Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii na mimi kuchangia katika hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, Rahim, kwa kutuwezesha kujadili hapa katika hali ya uzima na afya, lakini pili nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini kuendelea kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tatu, naomba nikushukuru wewe Spika na nikupongeze sana kwa kazi nzuri ambayo unaifanya, na hili, wote ni mashahidi na tunaamini kwamba, kwa mujibu wa tafiti wanawake wanapopewa nafasi ama wanapokuwa na nafasi hawajawahi kushindwa, kwa hiyo, nawapongeza sana, lakini pili wanakuwa ni waaminifu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nimpongeze na nimshukuru pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Makamu wake na Wajumbe wenzangu wote kwa namna walivyotupa ushirikiano mkubwa katika suala letu hili, lakini niwashukuru pia Wabunge wenzangu kwa ushirikiano wao wote na michango yenu yote ambayo mmeitoa. Ni michango yenye afya, yenye dhamira ya kujenga Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru pia Waziri wangu, Waziri wa Fedha na Mipango, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, yeye kwangu huyu ni mentor yaani ni kocha mzuri ambaye anatupa maelekezo na tunaenda vizuri na kufanya kazi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru pia watendaji wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kiasi kikubwa sana ambapo wanatupa ushirikiano katika kazi zetu za siku hadi siku wakiongozwa na Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu, Makamishna na watendaji wote.

Mheshimiwa Spika, nijielekeze tu moja kwa moja katika mjadala ama hoja ambazo zimejadiliwa hapa leo na nianze na maoni ya Kamati; Kamati iliona kwamba tuna uhaba mkubwa wa wafanyakazi ama watumishi wa TRA.

Mheshimiwa Spika, hili nikiri ni kweli kwamba TRA watumishi wetu bado ni haba, lakini Serikali imechukua juhudi mbalimbali za kuongeza watumishi hao. Ndani ya mwaka huu Serikali imedhamiria kuajiri vijana 2,100 na tayari vijana 1,443 wamesharipoti kazi na wameshapatiwa mafunzo ya kiutendaji na 657 wamo katika mchakato wa kupatiwa ajira ndani ya mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, ipo hoja imezungumzwa kuhusu mali chakavu au vyuma chakavu. Baadhi ya watu wanaziita mali kachara. Ni kweli zipo na mchakato ule unaonekana ipo haja ya kufanyiwa mapitio. Hili tumelichukua na tutalifanyia mapitio ili kusudi mauzo ya mali kachara ama vyuma chakavu vile yaende kwa haraka sana katika mchakato wake.

Mheshimiwa Spika, lakini pia naomba nizungumzie suala la forodha ambalo amezungumza ama ametoa maoni Mheshimiwa Mbunda, jirani yangu pale kwamba ipo haja ya kufungua ama kuweka Ofisi za Forodha katika mipaka yetu.

Mheshimiwa Spika, hili tumelichukua na tayari limeanza kufanyiwa kazi na Serikali. Sasa hivi Serikali, iko timu maalum ambayo imeundwa inafanya tathmini ya sehemu kwa mfano kama vile Momba na sehemu nyingine kuona kwamba kama ipo haja ya kufungua Ofosi za Forodha latika mpaka fulani, basi Serikali haitasita na ipo tayari kutufua Ofisi za TRA katika mipaka yetu hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nizungumzie suala la ukusanyaji wa mapato ambayo Mheshimiwa Tarimba kwa kiasi fulani amegusa kidogo kwamba ipo haja ya kutanua wigo nalo hilo pia limechukuliwa na Serikali na Serikali imefanya juhudi hizo hata kama alivyosema yeye mwenyewe vijana 360 wamechukuliwa kuwekwa kwa muda, siyo waajiriwa lakini wanasaidia ukusanyaji wa fedha na kutoa taaluma kwa wafanyabiashara wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)