Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara ya Michezo. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri inayoonesha mwelekeo mzuri kwenye sekta yetu ya michezo hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa, niweze kuwapongeza Serengeti Girls kwa mafanikio makubwa ambayo wameyapata jana. Nimpongeze sana paka mweusi Bakari Shime pamoja na Edna Lyimo, kocha msaidizi, kwa kazi nzuri ambayo mmeifanya. Kwa sababu ni muda mrefu hizi timu zimeandaliwa lakini leo Mungu ameamua kutupa nafasi ya kwenda kushiriki Kombe la Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba nichangie kwenye mambo kama matatu hivi, jambo la kwanza ni suala la mfumo wa mchezo nchini kwetu na suala la maendeleo ya viwanja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, jambo la kwanza ambalo ninajisifia kwamba Wizara imepata mwanamichezo hilo ni la kwanza. Wakati mimi nahangaika na Singida United wewe ulikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, Haki na Hadhi za Wachezaji TFF, changamoto za wachezaji, changamoto za mpira, vyote unavifahamu. Kwa hiyo, ninafurahi kwamba tunakwenda kufanya kazi na mtu ambaye hii ni sehemu yake na ninafurahia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, mpira wetu una safari. Safari ndefu inaanzia kwenye mfumo wa soka letu la Tanzania, nitajikita sana kwenye soka. Mfumo wetu wa mpira wa Tanzania ambao tunaenda nao ni mfumo ambao wakati mwingine ni kama wa zimamoto, kwa sababu tunatamani sana tuwe na matokeo mazuri lakini hatujatengeneza grassroots nzuri za kuzalisha wachezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa hili leo tunaona Serengeti Girls wanakwenda huko, lakini mfumo wetu je, unawaandaa wengine kama hawa? Unakuta hauwaandai. Tunao majirani zetu ambao ni Watanzania wenzetu, Zanzibar. Zanzibar ndiyo watu ambao wana the best model ya mpira Afrika na Afrika Mashariki. Zanzibar wamechukuliwa model yao ya soccer development imekwenda kuwa applied Cameroon, Ghana na nchi nyingi, model ya soccer la Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa nini nazungumzia soccer. Katika Taifa lolote lile duniani lazima nchi ijipambanue nini inataka kwenda nacho. Leo nikiitaja Marekani ninataja basketball, nikiitaja Brazili ninataja samba, soccer, nikizungumzia Afrika Mashariki nikiitaja Kenya ninaitaja riadha. Leo nikiitaja Burudi ninataja makocha. Makocha wa timu zetu za Ligi Kuu karibu zote ni Warundi. Wenzetu waliamua wawekeze kwenye makocha. Nikiizungumzia Rwanda ninazungumzia basketball. Leo hii ndiyo wana-host basketball kwenye Afrika nzima. Sisi Tanzania tunajiangalia wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, tuna kitu cha kufanya kwa ajili ya Taifa letu. Sheria Na. 1 ya FIFA inazungumzia Taifa lolote lazima liwe na viwanja ndipo mpira uchezeke. Taifa letu kwenye suala la viwanja bado umekuwa ni mgogoro. Siku ile niliongea, mwaka jana, nikaomba hapa kwenye bajeti kwamba Mheshimiwa Rais atuondolee kodi kwenye nyasi bandia, akaondoa. Wakati ambao Taifa letu limepata political will ya Rais ni kipindi hiki. (Makofi)

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Taarifa.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mchangiaji ameongelea viwanja. Hapa Dodoma tuna uwanja wa kawaida sana, Uwanja wa Jamhuri, lakini ninapoongea hapa muda mwingi uwanja unatumika kwa maonesho na kufungiwa. Kwa hiyo, hata viwanja tulivyonavyo havitumiki kwa matumizi stahiki. (Makofi)

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ninapokea mchango wa Dada yangu ni mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, suala la viwanja limekuwa ni changamoto. I ask myself, was it the intention ya Mwalimu Nyerere kujenga viwanja nchi nzima, leo vigeuke magofu, vigeuke sehemu ambazo hazitumiki kwa ajili ya kuchezea, vimegeuka mazizi ya ng’ombe viwanja hivi, was that the intention of Mwalimu Julius Kambarage Nyerere? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Chama changu kina kazi ya kufanya. Nyerere alijenga viwanja kwa ajili ya michezo. Political will aliyonayo Mheshimiwa Samia kwa sasa kwenye michezo hadi akasema Mwanza kwamba nakielekeza Chama changu cha Mapinduzi kiweke nyasi bandia kwenye viwanja hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kwenye ukurasa wako wa 62, unasema tunatenga bilioni 10. Bilioni 10 unatenga kwa ajili ya ukarabati, hatua ya kwanza, hatua ya pili kwa ajili ya ukarabati, hatua ya tatu kuweka nyasi bandia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nikuombe Ligi Kuu ya Tanzania haihitaji ukarabati viwanja, inahitaji kuwekwa nyasi bandia. Mwalimu Nyerere alitujengea viwanja akiwa na Watanzania milioni 20 tu, leo tupo milioni 64 tunashindwa kuweka nyasi bandia kwenye Taifa hili? Mheshimiwa Waziri, nikuombe, hizo Bilioni 10 fanya kazi ya kuweka nyasi bandia kwenye viwanja vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2027 tunakwenda ku-host AFCON, tuta-host vipi AFCON kwa nyasi hizi? Kwa sababu hawa watu ambao tunakwenda ku-host AFCON wataenda kuangalia viwanja vyetu miundombinu yake ikoje. Nikwambie mbinu ambayo wametumia Zambia, waliamua CSR kwenye migodi ndiyo itumike kuweka nyasi bandia kwenye viwanja vya Zambia. Tanzania tunayo makampuni mangapi nchi hii yanayochimba madini? Tuna makampuni mangapi nchi hii yanayowinda wanyama wetu? Tuna makampuni mangapi nchi hii wanatengeneza bidhaa zao na wanauza? CSR ingetumika kuweka nyasi bandia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, you’ll be the game changer. Nikuombe Kaka yangu, viwanja, viwanja viwanja. Viwekwe nyasi bandia. Hiyo Bilioni 10 ninajua huna, unakwenda kumuomba Mama. Nitumie nafasi hii kumuomba Mheshimiwa Rais, Bilioni 10, achukue hata – kuna hizi fedha huwa mnarudisha mnaziita gawio – achukue hata gawio la Vodacom au Tigo au kampuni yoyote aweke kwenye viwanja, hapo tutakuwa tumemaliza tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, umezungumza hapa kwamba unakwenda kutengeneza ajira za vijana karibia 72,000 kupitia mtaa kwa mtaa. Hawa vijana utakwenda kuwapeleka wapi hatuna viwanja, hatuna academy. Mimi ninatoka Makete na hata hizi shule 56 za academy unakwenda kujenga, my suggestion is jenga kwa zones. For instance, kuna timu za Taifa zinakwenda kucheza maeneo ya baridi. Sisi tuna maeneo ya baridi ambayo ni Njombe, Makete na Mbeya, ungeweza kwenda kujenga kule shule moja kwa ajili ya kuwekea camp ili wanapokwenda kwenye mechi huko wakatumia hapa nchini. Kuliko hela za kambi, hela nyingi, tunakwenda kutumia nje wakati tungeweza kuja kuweka maeneo haya. Hizi 56 ni nyingi, hata chache tu anza nazo kwa sababu safari ni hatua. Ninakuomba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, wewe ulikuwa TFF, unajua wachezaji wetu walivyo na changamoto ya maslahi, it’s the time now. It’s high time now kwenye Taifa letu, lazima tuweke salary scale, lazima mishahara ya wachezaji wetu wa Ligi Kuu, wachezaji wetu wa Ligi Daraja la Kwanza, wachezaji wetu wa Timu za Taifa wawekewe kiwango cha mishahara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, vijana wetu wanacheza kwa jasho na damu, wanalipwa laki mbili kwenye ligi kuu, wanalipwa laki tatu. Hawa vijana wanapata magonjwa wanalazwa mahospitalini tunaanza kuchangishana, lazima tuweke salary scale ya kwamba mchezaji wa ligi kuu lazima alipwe Milioni Moja minimum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna fedha nyingi sana kwenye mpira zinapotea, tungewasaidia vijana hawa ambao leo hii hapa kila mtu anawapigia makofi wakiwa wamekaa pale juu, lakini do you know how much they get, wanapata shilingi ngapi? Inawezekana hata laki mbili mfukoni hawana leo. Lazima kama Taifa tufanye mabadiliko ya sera zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, umeweka Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Soka 2022 - 2032 miaka kumi hapa, moja ya vitu ambavyo unatakiwa uingize ni maslahi ya wachezaji wetu. Tutamshambulia Ndugu Karia lakini Ndugu Karia is the best president, amefanya kazi vizuri, anafanya kazi vizuri ndiyo maana leo wote tunajivunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, ninakuomba fanya mabadiliko…

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Sanga, kengele ya pili.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni mwanamichezo, tuendelee kum-support ndugu yangu na Kaka yangu, all the best. (Makofi)