Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Shabani Hamisi Taletale

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nianze kwa dua, “Rabbi shrahli swadri, wayassrli amri, wahlul-uqdata min-lisaani yaf-qahu qawli”.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kuomba hii dua ni kumwomba Mwenyezi Mungu ausimamie ulimi wangu kwa yale ambayo naenda kuyaongea leo. Sababu ya kuomba hii dua kumwomba Mwenyezi Mungu aisimamie hii Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mengi leo ya kuongea, lakini nitaanza na hoja zangu tatu. Kabla ya kuanza kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Nampongeza kwa kile ambacho anakifanya Morogoro Kusini Mashariki, ndio maana nimekuwa siwezi kuchangia Wizara yoyote naona mambo yanakuja, mambo yanakwenda kwa hiyo, Mheshimiwa Rais anaupiga mwingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na BASATA. Ninaposema nianze na BASATA, naanza na BASATA. BASATA ni chombo cha kusaidia wasanii, lakini bahati mbaya BASATA imekuwa Polisi wa Wasanii. Nampongezae Mheshimiwa Waziri Mchengerwa, amekuwa kila siku akizungumza nami. Nina miaka 20 kwenye music industry, najua nini kinaenda vizuri, na nini kinaenda vibaya. Leo hii tuongee ukweli, BASATA hawana utaratibu wa kuwapa elimu wasanii, hawana utaratibu wa kutoa semina kwa wasanii, lakini BASATA wana utaratibu wa kufungia nyimbo za wasanii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sanaa; watu wanatulia ku-create kitu asubuhi, mchana, halafu wewe jioni unaziba, unazuia eti kwa sababu ya sheria ambayo msanii haijui. Niseme leo, sijui kama sheria yako itaniruhusu kuimba. Nitaimba hapa Waheshimiwa Wabunge waitikie! Mamaa Amiinaa! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiimba hii nyimbo kama mtu akiitikia vile inavyopaswa, basi BASATA walikuwa wanatakiwa waitazame hii nyimbo na waifungie. Hawawezi kufanya hivyo kwa sababu hajaimba msanii ambaye kwao hawana maslahi naye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua Mheshimiwa Waziri roho yake ni nzuri, naweza kutafsiri baadhi ya wafanyakazi wake, watumishi wake wana roho mbaya. Hawa vijana wanahangaika ku-create vitu, kama tunakubali kuipeleka Tanzania katika international level, hatusemi kwamba tunavunja utaratibu wa sheria, hatusemi kwamba tunakwenda kuvunja utamaduni wetu, lakini wewe uko busy kuwaza huyu kakoseaje umfungie; mpe elimu, umeshindwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa naongea na Mheshimiwa Ummy nikampa hii nyimbo na kiitikio chake, alisikitika sana, lakini leo hii tuko na BASATA ambao wako busy tu kuangalia kafanyaje? Tumfungie! Kafanyaje? Tumfungie! Tuangalie hiki kitu, kama tuna nia ya kukuza industry ya Sanaa, tuangalie tunawezaje kuwapa elimu wasanii. Hakuna aliye juu ya sheria, hakuna ambaye anayetaka kufanya jambo kwa ajili ya kujifurahisha yeye.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda tu kumpa taarifa mtoa hoja kwamba, BASATA imekuwa ikiwashika mashati vijana wa Kitanzania na kuwavuta nyuma. Nikitolea mfano msanii kama Gigi Money, ni kijana ambaye alianza kusimama, lakini hawatoi elimu ya kuwasaidia wasanii bali kuwavuta nyuma. Angalia sasa hivi Gigi Money badala ya kwenda mbele tunamwona tayari ame-drop. Tunategemea BASATA iweze kuwasaidia wasanii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tale.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yake naipokea kwa mikono miwili kabisa, maana nilikuwa namwangalia nani anatoa taarifa? Maana leo nimesema atakeyetoa taarifa awe na experience ya muziki kama niliyonayo mimi humu ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiizungumzia BASATA unazungumzia vitu ambavyo… Aah, Alhamdulillah!

Mheshimiwa Naibu Spika, niachane na BASATA, nahamia COSOTA, maana naweza nikaongea kuhusu BASATA halafu nikaumia roho vile vile. Hii taasisi ya COSOTA kama siku utaipelekea TAKUKURU pale unafunga wote wale. Natoa mfano, nina msanii wangu hamna asiyemjua hapa anaitwa Kassim Mganga, anatokea Tanga, hakuna asiyeimba nyimbo zake kwenye msimu wa harusi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kassim Mganga unamwita, unaenda kumpa shilingi 50,000 halafu unaenda kumwita Lulu Diva unampa shilingi 550,000 halafu umetumia vigezo gani? Kuna utaratibu gani ambao unatumika COSOTA kwenye kugawa mirabaha? Tumpongeze sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, ametoa gari bovu uwani, kaliweka barabarani. Hii COSOTA ni gari bovu liko barabarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo naondoka na Shillingi ya Mheshimiwa Waziri, nashika mshahara wake, atafuata Shilingi Kusini Mashariki namuahidi brother wangu. Kama hajaja na hoja ya kubadilisha utaratibu wa COSOTA, wasanii wale wanaimba; kuna msanii kama Mzee Yusufu? Nimemwona pale juu, ni mwanamuziki anaimba, anaandika, anapata haki yake vizuri. Huwezi ukamkusanyia Mzee Yusufu Shilingi milioni tano! Ana worth ya Shilingi milioni tano? Tuongee ukweli! Hakuna utaratibu wa kugawa fedha kwa wasanii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie wanatumia utaratibu gani kwenye kuwapa pesa wasanii? Nimeona kuna baadhi ya wasanii wanawapa pesa kwa sababu ya ukubwa wao wa Instagram na makelele tu. Sitaki kuongea mengi, mimi ni Kiongozi wa Taasisi ya Wasafi, hakuna msanii mmoja aliyepewa hata Shilingi kumi anakwenda kusimama pale Kiongozi wa COSOTA eti ooh, hawajakusanya nyimbo, hawajasaini kwa sababu ya redio fulani. Kama unapewa kitu, taasisi ambayo inasimamiwa na Serikali, usiegemee upande mmoja, ongoza kama kiongozi. Kuna redio zipo huko Morogoro Vijijini na wapi, zinapiga nyimbo za Wasafi, upo kwenda kuchukua hela? Leo hii eti unakwenda kumpa msanii pesa, Madii unampa shilingi 250,000. Mwaka 2021 watu kibao walikufa na Corona, hakuna nyimbo iliyoimbwa kama “Kazi Yake Mola”, tuwe wa wazi. Unakwenda kumpa Madii shilingi 250,000 kwa vigezo gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena, nitaendelea kuishika Shilingi ya Mheshimiwa Waziri mpaka nijue utaratibu gani unakwenda kuufanya kwenye hii COSOTA? Naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwenye hili tulisimamie kwa sababu copyright haisimami kwenye muziki tu. Mimi ni publisher, leo hii nasimamia music, kesho na keshokutwa watoto wangu watakula nini? Si ndiyo copyright inasimama kwenye kila eneo. Hakuna utaratibu mzuri! Mheshimiwa Naibu Waziri ukijiona huna jibu kwenye hili, ujue huna Shilingi ya Hamis Shaban Taletale kutoka Kusini Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna kitu kizuri kama msanii anapofanya jambo akasifiwa. Hawa vijana wanahangaika kwenye kutengeneza vitu vyao mimi nimpongeze sana kuna dada mmoja anaitwa Lamata movie ilikufa nchini, tuwe wawazi. Yule dada amepambana; kuna kipindi kinaitwa Juakali, kinakwenda vizuri sana, lakini nikwambie, yule binti kama atataka kwenda kuigiza Polisi, haitawezekana. Kama atataka kwenda kuigiza Jeshini, haitawezekana kwa sababu ya utaratibu wa Wizara tulioufanya. Kama tunataka kuwasaidia hawa wasanii, tuwasaidie tusione hii ni sehemu ya wahuni. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Taletale, hii ni kengele ya pili.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.