Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninakushukuru tena, asubuhi nilipata fursa ya kukupongeza na kukushukuru kwa bahati mbaya ulikuwa kwenye majukumu mengine mazito ya Kitaifa.

Mheshimiwa Spika, ninachukua fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, ninaishukuru sana Kamati ya Bunge ambayo imekuwa ni mshauri mzuri wa Wizara hii, tumepokea maelekezo, tumepokea maoni yote ya Kamati na yale maeneo yenye mapungufu mawili, matatu tayari Naibu Waziri amekwisha yatolea ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, siku ya leo kumekuwepo na wachangiaji zaidi ya 20 na wachangiaji wengi toka asubuhi wamekuwa wakitupongeza Wizara, hivyo Wizara tunalichukua hilo kama deni ili tuende tukafanye vizuri zaidi. Ukiangalia maelezo yetu Wizara, hotuba yetu imejikita katika taarifa ambazo kwa kweli msingi wake ni Bunge, ndiyo maana tunaipongeza sana Bunge, tunawapongeza sana Wajumbe wa Kamati wakiongozwa na Mwenyekiti mahiri kabisa Mheshimiwa Stanslaus Nyongo kwa kutushauri, kwa kutupa maoni na kimsingi naomba niwaambie Watanzania kwamba Wizara hii itaongozwa na ubunifu, Wizara hii itaongozwa na weledi pia Wizara hii itaongozwa na uchapakazi.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni Wizara ya wananchi kwa msingi wake kwa sababu wananchi wanaitegemea izara hii katika kuleta furaha na faraja, kwa mantiki nyingine Wizara hii ni Wizara ya furaha na faraja kwa Watanzania. Jukumu letu kubwa tutaiponya mioyo ya Wasanii. Ninaahidi mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba tunakwenda kuponya mioyo ya wanamichezo pia tunakwenda kuimarisha utamaduni, hivyo haya naomba niweze kuyaweka vizuri kabisa katika Bunge lako Tukufu kwamba tutakwenda kuchapa kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba ile kazi ambayo tuliianza nayo tunakwenda nayo mbele ili Kwenda kuleta faraja kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja chache ambazo Naibu Waziri hakupata fursa ya kuzitolea ufafanuzi wa kina, hapa ninaomba nitoe ufafanuzi wa baadhi ya hoja chache ambazo ninaamini Watanzania wanatamani kuzisikia. Imeibuka hoja hapa kuhusu suala la ZFF, FIFA, CAF na TFF. Eneo hili Wizara tunahitaji kuendelea kulifanyia kazi sana ili Watanzania waweze kuwa na furaha kwa pande zote mbili. Ninachukua fursa hii kulitangazia Bunge lako Tukufu kuwa kwa mara ya kwanza kabisa katika historia, tumekuwa na ushirikiano wa karibu kabisa baina ya Wizata yetu ya Michezo, Utamaduni na Sanaa pamoja na Wizara ya Michezo ya Zanzibar, tumeshirikiana na karibu sana, nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa Michezo Zanzibar, amefanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba timu yetu ya Serengeti Girls iliweka kambi Zanzibar toka tunaanza mashindano ya kulekea Kombe la Dunia, kwa hiyo ninawapongeza sana Viongozi wa Zanzibar, leo nafikiri tulikuwa nae Rais wa ZFF hapa Bungeni. Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia miongoni mwa Wajumbe ambao niliwateua kuingia katika Baraza la Michezo BMT, mmoja wa Wajumbe katika Baraza la Michezo anatoka Zanzibar. Pia tumewashirikisha wenzetu kutoka Zanzibar katika baadhi ya Kamati mbalimbali muhimu za nchi yetu katika kuendeleza michezo hapa nchini, hivyo Wizara tunashirikiana vizuri.

Mheshimiwa Spika, lazima tukiri kazi kubwa inayofanya na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, pia ni lazima tupongeze na tukiri kazi nzuri inayofanywa na Rais wa Awamu ya Nane wa Zanzibar, ni kazi kubwa na nzuri. Tunaliahidi Bunge lako Tukufu kwamba eneo hili tutakwenda kulifanyia kazi, msemo ambao napenda niutumie hapa ni kwamba hakuna mkate mgumu mbele ya chai, hivyo katika Wizara hii hakutakuwa na jambo gumu, kila jambo tutahakikisha tumelifanyia kazi na kulitatua kwa mustakabali wa Taifa letu. Hivyo naomba niwashauri Waheshimiwa Wabunge wasiwe na wasiwasi kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo lilizungumzwa hapa ni kuhusu Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake (TWFA) kwamba kifanye uchaguzi. Watanzania wanataka mabadiliko, wanataka mabadiliko katika sekta ya michezo, eneo hili ninatambua Mheshimiwa Mbunge amelizungumza hapa, lakini kwa mujibu wa taratibu na kwa mujibu wa miongozo, utaratibu wangu ni kufuata utaratibu. Ninatambua Mheshimiwa Mbunge anaweza asiridhike na majibu haya lakini siwezi kuwa na majibu mazuri ya kumfurahisha zaidi ya haya ninayoyasema sasa.

Mheshimiwa Spika, inawezekana huko nyuma wenzangu hawakufuata taratibu lakini mimi nitanyooka kwenye taratibu. Ninawathibitishia kabisa kwamba TWFA haina wanachama katika baadhi ya Wilaya, haina wanchama walisajiliwa katika baadhi ya Mikoa, tayari nimeshawaagiza wenzangu katika Mikoa na Wilaya kuhakikisha kwamba wanaharakisha michakato ya kupata wanachama wa TWFA ili tuweze kuwapata Viongozi ambao wamechaguliwa katika misingi ambayo wanachama wao wenyewe wamewachagua. Kwa hiyo, inawezekana nisiwe na majibu mazuri hapa, lakini ninawathibitishia Waheshimiwa Wabunge, inawezekana tulikuwa hatufanyi vizuri kwa sababu tulikuwa hatufuati utaratibu.

Mheshimiwa Spika, nyakati zangu hizi tutahakikisha tumejikita katika misingi ya kufuata taratibu ili tuweze kufanya vizuri. Ninakuomba Mheshimiwa Mbunge ninatambua majibu haya hayawezi kukufanya ushindwe Ubunge lakini sitakuwa na majibu mazuri zaidi ya haya ninayokuambia kwamba watu wafuate taratibu nami nitajikita katika misingi ya taratibu. Hayo ndiyo majibu yangu kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la Uwanja wa Dodoma, Serikali yetu ya Awamu ya Sita imedhamiria hakika katika kuhakikisha kwamba uwanja wa Dodoma unajengwa. Ninaomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba dhamira na ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba Tanzania tunaendesha mashindano ya Afrika ya mpira wa miguu ifikapo mwaka 2027, hizi ndizo ndoto za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Katika maeneo ambayo Wizara yetu imeyapa kipaumbele ni ujenzi wa uwanja wa Dodoma. Naomba niwathibitishie Wabunge kwamba Wizara hii itaongozwa na mikakati, itaongozwa na weledi na uchapakazi, hatutajikita katika sehemu ambayo tumefungwa na bajeti tu. Viongozi katika Wizara hii tumekubaliana kila mmojawepo kuhakikisha anachapa kazi, tunajiongeza tusifungwe na mipaka ya bajeti tuliyonayo, huu ndiyo msingi ambao nimeujenga katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika Wizara tayari tumeshafanya vikao kadhaa na wadau wa michezo. Naomba nilitaarifu Bunge lako kwamba tayari tumepokea wadau mbalimbali wa michezo zaidi ya Saba ambao wako tayari kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa uwanja wa Dodoma na tayari tumekwishaonesha michoro ya uwanja wa Dodoma, mchakato wetu ni kuhakikisha kwamba uwanja huu umejengwa ndani ya miezi 17, pengine baada ya kuahirishwa kwa Bunge hili Tukufu tutaendelea na michakato ya kumpata mdau ambae atashirikiana na Serikali katika ujenzi wa uwanja huu.

Mheshimiwa Spika, naomba niwathibitishie Watanzania wote kwamba Dodoma ndiyo Makao Makuu ya Nchi, tutahakikisha kwamba tunajenga uwanja wa kisasa, siyo uwanja tu wa kawaida, nimewaagiza wenzangu, tumepokea michoro ile ya awali lakini tumesema kwamba hatuwezi kuwa na uwanja ambao unatumika tu kwa ajili ya mpira wa miguu, tunataka tupate uwanja ambao utakwenda kutumika katika kuendesha mikutano mbalimbali, kuwepo na shopping mall ndani, maduka mbalimbali pia kuwepo na ofisi. Dhamira yetu ni kujenga uwanja wa kisasa kabisa, hii ndiyo ndoto ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba uwanja wa Dodoma umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu kodi kati ya timu ya Yanga na Simba ambalo limezungumzwa hapa, Wizara tayari tumekaa na Wizara ya Fedha nae neo hili ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wasiharakishe kwa sababu tayari Waziri wa Fedha amelichukua na pengine kwa kuwa tunae siku ya kesho hapa ataweza kulitolea ufafanuzi wa kina kabisa eneo hili la kodi kwa sababu linaangukia katika Wizara yake, lakini mimi Waziri mwenye dhamana kwenye eneo hili tutaendelea kushirikiana na Waziri wa Fedha kuona ni namna gani tunaleta nafuu kwa Watanzania ambao wamejitolea kuendesha michezo hapa nchini hasa timu hizi kubwa za Yanga na Simba. Tumelipokea suala hili na tutakwenda kulifanyia kazi, ninaamini kwamba kwa kuwa maandalizi ya Finance Bill yanaendelea Waziri wa Fedha atakuja kulitolea ufafanuzi wa kina kabisa eneo hili. Serikali tumelipokea na tutakwenda kulifanyia kazi kwa maslahi na maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la ujenzi wa Arena, viwanja vya sanaa, naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba tayari Wizara imeshakaa na Wadau mbalimbali ambao wamejitokeza kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa viwanja vya Sanaa. Tunakwenda kujenga viwanja ambavyo pengine kwa mara ya kwanza Afrika vitakuwa ni vizuri na bora kuliko viwanja vyote Afrika. Kwa Mkoa wa Dar es Salaam tunategemea kujenga uwanja ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua na watu 16,000 mpaka 20,000 pia kwa Mkoa wa Dodoma tunakwenda kujenga uwanja utakaochukua watu takriban 15,000. Eneo hili michakato yote imekamilika, michakato ya maongezi na wadau imekamilika, hatua ambayo tumebakiza hivi sasa ni ya majadiliano baina yetu na wadau ili kuweza kuona ni namna gani tunaweza Kwenda nalo na kulikamilisha eneo hili, lakini Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inayo dhamira ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba tumejenga Sports and Arts Arena.

Mheshimiwa Spika, Rais wetu kwa mara ya kwanza ifikapo mwaka 2023 pengine anategemea ku-host mashindano ya kutafuta wanasanaa bora hapa Afrika, MTV Music Awards. Kwa mara ya kwanza kabisa Afrika ni dhamira ya Mheshimiwa Rais anataka kuona pengine mashindano ya kuwatafuta wanamziki bora yamefanyika katika viwanja vyetu vya Sanaa. Hili tunaenda kulifanyiakazi Pamoja na wadau kuhakikisha kwamba Serikali imetekeleza eneo hili.

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa hapa eneo la COSOTA kuhusu mirabaha. Wizara ni lazima tukiri mapungufu ambayo tumeyaona kwenye eneo hili la mirabaha. Tumeshauriwa na Kamati pia Waheshimiwa Wabunge hapa wamelizungumza suala hili kwa kina kabisa wakibeba maono na maoni ya Wasanii nchini. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kama ambavyo nimesema awali, yapo mambo makubwa ambayo tumekwishaanza kuyafanya, katika eneo hili naomba niwaambie wenzangu akiwemo Mheshimiwa Babu Tale, kwamba mkate mgumu utawezekana mbele ya chai. Eneo hili ni dogo sana, tutakwenda kulifanyia kazi. Mimi kama Waziri nimepata fursa ya kukaa na kuzungumza na Mameneja wa wanaoendesha kampuni ya Wazafi, nimezungumza nao. Nimezungumza na viongozi wao, Babu Tale mwenyewe, nimezungumza na Meneja Mkuu anayemsimamia Diamond Platnumz, pia nimezungumza na Diamond mwenyewe ili tuweze kwa pamoja kushikamana, tuzungumzie kero zetu na tuweze kuzitatua. Nimefanya mazungumzo hayo ili kwa pamoja tuweze kuleta manufaa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto hizi na tayari Mheshimiwa Rais amekwishatupa maelekezo tarehe 31 Mei, kwamba tuhakikishe tunakwenda kuzimaliza changamoto hizi. Nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba tayari nilikwishatoa maelekezo kwa COSOTA kuhakikisha inashirikiana na wadau mbalimbali kutafuta mfumo mzuri ambao utatoa haki ili kila msanii mwenye haki aweze kupatiwa haki yake. Kwa hiyo hili tumelipokea na tutakwenda kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, Mheshimiwa Sanga amelizungumzia hili eneo la ujenzi wa viwanja akitoa nukuu za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu, kwa mwaka huu wa fedha tunakwenda kukarabati uwekaji wa nyasi bandia na ujenzi wa viwanja vya kisasa kabisa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, naomba nilitangazie Bunge lako tukufu kuwa, tunakwenda kuweka nyasi bandia na kukarabati Uwanja wetu wa Jamhuri wa Dodoma. Kwa mwaka huu wa fedha tunakwenda kukarabati, ukarabati mkubwa ikiwa ni pamoja na kuweka nyasi bandia katika Uwanja wetu wa Sokoine, Mbeya. Naomba nilithibitishie Bunge lako tukufu kwamba tunakwenda kukarabati pamoja na kuweka nyasi bandia katika Uwanja wetu wa Sheikh Amri Abeid kule Arusha. Naomba nilithibitishie Bunge lako tukufu kwamba tunakwenda kuweka nyasi bandia na kuboresha Uwanja wetu wa Mkwakwani uliopo kule Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nilithibitishie Bunge lako tukufu kwamba tunakwenda kuweka nyasi bandia na kukarabati Uwanja wetu wa Kirumba ulikoko kule Mwanza. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwa kiasi cha fedha ambacho Mheshimiwa Rais ametupatia kupitia Wizara ya Fedha tunakwenda kufanya ukarabati mkubwa katika Uwanja wetu wa Benjamin Mkapa pamoja na Uwanja wetu wa Uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndoto za Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha kwamba Taifa letu linaendesha mashindano ya Afrika (AFCON) ifikapo mwaka 2027. Hii ndiyo sababu tumeanza kutenga kiasi cha bilioni kumi kwa ajili ya ukarabati mkubwa katika viwanja vyetu hivi. Tunakwenda kuweka nyasi bandia lakini pia tunakwenda kukarabati miundombinu ya ndani katika viwanja vyetu hivi.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kutoa hoja. Ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naafiki.