Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Jeremiah Mrimi Amsabi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Maliasili na Utalii. Awali ya yote nimpongeze sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameifanya ya kutangaza nchi yetu hasa hasa kupitia filamu ya Royal Tour, tunamshukuru sana. Lakini pia niipongeze sana Wizara hii ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea nayo na kipekee kabisa tunawapongeza, pale Serengeti wanaendelea na uratibu wa miradi mikubwa ya kijamii inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani ya KfW. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua Wizara hii ya Maliasili co-business yake ni kuhakikisha wanahifadhi maliasili zetu zote pamoja na kuliwezesha Taifa kupata mapato. Sasa yako mambo kama matatu hivi ningependa kuyachangia ili kuona kuwa wanaweza kufanya kazi hii vizuri.

Jambo la kwanza naishauri Wizara hii sasa iharakishe ujenzi wa uwanja wa ndege wa Serengeti. Uwanja wa ndege wa Serengeti unaweza kutusaidia sana kuongeza uhifadhi, ukienda ndani ya Hifadhi ya Serengeti kuna viwanja vingi sana, kuna utitiri wa viwanja na viwanja vile vinaathiri sana uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna ndege nyingi zinatua, ni makelele mengi, sasa mambo haya huwa yanakwenda taratibu taratibu, yanafukuza wanyama kuna hali ya utulivu kukosekana, wiwanja vimekuwa vingi sana. Sasa sisi katika Halmashauri ya Serengeti tumetenga eneo tayari na ninaishukuru Wizara inaendelea na michakato ya ujenzi wa uwanja. Sasa tunawaomba waongeze kasi ya ujenzi wa uwanja ule na ujenzi wa ule pia utasaidia sana wananchi kuona sasa manufaa makubwa ya uwepo wa Hifadhi ya Serengeti katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna habari ya ushindani wenzetu wa upande ule ambao tuna-share nao ecosystem na wao sasa wanakimbizana, kuona namna ambayo wangefanya wapate watalii wengi sana na watalii hao ni wale wale wanaokuja Serengeti. Sasa niwaombe sana waongeze kasi ya ujenzi wa uwanja huu itatusaidia sana kuongeza mapato kwa sababu pia hata watalii hawa itawapunguzia cost kwa sababu hawatasafiri umbali mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kuna mikataba ambayo Wizara ya Maliasili inaingia na mahoteli ambayo yanajengwa katika hifadhi. Mikataba hii tunaomba sana Wizara, Wabunge wengi wamelalamika habari ya CSR haieleweki, habari ya service levy haieleweki katika mahoteli. Lakini ukiangalia kwa kiasi kikubwa ni kwa sababu ya mikataba. Mikataba hii tungeiomba Wizara inaposainiwa iweze kubainisha kabisa wazi kwamba wahusika watalipa service levy pamoja na CSR katika halmashauri ambazo hoteli hizi zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaiomba sana Wizara izingatie hili leo ni aibu sana unakwenda katika Wilaya kama za Serengeti zenye hifadhi kubwa halmashauri hazina mapato. Kwa nini hazina mapato ya kutosha na mahoteli? Ni kwa sababu hoteli zile, hazioni zinawajibika direct kulipa CSR pamoja na service levy katika halmashauri hizi. Kwa hiyo, tunaomba sana Wizara hii ijitahidi kuhakikisha jambo hili sasa linaondolewa utata. Pale Serengeti tumehangaika muda mrefu tunazo hoteli nyingi ndani ya hifadhi zaidi ya hoteli 200 pamoja na camp sites, lakini malipo yao ya service levy imekuwa ni shida malipo yao ya CSR yamekuwa ni shida, tunaomba sasa kwa mwaka huu unaoanza Wizara hii itusaidie kumaliza tatizo hili. (Makofi)

Jambo lingine la tatu, ningeiomba sana Wizara hii ya Maliasili na Utalii ipitie upya, Wabunge wengi wamelalamika kuhusiana na tembo pamoja na wanyama wakali. Tembo na wanyama wakali wameendelea kuwepo karibu kila mahali. Sasa tunaiomba Wizara kwa sababu uhifadhi umekuwa ni mzuri sana na wanyama wameongezeka na wanyama hawa ndio ambao watalii wanawafuata. Sisi hatuna lengo la kusema wanyama hawa sasa waondolewe wasiwepo, sasa tunaomba tupitie vizuri zile taratibu zetu za uhifadhi. Kuna haja sasa ya kujenga fence ya umeme ambayo haina madhara tunahaja hiyo na ukiangalia wenzetu kule wanafanya. Kuna wakati nimepita Masai Mara nimeona pembeni wao wamejenga fence na hakuna namna ambayo tutazuia wanyama hawa wasiweze kuwadhuru wananchi…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, sasa tutalia hapa tutapiga kelele tutaonekana kwamba hatuna mapenzi mema na hawa wanyama hapana, tunawahitaji.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Amsabi, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nampa taarifa Mheshimiwa Amsabi kwamba ni kweli kuna haja ya kuweka fence, lakini fence hiyo ikijengwa isije ikajengwa kuziba mito iliyozunguka wananchi. Kwa hiyo, ijengwe kuelekea mapori ya wanyamapori, sio kule kwa wananchi. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, taarifa imetolewa lakini nilishawakumbusha hapa ndani, sio kazi yako wewe kusema kama Mbunge anachokisema ni halali sio halali; kweli au si kweli labda kama umesimama Kuhusu Utaratibu. Kwa hiyo, huwezi kusema anachokisema ni kweli yeye anajua ni kweli ndio maana kasema.

Mheshimiwa Amsabi, unapokea taarifa hiyo?

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante napokea taarifa hii na nipende kuhimiza sana kwamba kuna maeneo ya vijiji ambavyo sasa ile buffer zone haipo, kwa mfano, kule kwenye Jimbo langu ukianzia Kijiji cha Mbilikili ukienda hapa Bisalala, Tamkeli, Mbalibali, Machochwe mpaka Merenga kule wamemaliza kabisa eneo la buffer zone halipo. Sasa maeneo kama haya ndio ambayo naona kwa sasa ni lazima fence iwekwe, kwa sababu kwa namna yoyote ile wale wanyama hakuna namna ya kuwa-control, lile eneo la kinga halipo tena. Kwa hiyo, katika maeneo kama haya yapewe kipaumbele cha kwanza katika kuangalia kwamba sasa yawekewe buffer zone. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwa nini wanyama hawa wanapowaua wananchi na wanapoharibu mazao fidia imekuwa ni changamoto sana. Kwa hiyo, niiombe Wizara hii wanayo taasisi ya TAWA ambayo tunajua kwa utaratibu wao ndio wanaoratibu kutoa fidia kwa wananchi. Lakini pia wapo Maafisa Wanyamapori hawa DGO’s hawa Maafisa Wanyamapori pamoja na TAWA process ile inakwenda kwa taratibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)