Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja ya Wizara yetu siku ya leo. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetujaalia afya njema sisi sote humu ndani kuweza kuiona siku hii lakini tukiwa na afya njema.

Mheshimiwa Spika, lakini pili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kuendelea kuniamini kuwa Naibu Waziri katika Wizara hii. Mheshimiwa Rais nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishukuru pia Wabunge wenzangu ambao wewe unatuongoza katika Bunge hili tukufu kuendelea kuwa washauri katika Wizara yetu, siyo washauri tu, lakini wewe binafsi wewe pia ni mwanamichezo mwenzetu, lakini pia na Waheshimiwa Wabunge wenzetu ambao pia mmetukumbusha katika hotuba yetu kuwaweka pale ambapo tumesahau mtuwie radhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishukuru Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambayo imekuwa ikitusimamia na ikitushauri kwa niaba ya Bunge zima katika masuala mbalimbali kwa ajili ya Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nimshukuru Waziri wetu, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, amekuwa kiungo kwetu sisi wasaidizi wake, lakini amekuwa akitushauri kwa upendo, amekuwa akitusisitiza tushikamane sisi kama Wizara na wasaidizi wake tumekuwa na amani sana kufanya naye kazi na ndiyo maana mambo yanakwenda, Mheshimiwa Waziri tunakushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Babati Mjini ambao wameendelea kuniamini na kunifanya Mbunge wao, niwaahidi kwamba jambo letu la maendeleo liko palepale na tutafikia Inshallah Mwenyezi Mungu atutangulie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishukuru familia yangu kwa maombi yao lakini pia watanzania kwa maombi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache kwa shukrani naomba sasa nipitie kwa haraka haraka baadhi ya hoja za Kamati na hoja Waheshimiwa Wabunge wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja namba moja ambayo nilitaka kuzungumzia ambayo imetokana na Kamati ni hoja inayosema kuibua vipaji vya michezo, Serikali ina mkakati gani. Mikakati yetu tumeeleza pia katika hotuba Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri, lakini nitaje baadhi. Baadhi ya mikakati tuliyonayo ni pamoja na kuanzisha shule maalum kwa ajili ya michezo, hizi academy za michezo 56 kote nchini. Lakini mnakumbuka Mheshimiwa Rais pia alituelekeza kwamba turudishe Taifa Cup ambayo ilichezwa mwaka jana na mwaka huu pia tuko kwenye ratiba hiyo. Lakini pia kupitia Taifa Cup tumekwenda tena mwaka huu kwenda mtaa kwa mtaa ndiyo mpango wetu tumesema kwenye bajeti yetu, kuhakikisha kila mtaa, kila kata tunaenda kuibua vipaji na ndiyo maana tunaomba bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni uwekezaji katika wataalam ya michezo, Kamati imeshauri na imesisitiza jambo hili, sisi kama Wizara tumeona ni jambo la msingi sana kwa sababu tukiibua vipaji toka kwenye ngazi za chini lazima tuwe na wataalam. Ndiyo maana katika mpango wetu huu na Waheshimiwa Wabunge wenzangu mmeona tumeweza kuweka fedha kwenye Chuo chetu cha Malya, kuhakikisha kwamba kozi pale zinatolewa. Lakini pia wanachuo wanaokwenda pale tunawajengea hosteli waweze kutulia, wapate mafunzo tukishirikiana na Wizara ya Elimu kwa upande wa mitaala. Kwa hiyo, Wizara imeshaona hili lakini pia tunashirikiana pamoja na mashirikisho, BMT tunashirikiana nao ili kuhakikisha kwamba wataalam hawa wanapatikana.

Kwa hiyo, sisi tushukuru Bunge lako tukufu limeendelea kututengea fedha kupitia Wizara hii kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Michezo. Kazi mojawapo ya kuhakikisha kwamba fedha hizi zinatumika vizuri ni pamoja na kuibua wataalam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingine la usimamizi wa vyama na mashirikisho liachwe kwa wadau wenyewe. Hili jambo sasa ndivyo lilivyo, sisi kupitia BMT, kupitia Msajili wa Vyama vya Michezo tunasimamia katiba zao na tunahakikisha kwamba wanachama wanatendewa haki na Mheshimiwa Waziri alishamteua Msajili, mwanzoni tulikuwa hatujampitisha lakini amepatikana, tunaamini Waheshimiwa Wabunge zile kero ambazo ziko kwenye vyama, ziko kwenye mashirikisho zinakwenda kusimamiwa kupitia BMT. Lakini Katiba za vyama zinasimamiwa ili wanachama watendewe haki.

Mheshimiwa Spika, lingine ilikuwa ni kwa nini mshahara umepungua katika Wizara hii ilikuwa ni hoja ya Kamati. Waheshimiwa Wabunge wenzangu, fedha hizi zimepungua kutoka kwenye Wizara yetu baada ya Mheshimiwa Rais kupunguza majukumu ya Wizara yetu ya Habari kuondolewa kwetu, zaidi ya bilioni sita zimeondoka na Idara ya Habari kwenda kwenye Wizara nyingine.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda naomba niende kwenye hoja za Wabunge baadhi ya Waheshimiwa Wabunge. Mheshimiwa Bulaya na Wabunge wenzangu tunapokea pongezi zetu zote ambazo mmetupatia kwa ujumla na tunazithamini. Mheshimiwa Bulaya ameshauri kwamba Serikali iandae fedha kwa ajili ya timu yetu ya Serengeti Girls.

Kwanza niwapongeze sana hawa mabinti zetu, niwapongeze kwa moyo wa dhati kwa sababu jana mwenyewe nimeshuhudia jinsi ambavyo ule mchezo ulikuwa mgumu sana dhidi ya Cameroon. Mheshimiwa Waziri nashukuru uliniamini nikuwakilishe kule, lakini wale watoto walipambana kuhakikisha bendera yetu inapeperushwa na tunashinda, pamoja na ngumi, pamoja na adha zote walizozipitia hawa vijana wametuheshimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tunawathamini, tunawapenda na Taifa linawapenda, lakini hatukuwa nyuma kuwawezesha, tumetumia zaidi ya milioni 140 kuwawezesha mpaka wamefika hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru BMT, tunashukuru TFF, tunashukuru Chama cha Mpira wa Wanawake kuhakikisha vijana hawa wanapata stahiki zao, kwa kweli hawakupungukiwa. Pia mwaka unaofuata tumetenga zaidi ya Milioni 985 kwa ajili ya kuhakikisha hizi timu zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ilikuwa ni uwekezaji wa mpira wa wanawake mpaka ngazi za chini, nikuhakikishie kupitia Taifa Cup, kupitia viwanja tunavyovijenga tunazingatia viwanja vya Netball, pia kule mpira hautachezwa wa miguu tu ni pamoja na Netball tutahakikisha unachezwa na viwanja vinajengwa sambamba na viwanja vingine.

Mheshimiwa Spika, kuhusu CHANETA iwezeshwe kifedha. Tunawapongeza BMT wamesimamia uchaguzi wa CHANETA umefanyika, wamekuja mpangokazi wao wa miaka kumi kuhakikisha kwamba wanafufua mpira wa Netball hapa nchini. Mheshimiwa Bulaya nikutoe wasiwasi kwamba jambo hili tunalifuatilia kwa karibu sana mimi kama Naibu Waziri, Waziri na timu nzima ya Wizara kuhakikisha CHANETA mpangokazi wao watakaotuletea tutawakutanisha na wadau mbalimbali na wao waweze kupata ufadhili. Tumeshawaambia watuletee writeup zao ili kuhakikisha kwamba na wao wanaweza kupata ufadhili.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye hoja za jumla. Mheshimiwa Profesa Mkumbo amezungumza jinsi ambavyo sheria inatakiwa irekebishwe kuhakikisha kwamba starehe hatuiwekei mipaka kama ni usiku, asubuhi kuna mtu anataka kustarehe, tuongee na Wizara zingine kuhakikisha kwamba sheria hii inarekebishwa.

Mheshimiwa Spika, kingine ambalo nataka kuzungumza ni suala la riadha nchini. Ninaliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yetu tumeamua kutenga Mikoa kulingana na vipaji vyao. Kwa upande wa riadha tumeteua si chini ya Mikoa, Manyara, Arusha, Singida ambapo Kaka yangu Simbu anatoka, Mara na Mbeya. Tunawahikikishia Waheshimiwa Wabunge tutaibua vipaji vya riadha kuanzia ngazi za chini kabisa mpaka kuja juu tutapata vijana wazuri sana, huo mkakati tunao.

Mheshimiwa Spika, suala lingine la Kaka yangu Mheshimiwa Hamis Mwijuma kuhusu COSOTA naomba nilisemee kwa dakika kadhaa ambazo zimebaki. Kwanza tunakubali kwamba hoja zote ambazo Wasanii hawa wamekuwa wakizungumzia kuhusu COSOTA ni za kweli, pia niwapongeze kwa kuwa mmekuwa wakweli. Mheshimiwa Babu Tale amesema kama ni gari lipo barabarani linaanza kazi, tunashukuru kwa kulitambua hilo. Kuna mambo matatu kwenye suala la mirabaha.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni suala la mirabaha hii inapatikana wapi. Mheshimiwa Mwijuma ninakushukuru kwamba ilikuwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, nasi tumeyafanyia kazi, tumekaa na Wizara ya Fedha kuhusu blank tape Levy ianze kufanyiwa kazi. Tunashukuru Wizara ya Fedha wamepokea, naomba tusiwahishe shughuli tuwasubiri kwenye Finance Bill watuambie sasa wame-adopt mambo gani. Pamoja na nyasi bandia tumepeleka zile accessories kwa ajili ya kuweka nyasi kwenye uwanja, inahitajika kuna vitu vinahitajika vipunguzwe kodi vyote tumepeleka. Hili la kwenu mlihitaji kwamba tuwe na chanzo ambacho ni cha uhakika kwa ajili ya mirabaha, mkasema kwamba kule kwenye Halmashauri zetu tulikuwa na Maafisa Utamaduni wakusanye, washirikiane na Maafisa Biashara katika Hotel, Restaurant na maeneo mengine. Jambo hili COSOTA wamejaribu na ndiyo failure ambayo ninyi mmekuwa mkiongelea, lakini wewe mwenyewe ulituletea swali ukihitaji kwamba CMOs zenu zikusanywe.

Mheshimiwa Spika, hayo yote tumepokea na ahadi yetu kama Wizara kwa tasnia hii ni kwamba tutakutana na wadau, tutapitia haya yote lakini pia Finance Bill itakapoletwa maana yake sasa kama kutakuwa na adoption ya Blank Tape Levy source itakuwa imepatikana.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili katika hili la COSOTA ilikuwa ni suala zima la distribution ya mirabaha, tunapokuwa tumepata tunagawa vipi, mfumo uko wapi? Ninakiri kwamba ni lazima tuwe na mfumo ambao utawekwa kwenye redio zote, television zote, media zote ambazo zitakuwa zinacheza nyimbo hizi ili ijulikane ni wimbo upi ambao umechezwa wapi. Hii ya juzi siyo kwamba tuligawa tu kama zawadi hapana! Tulitumia mfumo ambao unatumika kidunia.

SPIKA: Malizia sentensi.

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.

Suala hili tulitumia mfumo unaitwa WIPO ambao wao wanaufahamu, ambao unakubalika worldwide na zile nyimbo nani kapata nini ilipatikana pale. Tatizo tulikuwa na pesa chache sana, tulikuwa na Milioni kama Mia Tatu ambazo ukizigawa mtu anaona amepungukiwa kidogo ndiyo maana tunasema sasa redio zote, kwa sababu ule mrabaha tulitoa ulitokana na redio kama tisa tu kati ya redio zaidi ya Mia Mbili. Ninaomba niwaahidi Waheshimiwa Wabunge wenzangu hili jambo Wizara tumelipokea na tunalifanyia kazi baada ya Bajeti hii tutakutana tuhakikishe kwamba tunakwenda vipi na tunawahakikishieni kwamba haki zenu mtapata.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)