Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya bajeti. Awali kabisa nipende kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu yeye ndiyo msimamizi mkuu aliyeweza kubuni mambo kama haya ambayo yamo katika bajeti hii inayomgusa mwananchi moja kwa moja. Vile vile nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake na hasa Mheshimiwa Waziri kwa kazi ambayo ameifanya namwona anafaa kabisa kuwemo ndani ya miongoni mwa wananchi. Hongera sana kwa Mheshimiwa Mwigulu kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu nitaulenga katika uchumi wa Taifa letu na nitajaribu kuupima na mapato ya kodi ya Serikali. Nimevutiwa sana kuona kwamba mapato ya kodi yameongezeka kwa asilimia18.5 ukilinganisha mwaka jana kuanzia Julai hadi Aprili na kipindi kama hicho cha safari hii na nikavutika kusema kwamba hebu niangalie mafanikio haya ya ongezeko la kodi za Serikali dhidi ya kitu wanaita Tax to GDP. Nilikuwa najaribu kuangalia huu uwiano wa kodi zinazokusanywa dhidi ya pato la Taifa, kwa sababu huko duniani hiki ni kipimo ambacho kinachotumiwa ili kuweza kuangalia kwamba Serikali inakusanya vya kutosha ili kuweza kuhimili matumizi yake ya Serikali pamoja na kuiletea maendeleo nchi hiyo na kuondoa au kupunguza umaskini.

Mheshimiwa Spika, nikaona kwamba kulinganisha vitu hivyo viwili huo uwiano wa hivi viwili nikarejea kwenye andiko, kuna taasisi moja inaitwa Action Aid, hawa walitoa andiko niliwahi kulisema linaitwa ceiling the gaps report la mwaka 2021, ambapo wao wanasema Tanzania yawezekana kuna trilioni 17.4 haikusanywi, wao wanasema hivyo. Sasa katika hilo nikajaribu kulinganisha pato la Taifa kwa miaka kadhaa kuangalia ukuaji wake, je, unaakisi ukusanyaji wa kodi. Nikaangalia mwaka 2015 Pato la Taifa lilikuwa trilioni 111. Nikaja 2016 trilioni 116, mwaka 2017 trilioni 124, mwaka 2020 trilioni 145 na kote huko maana yake kulikuwa na ongezeko mwaka hadi mwaka, lakini ukienda kwenye makusanyo bado tumebakia asilimia 11, sasa hii ikanionyesha nini?

Mheshimiwa Spika, hii ikatafsiri kwamba kipato cha mwananchi wa kawaida kinaongezeka na kwa kuwa kipato kinaongezeka hebu tuangalie mwaka 2015 pato la Mtanzania lilikuwa US Dollar 943 sawa na Sh.2,180,000.00, ukienda mwaka 2020 pato la mwananchi liliongezeka kwenda USD 176. Sasa kwakuwa kipato cha mwananchi kimeongezeka ni dhahiri kabisa ingeweza ika-translate kuongezeka vilevile kwa makusanyo ya kodi za Serikali lakini hatukusanyi vile inavyotakiwa tumebakia 11 kwa kipindi cha miaka 10. Sasa hali hii inaonyesha kwamba hatuwezi tukafikia malengo yetu ya kukuza uchumi ipasavyo, lakini vilevile kupunguza umaskini wa watu wetu, itatupa tabu sana. Nilikuwa nikiangalia Benki ya Dunia inasema nini? Benki ya Dunia inasema angalau watu wakusanye asilimia 15 ya pato la Taifa kama kodi ili tuweze kufikia malengo yetu.

Mheshimiwa Spika, sasa ukiangalia ulinganishi huo na sisi tunahitaji kuifanya nchi iwe ni competitive kwa maana tuvutie wawekezaji, tunatakiwa tufanye nini? TRA wao walikuwa wanaangalia mifumo yao, wanasema tuboreshe mifumo. Hili jambo tumelizungumza sana, mifumo ya TEHAMA izungumze, kwenye kila eneo ambalo linahusiana na ukusanyaji wa mapato, hilo nakubaliana nao. TRA wanasema waboreshe shughuli za forodha na hiyo ni kweli tunahitaji kuboresha shughuli za forodha kwa maana ya vitu vinavyoingia, utunzaji kodi wake na uandishi wake kwa kupitia TEHAMA hiyo ni sahihi.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo pia la matumizi ya EFD tumelizungumza sana masuala ya EFD kuhakikisha migogoro ya kikodi tumeizungumza sana fedha zilizopo kule kwenye mahakama trilioni tano na ushee, nyingine zilipo kwa Kamishna General wa TRA, zipo nyingi tu kule zaidi ya trilioni 300, sijui, zinazosemwa, elimu ya kodi hiyo inafanyika, lakini haya mambo yalikuwa yamezungumzwa humu yapo yanafanyika, lakini hatupigi hatua sasa tunataka tufanye nini?

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, nilikuwa naingalia Sheria ya Tax Administration, utaniruhusu niseme tax administration inahitaji kufumuliwa ili iwepo mipango bora ya kuhakikisha kwamba tunatanua wigo wa walipakodi. Suala hapa si kuongeza vima, tatizo la sisi wananchi wa Tanzania hasa upande wa Serikali wanam-target yule anayelipa kodi wanayemwona leo hiyo ni asilimia 10, kesho ni asilimia 12, asilimia 13 kama njia ya kupandisha mapato ya Serikali. Huo utaratibu ni mbaya kwa sababu watu wengi na watalaam wanasema less is more, weka vima vidogo ili iwe rahisi kufanya compliance na wengi wataweza kulipa kodi. Ukiwawekea vima vikubwa Watanzania sisi tunaitwa wabongo, tutafuta njia ya kupenya na kupenya kwenyewe aidha tusilipe kodi, tukimbie ama tutafute njia nyingine ambazo si sahihi kwa mujibu wa sheria. Hivyo, Serikali iangalie utaratibu mzuri, tanua wigo, kodi iwe chini, hapo utawapata wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tuwekeze katika mifumo na namshukuru sana mwananchi Mheshimiwa Mwigulu, kwamba tulivyolisema hili mara ya kwanza wakati nipo katika kujadili hotuba ya Waziri wa Fedha katika Wizara yake nililizungumza hili na nafurahi kuona TRA walitufanyia semina juzi tu hapa juu ya mifumo na ule mfumo wa IDRAS ambao nilikuwa nauzungumzia wameuchukua kwa nguvu sana na wamekwenda kuufanyia kazi. Kwa hilo niipongeze Serikali na wawekeze katika mifumo mingine ili mifumo hii iweze kuongea.

Mheshimiwa Spika, nataka niongezee neno lingine, waboreshe mifumo ya property tax, mambo ya mfuto tuachane nayo yalishazungumzwa hayo sitaki niongeze sana, lakini tuthaminishe majengo ili kila mtu alipe kwa uwezo wake. Tuwekeni scanners huko kwenye maeneo yetu ya mipakani na naamini kabisa kutakuwa na ufanisi mwingine.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo ambalo linazungumzwa sana, ni uzito wa kufanya biashara na nataka nijikite kwenye hizi tax audits ambazo huzaa interest na huzaa penalties, kiasi kwamba mfanyabiashara hatimaye anashindwa kulipa kodi kwa zile kodi ambazo atakuwa hajazilipia. Sasa nilikuwa nashauri tax audits Mheshimiwa Waziri ananisikiliza, angalau zifanyike kwa mwaka mara moja badala ya kusubiri miaka mitatu. Ukisubiri miaka mitatu interest na penalties zinakuwa kubwa, mtu hawezi kulipa, anafunga biashara na akifunga biashara ni hasara kwa Serikali. Kwenye hili natarajia kuleta schedule of amendments kuweka sharti la kisheria kwamba TRA ifanye audit cycle angalau mara moja kwa mwaka na wakikosa angalau iwe ni miaka miwili ili kupunguza mzigo wa kutengeneza interest na penalties.

Mheshimiwa Spika, lingine misamaha isiyo na tija. Hakika hili ni jambo ambalo limezungumzwa kwa muda mrefu sana. Ipo misahama mingine haitusaidii kama Serikali, haitusaidii kama wananchi. Kwa mfano, tulitoa msamaha kwaajili ya simu janja kuondoa VAT, bei haikupungua, bei imebakia palepale, misamaha kama hii inanufaisha sana wafanyabiashara. Tulitoa misamaha samahani kwa taulo za kike, lakini bei haikushuka, wanaofaidi ni wafanyabiashara. Unaweza ukatoa msamaha kwenye jambo ambalo pengine halina manufaa kwa mwananchi kama kupunguza au kuondoa kodi kwenye kutengeneza mitungi ya gesi, anayefaidi ni mwenye kiwanda tupunguzie kodi ya gesi ambayo mwananchi anaitumia. Sasa misamaha ambayo haina tija tuondokane nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, tuboreshe sekta isiyo rasmi. Sekta isiyo rasmi ni kundi kubwa hata hilo la Wamachinga tunalozungumza ni sekta isiyo rasmi. Uwepo mfumo ambao utafanya sekta isiyo rasmi kutambulika iwe rasmi na waingizwe katika mifumo ya kikodi, nao waweze kuchangia katika pato la Taifa lao pamoja na kodi za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa katika jambo kama hili napenda sana kuona kwamba tunaliendea kwa ukamilifu wake kuhakikisha kwamba Serikali Kuu pamoja na Serikali za Mitaa zinafanya kazi kwa pamoja. Kivipi? Tuna tatizo sasa hivi la watu wa kodi kufikia kila biashara. Nililisema hili na bahati nzuri TRA wakapeleka vijana 250.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naunga mkono hoja hii. Ahsante sana. (Makofi)