Mheshimiwa Waziri anasema hilo halitakuwepo kwa sababu, hilo ni kuwaadhibu wananchi ambao hawana hatia.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine zuri ni Usajili wa Wakuu wa Taasisi kwa ushindani, kuwapa malengo ya taasisi na malengo yanayopimika, ni jambo zuri, kufuta ada ni jambo zuri, kuongeza bajeti ya kilimo kutoka bilioni 294 mpaka 954, ni jambo zuri. Hapa kwa kweli, nitapasemea huku mbele kwa sababu, naona hili ni jambo kubwa sana ambalo ningekuwa na uwezo ningemwambia Mheshimiwa Waziri wa Fedha, basi tarehe Mosi, Julai au tarehe 2 Julai, ampatie Waziri wa Kilimo hizi fedha zote ili akatekeleze bajeti ya kilimo kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mazuri ni mengi sana, lakini napenda kusema wazi kwamba, mimi kama kijana siwezi kuunga mkono suala la kuondoa 5% katika 10% ya mikopo ya vijana katika halmashauri. Kama walivyosema Wabunge wengine hapa haiwezekani, kwanza haieleweki. Mimi nina Ilani ya Uchaguzi nimesema hapa nimeisoma hii Ilani inaahidi kuhusu hiyo 10% na sisi tunatekeleza hii ilani sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Godfrey Chongolo, amezunguka hata juzi anasema kuhusu hiyo 10%. Sasa wale waliofanya ubadhirifu kukopa fedha hizi bila utaratibu wasisababishe fedha hizi zikaondolewa kwa vijana, Serikali iwawajibishe tena hata kule Kilombero, Morogoro tunao. Wawajibike waende Mahakamani wachukuliwe hatua wawajibike. Machinga ni watu wazuri sana, lakini tutafute vyanzo vingine mbadala vya kuendeleza masoko ya Machinga.

Mheshimiwa Spika, halmashauri ambayo ina mapato ya bilioni moja ukitoa 10% milioni 100, ukitoa 5% ni milioni 50, itajenga soko gani na 50 zinazobaki zitasaidia vijana wangapi? Kwa hiyo, nafikiri Mheshimiwa Waziri arekebishe katika paper yake hapo tuachane na jambo hili tuendelee kutekeleza ilani kuhakikisha kwamba, tuna 10% ile ya 4:4:2 kama ilivyo kawaida.

Mheshimiwa Spika, ziko falsafa zinatufundisha, pamoja na utekelezaji wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri, kufikiri nje ya box zaidi na kutazama bajeti zetu nyuma. Sidhani kama kuna bajeti ilishawahi kuja hapa Bungeni haikuwa na shamrashamra? Bajeti zote zina shamrashamra, bajeti zote zinapendeza, bajeti zote tunasema ni sawa, tunazisema vizuri, lakini tunafanya tathmini ya miaka mitano nyuma mathalani. Tunaweza tukasema korona hii ya juzi, vita ya Ukraine, lakini miaka mitano nyuma utekelezaji wetu wa bajeti ni asilimia ngapi? Ni vitu gani vinatukwamisha katika kuhakikisha hatufikishi asilimia 80 ya utekelezaji wa bajeti? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa si lazima Mheshimiwa Waziri, sijui kama hii 41 trillion ambayo tunaitafuta sasa hivi tutaipata na tutatekeleza kwa 100% ama asilimia 80 ama asilimia 90 sina uhakika, lakini kufikiri nje ya box ama falsafa ya kusema jikadirie kihalali, kama anavyosema Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson; lazima tujikadirie kwa kujiuliza miaka 10 nyuma je, tunajitazama kweli sisi kama Watanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu, hatuwezi kutaja bajeti zinazoongezeka tu tuonekane nchi yetu inaendelea, lakini utekelezaji haufiki 80%, lazima tujikadirie kihalali na ni lazima tufikirie nje ya box. Tazama 2016/2017 ilikuwa trilioni 25; mwaka unaofuata 2017/2018 ikawa trilioni 26; mwaka 2018/2019 ikawa trilioni 28; mwaka 2019/2020 ikawa trilioni 29; mwaka 2020/2021 ikawa 32; mwaka 2021/2022 ikawa 39; mwaka 2022/2023 tuna trilioni 41. Inaongezeka ndio, ni vizuri, lakini hata katika economics ya form five na six katika economics ya diploma, yuko baba yangu Mkenda atasema, walitufundisha aina tatu za bajeti na ziko nchi zinatumia aina nyingine za bajeti. Sasa kama nchi yetu tangu ipate uhuru inatumia aina moja ya bajeti, deficit budget kwamba, matumizi tunapanga mengi kuliko mapato, tuachane nayo na kwa ushahidi kwamba, hatufikishi asilimia 80. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wametufundisha kuna balanced budget kwamba, zipo nchi zinapanga matumizi sawa na mapato yao na kwa sababu, zina mipango ya maendeleo ikitokea fedha za IMF, World Bank na misaada mingine wanachukua, wana-click katika ile check list kitu gani tulipanga kufuata tukifanye tuingize pale na Watanzania ni waelewa, hiyo ni balanced budget kwamba, tunapanga matumizi sawa na mapato yetu.

Mheshimiwa Spika, tumefundishwa kuna surplus budget. kwamba, unaweza ukapata mapato mengi ukapanga matumizi kidogo, lakini ya mwisho hii deficit ambayo tunaing’ang’ania ya matumizi mengi kuliko mapato, ufanisi wake miaka mitano nyuma unaonekana haufiki 80%. Kwa hiyo, nasema kufikiri nje ya box, kujikadiria sijui hii 41 trillion iko wapi kwa sababu, tunakopa tena five trillion hapa tunaongezea kwenye hii bajeti. Hatuna uhakika kwa sababu, majanga yamekuwa majanga, Covid-19 itakuja Covid-42 itakuja ngapi, sisi tunaamini hizo nchi zitatupa hizo fedha tuongezee kwenye bajeti utekelezaji ukija hapa asilimia 60, asilimia 70 au asilimia 80. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania ni waelewa. Mathalan tunapata shilingi trilioni mbili kwa mwezi kutoka TRA. Kwa mwaka ni shilingi trilioni 24, mapato yasiyo na kodi shilingi trilioni sita, una shilingi trilioni 30. Mheshimiwa Waziri panga mipango yako katika shilingi trilioni 30 tuletee hapa tutoe vipaumbele vya kutekeleza asilimia 100. Peleka kwenye hizo Wizara kama tano za mfano, tutekeleze asilimia 100, tusonge mbele, watu wataelewa. Halafu on the way tukipata fedha za World Bank, UVIKO na kadhalika, tunakaa kama Bunge tunaeleweshwa, tunaendelea na mpango wetu wa Serikali wa miaka mitano. Hilo Watanzania watalielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mathalan tunahitaji shilingi bilioni 954 hii ya kilimo, hata Mheshimiwa Waziri Bashe apewe kesho. Ila kwa mfumo wa Wizara zote kupewa pewa fedha hivi, hakuna Wizara itatekeleza kwa hundred percent. Vipaumbele vya Taifa letu ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nasisitiza, katika kilimo hapa ni pazuri sana na vipaumbele vya Taifa vichache vya kutekeleza kwa asilimia 100 kwa kutegemea mapato yetu tuliyokuwa nayo ni ya uhakika, kuliko kwenda mwakani kwa sababu tuna fourty one, lazima tujikadirie kihalali. Tuna fourty one leo, mwakani tunataka tuwe na fourty five billion, how tunaipata na uchumi wa dunia unarudi chini?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri siyo lazima kufikiria zaidi ndani ya box tangu uhuru mpaka sasa hivi, ndani ya box tu, kwamba sisi surplus bajeti mwaka 2021 ilikuwa fourty one, tukiongeza fourty five ndiyo tutaonekana tunaendelea, no! Tuna uhakika gani na mapato ya nchi yetu ya uhakika ya TRA na mapato yasiyokuwa na kodi tukijumlisha tupange mipango hiyo, Watanzania watatuelewa.

Mheshimiwa Spika, uzuri wake, Mheshimiwa Rais Samia sasa hivi amesema vizuri sana, amekuwa muwazi na anakuwa kama ana mashaka na mambo ya mikopo. Wakati wa mikopo hii ya one trillion ya COVID amezungumza wazi, tumieni vizuri mikopo hii, Watanzania watalipa. Juzi tulikuwa tuna miradi 28 ya maji, amezungumza hivyo hivyo, amesisitiza kwamba tutunze sana fedha hizi za mikopo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri sana kwa kumalizia kuwa Mheshimiwa Waziri mwakani kama hii haitafika eighty percent, basi tufikirie bajeti ya kupanga kutokana na matumizi yetu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, tujikadirie tuje nje ya box. (Makofi)