Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Nimesimama hapa, awali ya yote naomba nimshukuru Mungu kwa nafasi hii kwa sababu kwa kweli leo ukumbi umekaa vizuri na kila mtu ana bashasha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii pia kumpongeza sana Waziri kwa kuwakaribisha hata machifu, wako huko na niseme leo ni siku ya tofauti niliyoiyona, mpaka saa hizi gallery zako zimejaa na zimetulia. Mara nyingine ikifika saa 4.00, ikishasomwa hotuba, hakuna mtu huko juu. Namshukuru sana Waziri kwa kutupa hotuba nzuri. Nampongeza yeye, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na timu yao yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze tu kwa jambo moja; nimeipitia hii hotuba kwa makini, au labda nimepoteza, sikusikia mahali ambapo amepongeza Bunge hili kwa vikombe vilivyokuja mwaka huu vingi vilivyozidi. Nimerudia, nimerudia, sikuona, labda siyo mahali pake. Hatuombi sisi chochote kwenye hii bajeti, kwa sababu Spika tayari ana fungu lake, lakini nimeumia, nimekwazika.

SPIKA: Mheshimiwa Shally Raymond hebu rudia hapo kidogo. (Makofi/Kicheko)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimechukua muda sana kuipitia hii ripoti ya Mheshimiwa Waziri na labda atanisahisha atakapokuja kutoa na taniambia ukurasa kwa sababu mimi namuamini, kwanza yeye ni msomi, ni Wakili Msomi na ninamwamini hata kama hajazishika hizo nyadhifa. Sikuona kwa nini hakulitamka Bunge hili kwa ushindi uliopatikana Uganda, Kenya, East Africa yote. Sasa mimi nimesikitika nimeona itaniumiza, nashukuru, nimeona lisiniue kifuani niliachie tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kama nimemkosea atanisamehe, lakini atanionesha ushahidi, maana yake yeye ni muda wa exhibit, utanipa exhibit kwenye ukurasa.

Mheshimiwa Spika, nimesimama zaidi hapa kumuomba Mheshimiwa Waziri kama ataona ni muhimu basi Kilimanjaro nayo ipate uwanja wa mpira. Mikoa yote ina uwanja wa mipira kasoro mikoa michache sana mmojawapo ni Kilimanjaro. Endapo tunaweza tukakaa hapa Waziri wa TAMISEMI akatoa amri, Halmashauri shirikianeni jengeni vituo vya afya katika kila kata, shilingi milioni 400, milioni 400; inashindikana nini Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoa tamko, Kilimanjaro sasa kujengwe uwanja mkubwa wa michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tuna eneo linaitwa memorial ni kubwa sana pamoja na kwamba sehemu inafanyika ni soko la mitumba, lakini hilo linalobakia linatosha kabisa kujenga uwanja na uwanja huo una upako. Kwa sababu alipokuja Baba Mtakatifu Tanzania alikanyaga ardhi ile. Kwa hiyo, kama tutajenga huo uwanja tukiwa na mashindano na Kenya, na nchi nyingine, Uganda na wapi tutashinda tu, kwa sababu pale ni patakatifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa namuomba sana Mheshimiwa Waziri kuliko tunavyofanya sasa kwenda kucheza kwenye uwanja wa Cooperative University, kwa nini tusiwe na uwanja wetu Kilimanjaro. Tunaomba sana na chonde chonde na ninaposema hapa na Mheshimiwa Rais ananisikiliza, tunaomba na yeye pia akipata namna atuangalie watu wa Kilimanjaro tupate uwanja wa michezo. Eneo tunalo tayari lakini halijawahi kuendelezwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo mimi niseme kwamba nilitamani sana katika vipindi vya michezo vinavyooneshwa, wasanii wetu wawe wabunifu, vipindi vya watoto viwe vya mafunzo zaidi. Kuna filamu zinazooneshwa sasa hivi zimekwaza wazazi japo wazazi ndiyo wanaonunua kifurushi cha kuangalia tv. Lakini kila mtu unamsikia anasema aaah, ile filamu ya watoto ya Azam Tv hivi na hivi. Sasa kwa nini msifanye filamu za watoto au katuni za watoto ninyi wabunifu wazuri.

Mimi huwa naangalia sana Mizengwe na kweli mizengwe hainipiti, lakini leo sijamuona hata mmoja wao huko juu. Lakini hiyo nasema kwetu sisi watu wazima, nimetoa mfano Mizengwe inafundisha leo watakwambia jinsi gani mtu alikwenda kupangisha nyumba, labda hakulipa nakadhali. Lakini pia wasanii wetu wangeweza wakawa wabunifu wakawafikiria pia watoto, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. (Makofi)

Kwa hiyo, nilikuwa nawaomba kwa vile wote wako hapo na wengi wao waangalie namna fulani au watakuja tu wanaweza kuigiza sauti kama kina Steve Nyerere na wengine, basi wanaweza kuja na ubunifu huo wakuweza kufanya hizi katuni za watoto zikawa more interesting yaani zenye elimu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo sikuwa na mengi ya kuzungumza zaidi ya kuomba huo uwanja wa memorial yaani Kilimanjaro tuwe na uwanja wa michezo. Niwapongeze wageni wetu wote waliotufikia siku ya leo kwa kweli mmetupa joto na sisi tunawapenda sana, ahsanteni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)