Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyoko mezani. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kunipa nafasi, lakini nawashukuru wananchi wa Urambo pamoja na familia yangu kwa ushirikiano wao mkubwa wanaonipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukuwe nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Pindi Chana, Naibu wake Katibu Mkuu, Wakuu wa Idara na watendaji wote walioko katika Wizara hii kwa kweli kazi yao ni kubwa cha maana ni kwamba tuwape mawazo mengi na jinsi ambavyo wanaweza kuhakikisha kwamba kazi inaendelea vizuri zaidi ya kile kinachondelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza mama yetu Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anajitahidi kupata njia mbalimbali za kuongezea mapato ikiwa ni pamoja na Royal Tour. Mimi nina kata nne ambazo zinaingia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugara, Urambo. Niishukuru Serikali kwa kutupa hifadhi hiyo walivyopitisha kama azimio tulishukuru, lakini yako mambo ambayo pamoja na shukrani inabidi yafanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano tulipoambiwa kwamba tumepata hifadhi pamoja na kushukuru mimi nilikwenda kuonana na Kamati inayohusika nikawaambia kwamba panapotokea kitu kikubwa kama hiki watu wamepata hifadhi kwa mara ya kwanza, ni vizuri ingekuwa inatolewa elimu kukutana na wananchi wanaohusika, kuwaambia hifadhi maana yake nini, wajibu wao kama wananchi, wajibu wa Serikali ili wajue kwamba kweli hiki tumekipata lakini utaratibu wake wa kushughulika nacho ni moja, mbili, tatu, nne. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikwenda kuwaomba Kamati husika kwamba waongeee na Wizara ili waje waongee na wananchi wanaopakana na hifadhi ikiwemo ni kata nne zifuatazo; kuna Nsenda, Ukondamoyo, Ugara na Uyumbu; na kulikuwa na umuhimu wa kukutana na watu hawa kwa sababu katika mwaka 2013/2014 wananchi hawa walilima mazao yao, wakaruhusiwa kwamba mkivuna msirudie tena, lakini kabla hawajavuna yakachomwa moto mazao yao, kwa hiyo ikaleta uhasama kati ya Serikali na wananchi kwa sababu waliwachomea mazao yao wakati waliwaahidi kwamba hawatayachoma mpaka wamalize kuvuna ila wasirudie tena.

Mheshimiwa Spika, na ndio maana nikaona kwamba kumbe kitu kikubwa sana ni ilikuwa ni elimu na kukutana na wananchi ili kuweka mahusiano yawe mazuri, na wao wananchi wa kata hizo nne walikuwa na sababu zao wanasema wakati wa kuunda vijiji mipaka ilikuwepo, lakini maliasili ilipokuja kuweka mipaka yake ikawarudisha nyuma wakati kama walivyoongea wenzangu watu wanaongezeka idadi na wao wale wazee tulikwenda nao Mheshimiwa Hasunga alikuja kama Naibu Waziri, Mheshimiwa Ramo Makani alikuja kama Naibu Waziri, Mheshimiwa Mabula kama Naibu Waziri wa Ardhi kuja kuona mgogoro na tuliandika barua rasmi kwamba wao wanaona kwamba eneo lao la asili wamesogezwa nyuma, kwa hiyo, wana uhaba ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ndio nikaona kwa kweli kulikuwa na haja ya kukaa nao kuwekana sawa kabla haijawa hifadhi, lakini bado tunashukuru hifadhi imepatikana, lakini kuna haja ya kufanya yafuatayo; na huu mgogoro unajulikana tulileta hapa rasmi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ombi langu mimi kwa niaba ya hizo kata nne ni kama ifuatavyo; la kwanza pamoja na shukrani ya kupata hifadhi bado wakakae na wananchi waongee nao waone jinsi ambavyo watashirikiana nao.

Mheshimiwa Spika, la pili na ambalo pia nimeongea Mheshimiwa Rais alipokuja Tabora nimeliongelea kwamba pamoja na kushukuru kupata hifadhi wananchi kwa sababu wameongeza tunaomba eneo tupate angalau kilometa 5.5 hata ikiwezekana Serikali itupe kilometa 6 ili wananchi waliozoea kufunga nyuki na njia mojawapo ya kupatia mapato waweze kuweka mizinga yao. Kwa hiyo, bado narudia kuomba tena ndani ya Bunge hili tukufu kwamba Serikali ione umuhimu wa kuwarudishia angalau kilometa tano au sita waweze kupata mahali pa kuweka mizinga yao na kuvuna asali na pia mifugo yao iweze kupata eneo, hilo ni ombi la pili.

Mheshimiwa Spika, ombi la tatu; sasa hivi awaruhusiwi kuingia kwenye Hifadhi yetu ya Taifa kwa sababu wanasema hawawezi kwenda kuvuna asali yao, asali inavunwa kuanzia mwezi huu wa sita na mwezi wa saba, naiomba Wizara iwaruhusu watu wanaofuga nyuki waende wakavune asali zao tayari sasa hivi mwezi wa sita na mwezi wa saba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia sisi kama Urambo tuna asali yetu ina kaweusi hivi, sasa tulivyoipata nyingi tukatafuta wamarekani wanaitwa Follow the Honey wakaja kuomba wakasema ile asali yetu sisi inafaa sana kutengeneza chocolate, kwa hiyo tukaandika barua rasmi Wizara ya Maliasili na Utalii kuomba mashine na tukawaonesha eneo ambalo tumeliandaa kwa ajili ya kukusanya asali. Nawashukuru Wizara walimtuma mwakilishi wao mkurugenzi akaja akaahidi kwamba Urambo tutapata mashine ya kuchenjuwa asali na sisi Urambo tupeleke asali Amerika na kwingineko wakatengeneza chocolate, lakini mpaka sasa hivi hatujapata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mimi naamini kama Wizara ilituma Mkurugenzi tunaomba ile ahadi iendelee kwa sababu Serikali yetu ni sikivu watupe mashine ya kuchanjua asali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na la mwisho, kengele?

MBUGE FULANI: Mheshimiwa Spika, bado.

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ya kwanza.

Kwa hiyo tunategemea kupata mashine kwa sababu ahadi ni deni tunaiomba Serikali ituletee mashine na sisi tuchenjeu asali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na lingine ni suala la Serikali kama kuna tatizo mimi ningeomba liwe linaisha, fikiria sisi tangu mwaka 2014 Mawaziri wote wamekuja hao akina Hasunga, wamekuja akina Makani, wamekuja mama Mabula suala linaendelea. Mimi ningeomba Serikali kama kuna changamoto imetokea ifuatiliwe iishe, kuliko wazo moja tatizo linaendelea miaka na miaka mimi naona sio kitu kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzangu wameongelea sana kuhusu tembo na mimi pia kuna tembo kwangu tarehe 21 mei, Mzee Damian Lukaka, Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi ameuawa na tembo katika Kata ya Ukondamoyo Kijiji cha Kamalenge na mimi mwenyewe nikapeleka pole. Naomba kweli suala la tembo liangaliwe kwa njia nzuri, kweli tunahitaji tembo, lakini pia tunahitaji usalama wa wananchi wetu kwa hiyo naomba suala la tembo liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba tu nirudie kwa mara ya mwisho kabla kengele ya mwisho haijalia, kwanza tupate elimu, tushirikishe wananchi; pili tunaomba tutengewe eneo; tatu tunaomba wafuga nyuki waruhusiwe kwenda kuvuna asali yao; na nne kama nilivyosema mashine ya kuchenjua asali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono, ahsante sana. (Makofi)