Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuwa mchangiaji wa mwisho wa hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa filamu yake ya Royal Tour ambayo Mheshimiwa Naibu Spika alisema asubuhi kwamba, mama ameupiga mwingi na sisi tunaupiga wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi niwashauri Wizara kwamba Mheshimiwa Rais ametutangaza vya kutosha, sisi tunatakiwa kuweka miundombinu wezeshi kwa ajili ya kuwapata watalii. (Makofi)

Kwanza ukijaribu kuangalia barabara zetu zinazokwenda kwenye hifadhi zetu nikitolea mfano barabara kutoka Lodoare kwenda Nabi Gate ni barabara ambayo yanapita magari yanayokwenda Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Serengeti, kwa hiyo, tunatakiwa kuhakikisha kwamba, tunaboresha miundombinu yetu. Lakini pia barabara inayotoka Mto wa Mbu kuelekea Loliondo ni barabara muhimu pia ambayo Wizara hii inatakiwa kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi kuangalia namna ya kuboresha ili watalii waweze kupita katika njia zile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kipengele cha idara ya wanyamapori, nimeona mapendekezo yao ya kuweza kupandisha baadhi ya mapori tengefu kuwa mapori ya akiba. Mapori hayo yaliyotajwa, kipengele namba 5.3.1.1 Lake Natron, Kilombero, Loliondo, Lolkisale, Longido, Mto wa Mbu na Simanjiro. Mimi naomba niwaambie kwa upande wa pori tengefu la Loliondo wananchi wa Loliondo wameleta mapendekezo yao na wameshakabidhi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Niishauri Wizara mkapitie taarifa zile za Loliondo pamoja na Ngorongoro ili angalau zikafanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini leo huku tunalia Loliondo, mmeshaenda Lake Natron. Wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro pande zote mnapiga Mashariki, Kusini, Kaskazini, wananchi wanalia kote. Lake Natron ni Wilaya ya Ngorongoro pia, Loliondo ni Wilaya ya Ngorongoro, ukienda Ngorongoro tarafa ya Ngorongoro eneo la Ngorongoro Conservation Area ni Wilaya ya Ngorongoro. Sasa hao wananchi kwa nini hamtaki wapumue? Kila upande mnawapiga, kwa nini? Leo mnakuja kusema mnapandisha pori tengefu la Mto wa Mbu, hivi pori tengefu la Mto wa Mbu liko wapi? Liko wapi?

Mheshimiwa Spika, kote kumekuwa ni mji, sasa maana yake tunaendelea tena kwenda kuongeza taharuki kwa wananchi wa Wilaya ya Monduli. Bado hatujamaliza Monduli, Wamasai wa Longido watalia kwa sababu mmeandika hapa, bado hawajapumzika hao tunaenda Lolkisale watalia kule, bado hatujanyamaza tunaenda Simanjiro. Hao wananchi tunawatakia nini? Huu uhifadhi tunaouhifadhi ni kwa manufaa ya nani?

Mheshimiwa Spika, kama uhifadhi sasa imekuwa kilio kwa wananchi haina haja ya kuwa na uhifadhi huu. Ni lazima tuwe na uhifadhi ambao unawaletea wananchi maendeleo, lakini uhifadhi ambao unaleta kilio kila siku kwa Watanzania hauna manufaa kwa sababu leo wakilia wananchi wa Kilombero, watakimbia Loliondo, wakilia wa Loliondo wataenda Lake Natron, wataenda Simanjiro, wataenda Lolkisale, sasa sijui hawa wananchi tunawatakia nini?

Mheshimiwa Spika, mimi nadhani kinachotakiwa sasa ni lazima tuamue mgogoro wa eneo la Loliondo umedumu kwa zaidi ya miaka 31 sasa, Serikali ni lazima tufikirie namna wale wananchi waachwe waendelee na maisha yao, tumewarudisha nyuma kimaendeleo, kiuchumi na lile eneo ndipo wanapochungia mifugo yao.

Kwa hiyo, mimi nishauri Wizara kuna maeneo mengi tumeshahifadhi, square kilometer 307,800 za Tanzania nzima ambayo ni asilimia 32.5 mpaka 40 ya ardhi yote tuliyonayo Tanzania. Maeneo mengine tuwaache wananchi waendelee na maisha yao.

Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine Wizara hii, kama alivyosema Mheshimiwa Mulugo, wanyamapori wanaingia kwenye mashamba ya wananchi, tunasema tunatoa fidia, lakini miaka yote tumeshindwa kutoa fidia kabisa. Kama alivyosema Mheshimiwa Kuchauka hata wananchi wangu wa Kata za Oloipiri, Soitisambu, Ololosokwan na kata nyingine mashamba yao yote yameliwa na tembo. Sasa tutafute namna ya kuwapelekea chakula kwa sababu tembo wanaingia kwenye mashamba wanamaliza moja kwa moja, lakini hakuna fidia yoyote inayotolewa na Wizara ya Maliasili, lakini pia kuna wananchi wanauawa na tembo na wanyama wengine wakali…

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Shangai, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Londo.

T A A R I F A

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, sio tembo tu, hivi tunavyozungumza kwa wiki nne ndege wanashambulia mashamba ya wakulima katika Kata ya Kilangali, Wilaya ya Kilosa, lakini ndege hawa wanahifadhi ndani ya Hifadhi ya Mikumi na tumeomba zaidi ya mara tatu/mara nne tupate kibali cha Wizara ya Kilimo kwenda kuuwa ndege hawa, hatujapata mpaka sasa. Kwa hiyo, sio tembo tu wanakula mazao ya wakulima, hata ndege pia. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Shangai.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, mimi nashukuru na ninapokea Taarifa ya Mheshimiwa Londo, lakini kikubwa…

SPIKA: Ngoja, subiri kidogo.

Waheshimiwa Wabunge, ili upokee au ukatae Taarifa, lazima Kiti kiwe kimekuuliza unaipokea au unaikataa? Kwa hiyo, mimi sijakuuliza swali hilo, nimekuita tu ili uendelee kuzungumza.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, niendelee kwa sababu, jamaa ameamua kula muda wangu, lakini mimi nishauri Wizara hii wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro wameleta maoni yao, wamekabidhi kwa Waziri Mkuu, mkaisome, hayo ndio maoni ya wananchi na ndio msimamo wao.

Mheshimiwa Spika, naomba niende kukaa, ili badae Waziri atakapokuja atuambie fine kwa ajili ya mifugo wanaoingia hifadhini ni shilingi ngapi? Kwa sababu kumekuwa na varieties, leo unakuta ni 10,000; 50,000; mpaka laki moja; kwa hiyo, baadae Waziri atuambie ni kiasi gani kinatakiwa mifugo wanapoingia hifadhini? Ahsante nashukuru. (Makofi)