Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Amb. Dr. Pindi Hazara Chana

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kupata nafasi hii ya kutoa ufafanuzi wa baadhi ya maeneo. Nianze pia kwa kukushukuru wewe mwenyewe kwa kutuongoza vema, lakini pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kuchambua na kujadili taarifa ya utekelezaji wa bajeti yetu vizuri na ushauri waliotupa kwa kweli tutaendelea kuuzingatia.

Mheshimiwa Spika, tumepata wachangiaji takribani 36 na kati yao waliochangia kwa kuongea ni takribani 26 na pia waliochangia kwa maneno takribani wachangiaji 10.

Mheshimiwa Spika, nami niungane na Waheshimiwa wengine wote na Mheshimiwa Naibu Waziri kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Rais ametuonesha dira, ametuonesha njia juu ya suala zima la uhifadhi na masuala mazima ya utalii hususan suala zima la Royal Tour. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli nichukue nafasi hii kumshukuru sana sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kutuongoza vema katika kutukumbusha kwamba masuala haya ya utalii tujue na kutambua kwamba yanachangia pato la Taifa lisilopungua asilimia 17 na tuna maelekezo kwamba ifikapo mwaka 2025 tuendelee kuongeza pato la Taifa hadi kufikia dola za Kimarekani zisizopungua bilioni sita na watalii takribani milioni tano. Hivyo ni jukumu letu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuona ni namna gani eneo hili tunaliboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vile vile nishukuru sana kwa michango ya Waheshimiwa Wabunge wote Waheshimiwa Wabunge wamechangia michango mbalimbali na sisi Wizara tuseme tu kwamba michango hiyo tunaichukua tunaifanyia kazi na tutaleta majibu hayo kwa maandishi kwa michango yote tutaleta kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda haraka haraka katika eneo la udhibiti wa wanyama pori wakali na waharibifu nianze kwa kutoa pole kwa changamoto hii kwa wananchi kutokana na adha ya wanyama pori wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo Wizara yangu imeendelea kuchukua hatua za muda mrefu na muda mfupi kukabiliana na changamoto hii. Suala la wanyama hawa limekuwa ni changamoto iwe ni tembo na wanyama wengine na tumelizungumzia sana na kwa kweli tunaafiki kwamba eneo hili tuone namna gani ya kuboresha na tukiboresha ndipo sasa tutaweza kuwalinda wananchi wetu wasipate madhara na maumivu yoyote, lakini pia tukizidi kuboresha tutaona jinsi gani ya kulinda hata hifadhi zetu.

Mheshimiwa Spika, hatua za muda mfupi zinajumuisha kuanzisha ujenzi wa vituo 19 vya kudumu kwa ajili ya askari wa Jeshi ya Uhifadhi na kizimba kimoja kwenye maeneo yafuatayo; Wilaya ya Meatu - Kijiji cha Malwilo kutakuwa na kituo; Rufiji katika Kijiji cha Ngarambe; Busega katika Kijiji cha Kigereshi; Lindi katika Kijiji cha Milola; Tunduru katika Kijiji cha Milonde; Mwanga katika Kijiji cha Kwakoa; Iringa katika Kijiji cha Itunundu; Songwe katika Kijiji cha Udinde; Nzega katika Kijiji cha Ndala; Mvomero katika Kijiji cha Lubungo; Chamwino katika Kijiji cha Ilangali; Mpwapwa kutakuwepo na kituo pale Mtera; Nachingwea tutaweka kituo pale Nditi; Liwale Ng’ungu kutakuwa na kituo; Kondoa katika Kijiji cha Mkungunero; Malinyi kutakuwepo na kituo pale Kwa Kilosa Mpepo na Karatu kutakuwepo na vijiji vya Kambi ya Nyoka, Oldeani na Kambi ya Simba na kujenga kizimba kimoja cha mamba katika Jimbo la Buchosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vituo hivi 19 vitajengwa kwa bajeti ya mwaka huu 2021/2022 ambapo ndani ya mwezi Juni, 2022 ujenzi utaanza rasmi. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2022/2023 Wizara itajielekeza kujenga vituo vingine hivi ni vya mwanzo kutakuwa na vituo vingine tena 13 kwenye maeneo mengine yenye changamoto. (Makofi)

Vilevile hatua za muda mrefu ambazo zinajumuisha kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta nazo zitakuwepo kutoa elimu za uhifadhi kwa jamii zinazoathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu; kuendelea kuwadhibiti tembo, mamba, viboko, fisi na wanyamapori wengine ambao ni hatarishi kwa njia tofauti kwa lengo la kumaliza madhara haya; kutumia njia mbadala za kielektroniki kwa mfano kuwafunga wanyama GPS Collar na kuona ni namna gani tunaendelea kudhibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hata hivyo niendelee kutoa rai kwa wananchi kuona namna gani tunaweza tukajiepusha na kuvamia maeneo ya hifadhi kwa shughuli za kibinadamu ambayo hupelekea wanyamapori kusababisha migongano baina ya wanyama na binadamu. Kwa hiyo, tuendelee kushukuru sana kwa maoni ambayo tumepata namna ya kuendelea kuboresha maeneo haya ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni suala zima la Royal Tour na eneo hili ambalo linachangia sana pato la Taifa tumepata ushauri wa aina mbalimbali hapa umetokea ushauri wa jinsi ya kuratibu ziara za mafunzo kwa wakala wa utalii na hilo tutalizingatia na kuendelea kutumia watu maarufu na waandishi wa habari kwa ajili ya kutangaza vivutio vyetu. Wizara imeendelea kutumia watu maarufu na Wizara imetumia watu maarufu mfano mchezaji wa timu ya Taifa ya Ufaransa Mamodou Sakho; msanii maarufu wa filamu ya Nolly Wood kutoka Nigeria Gimy Aik; msanii maafuru wa filamu Will Smith wa Marekani pia amewahi kufika katika hifadhi zetu; mchezaji wa Klabu ya Real Madrid Vallejo Jesús; na mchezaji maarufu wa timu ya PSG Andrea Herrera, hii yote ni mikakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mnamo mwezi wa 10 tutaendelea kuwa na mkutano mkubwa sana pale Arusha hii yote ni katika kutangaza masuala ya utalii, huu ni Mkutano wa 65 wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia utalii duniani Kamisheni ya Afrika utafanyika nchini mwezi Oktoba, 2022 Jijini Arusha na utakuwa na takribani washiriki wasiopungua 500. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii ukiwa na watalii tuseme 1,000 wamelala Tanzania chukua mfano watalii wote hawa 1,000 kila siku asubuhi wanakula mayai mawili maana yake utalii huu unaongeza tija na sekta mbalimbali za uchumi maana yake yule mjasiriamali ambaye anafuga kuku, analima mchicha na mazao mengine ataongeza kipato na ndiyo maana tunasema suala hili la utalii tuone namna gani ya kuendelea kuliimarisha. Lakini pia tunaendelea kushirikiana na ofisi zetu za ubalozi kote duniani kuendelea kutangaza vivutio hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tumeona kwamba upo umuhimu wa kutumia digitali katika kutangaza utalii, kwa hiyo, tunaimarisha utangazaji wa utalii kupitia vituo maalum vya kidigital cha kutolea taarifa mbalimbali za vivutio vya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu idadi ya vitanda kwa mwaka 2021 Wizara ilifanya utambuzi na uhakiki wa huduma za malazi katika mikoa 26 nchini ambapo jumla ya huduma za malazi 10,432 zilipatikana zenye jumla ya vitanda 122,532 na vitanda 132,684. Hata hivyo tunaendelea kuhamasisha wadau mbalimbali waendelee kuwekeza katika huduma za malazi nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu mapitio ya sheria na kanuni; Wizara inafanya mapitio na sheria mbalimbali na kanuni na kuona kama kuna umuhimu wa kufanya maboresho ya tozo zilizopo. Sambamba na hatua hizi Wizara inaendelea kuboresha miundombinu ya utalii nchini ili kuimarisha kufikika kwa vituo vya utalii mbalimbali. Aidha, Wizara inatoa elimu kwa wadau mbalimbali wa utalii ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa watalii ambao wanatarajia kuongezeka kutokana na programu hii lazima tuwaandae watu wetu tutoe elimu na vyuo vyetu vya utalii vinaendelea kutoa elimu hiyo.

Mheshimiwa Spika, Wizara pia inaendelea kuimarisha ulinzi na kuendeleza rasilimali wanyamapori, misitu, nyuki na malikale kwa kufanya masuala mbalimbali ikiwa ni kuendeleza, kuimarisha kwa mfano Jeshi la Uhifadhi la Wanyamapori na Misitu na kuongeza vitendea kazi na idadi ya watumishi na kuwajengea uwezo kwenye nyanja mbalimbali. Hivi sasa tumeomba kibali cha kuweka askari 600 ambao askari hawa watasaidia pia kudhibiti wanyama wakali katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya nikushukuru sana kwa nafasi hii naomba kutoa hoja. (Makofi)

(Hoja imetolewa Iamuliwe)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.