Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia kwenye hotuba ya Wizara ya Fedha na Mipango. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha leo kusimama asubuhi hii.

Mheshimiwa Spika, nianze moja kwa moja kwa kuipongeza Wizara ya Fedha na Mipango katika utekelezaji wa kazi zake na kazi ambazo ningependa leo kuwapongeza mahususi ni usimamizi wa bajeti ya Serikali na kuratibu upatikanaji wa fedha kutoka taasisi za fedha za kikanda na kimataifa. Kwa nini naipongeza kwenye usimamizi wa bajeti za Serikali, bajeti hii ni ya kwanza kwa Serikali ya Awamu ya Sita, lakini tumeshuhudia Wizara mbalimbali zilivyowasilisha bajeti yao hapa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/2022, zimeonesha Wizara nyingi zimepata kiwango kikubwa cha mafungu yaliyokadiriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia hata hali ya makusanyo, lakini pia na matarajio. Lakini pia katika uwasilishaji wa bajeti za Wizara tumeziona zile Wizara za kimkakati za kuchangia katika kuona mapato ya Serikali yanapatikana mfano Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara zingine namna gani Waziri wa Fedha na Naibu wake…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, pamoja na Wizara zingine zilivyojikita katika majadiliano ya kuona ongezeko la bajeti ya Wizara hizo mahususi ili zitoe mchango katika ukusanyaji wa mapato.

SPIKA: Mheshimiwa Subira Mgalu kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nilikuwa nataka nimpe taarifa tu kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita hii ni bajeti yake ya pili sio ya kwanza kama alivyosema. (Makofi)

SPIKA: Ni bajeti yake ya kwanza kwa sababu ile nyingine maandalizi yake yalianza tangu Novemba, 2020 huko. Kwa hiyo yuko sahihi Mheshimiwa Mbunge. Ndio maana jamani si kifo kilitokea Machi na Machi tulikuwa tuko kwenye Kamati, huwezi kusema hii ni Kamati yake ya pili kwa hiyo, yuko sawa sawa huwezi kusema hii ni bajeti yake ya pili.

Mheshimiwa Subira Mgalu endelea na mchango wako. (Makofi)

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunisaidia.

Kwa hiyo, nilikuwa nataka niseme tulivyosikiliza bajeti za Wizara mbalimbali tumeona namna Wizara hii ya Fedha na Mipango ilivyowezesha Wizara hizo, kutekeleza bajeti ya mwaka 2021/2022 lakini na mipango thabiti ya bajeti ya mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo nimeona pia nipongeze kwa namna ambavyo imeratibu upatikanaji wa fedha kutokana na Taasisi za Kimataifa na za Kikanda na mahususi mkopo wa shilingi trilioni 1.3 ambao hauna riba na utalipwa baada ya miaka 10 na tija iliyopatikana kutokana na mkopo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa nimpongeze kipekee Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza mazungumzo yanayowezesha Taasisi hizi za fedha, kutoa fedha/mkopo wa bei nafuu kwa Serikali yetu na hivi karibuni pia tumesikia kazi nzuri tunatarajia kupata shilingi trilioni 1.2 kutoka kwa IMF. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo lakini pia naomba mchango wangu utajielekeza kwenye Mamlaka ya Mapato (TRA). Naomba niipongeze sana kwa kazi nzuri, mpaka Aprili, 2022 imekusanya zaidi ya asilimia 97 na hapa naomba nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa uteuzi wako wa kuniteua mimi kuwa Balozi, Mamlaka ya TRA imekuwa ikitutumia kikamilifu kuhamasisha kulipa kodi kwa hiari. (Makofi)

Niipongeze Idara ya Mawasiliano kwa Umma na Elimu kwa Mlipakodi kwa kazi inayofanywa mikoa mbalimbali na kampeni ya Mlango kwa Mlango Kamata wote Matumizi ya EFD. Lakini niishauri Serikali tunapopita kuhamasisha malipo ya kulipa kodi kwa hiari kwanza Watanzania au wafanyabiashara wanaishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Fedha kwa kuifanya TRA kuwa kimbilio na kwamba wanawa-engage katika mazungumzo na mipango mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wanaomba ikiwezekana TRA au Serikali iangalie utoaji wa mashine hizi za EFD iwe bure ili ishawishi Watanzania wengi kuwa na hizo mashine, lakini itasaidia kuongeza kwa kiwango kikubwa malipo ya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo niishauri Serikali itumie Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Idara za Biashara na Serikali za Mitaa na wale Wakuu wa Idara kwa sababu mfanyabiashara lazima apate leseni, kwa hiyo kupitia leseni Serikali itakuwa na uhakika wa kupata mapato yake.

Mheshimiwa Spika, lakini nishukuru sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu amevunja rekodi kwa kutoa vibali vya ajira. TRA imeajiri wafanyakazi zaidi ya 1,000 kuelekea 2,000 wamepata semina nzuri, tuna matarajio na sisi Mabalozi tutaungana nao mlango kwa mlango kuhamasisha malipo ya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo nichangie kwenye Idara nzima ya Ukaguzi wa Ndani. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na jitihada za Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Wizara hii ya Fedha kutafuta fedha, lakini kama haitaimarisha kwa nguvu Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Ndani kwa kweli matumizi mahususi ya fedha hizi ili yafanye value for money tunaomba idara hii iwezeshwe. Lakini hata hizi Kamati za Ukaguzi (Audit Committee) kama ambavyo imeshauriwa na Kamati yetu naunga mkono maoni yote ya Kamati na kazi nzuri iliyofanywa, kupitia uwezeshaji wako tunaomba muundo wa Audit Committee utazamwe upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kati ya wajumbe watano watatu wanatoka ndani ya Taasisi na wanateuliwa na Afisa Masuhuli na kwa kuwa kikao kinaweza kikafanywa na wajumbe watatu tu, ambao ripoti yao inapelekwa kwa Afisa Masuhuli hapo Serikali itazame hili kwa nia ya kurahisisha utendaji wa kazi. Lakini kwa kuwa pia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Ukaguzi wa Umma, anaweza aka-rely katika kazi ya Mkaguzi wa Ndani na inaweza ikarahisisha pia kazi ya Mkaguzi wa Nje naiomba Serikali iimarishe ofisi hii kwa fedha, kwa vitendea kazi, lakini ikiwapendeza iwape vote yao ili iwe huru na ifanye kazi iliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo naomba nichangie Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG). Naishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha imekuwa ikiipatia fedha, lakini naomba iendelee kuiwezesha kutokana na kazi zilizoongezeka, miradi mbalimbali ya kimkakati na kaguzi mpya mfano real time audit (ukaguzi wa ufanisi) iwezeshwe fedha ili iweze kufanya kaguzi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali iwasimamie Maafisa Masuuli Serikali mnapata doa, kutokana na uzembe wa baadhi ya Maafisa Masuuli. Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali anapokwenda kukagua anafanya interest conference anaeleza atakagua kwa mawanda ya aina gani (sampling yake) na anapoondoka anafanya exit conference anaacha hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na sheria imetaka ndani ya siku 21 hoja zijibiwe, lakini leo Maafisa Masuuli, wahasibu) wanachukua muda mrefu na hatimaye, hoja zinaendelea na kuwepo kwenye CAG Report inaonesha kwamba kuna upotevu mkubwa wa fedha, kumbe si kweli. Kwa hiyo, Serikali chukueni hatua kali katika hawa ambao hawatimizi wajibu wao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya kengele ya pili imeshagonga.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na ninakushukuru kwa kunipa fursa hii, ahsante sana kwa uongozi wako uliotukuka. (Makofi)