Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, hatimaye niungane na wachangiaji wote ambao wamechangia katika Wizara ya Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pongezi za pekee zimuendee Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuipaisha nchi yetu ya Tanzania si katika Afrika bali duniani kwa ujumla wake na hasa kupitia suala zima la utalii la Royal Tour. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si hivyo tu, kutokana na hivyo, Mama anatambulika duniani. Hivi karibuni Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepata tuzo ya aina yake kuhusiana na masuala mazima ya miundombinu ya barabara. Hongera sana Mama yetu mpendwa, Mama Samia Suluhu Hassan, fanya kazi Watanzania tuko nyuma yako na dunia inakuona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, naomba niwatambue viongozi katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii ambayo Wizara hii inaongozwa na Mheshimiwa Pindi Chana pamoja na Naibu Waziri wake, bila kusahau Katibu Mkuu wa Wizara hii. Wamewasilisha taarifa yao vizuri na taarifa ina mambo mengi na ndio maana tumepata fursa ya kuchangia Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo kwenye Wizara hii wameeleza mafanikio yaliyopatikana na mafanikio haya ni kupunguza kwa ujangili kwa asilimia 90. Sasa mimi nataka nianzie hapo katika kupunguza ujangili kwa asilimia 90.

Mheshimiwa Spika, kweli nakubaliana nao, ujangili umepungua kwa asilimia 90; kupungua kwa ujangili kwa asilimia 90 ndiyo kumeweza kuleta madhara. Tembo wameongezeka, tena wameongezeka kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa tembo hawa kumeleta madhara makubwa katika nchi yetu. Na hili ninalizungumza kila mtu hapa ambaye kwenye eneo lake anapitiwa na tembo. Unakuta tembo hao kama hawajaua watu, tembo hao kama hawajakanyaga mazao, kama hawajavunja nyumba, tembo hao kama hawajaharibu miundombinu ya barabara, si tembo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunachotaka hawa tembo watengenezewe mazingira ya kimkakati, tunajua tembo wanamanufaa, tembo anasaidia watalii wanapoingia kutafuta tembo alipo, pesa za kigeni zinaingia, lakini pamoja na kuingia pesa za kigeni madhara tunayoyapata kama wananchi ni makubwa. Akikanyaga mazao watu watapewa fidia, either ya chakula na vitu vingine. Chakula kitatolewa, lakini mtu huyu anapouawa compensation yake ni kitu gani, uhai hakuna kitu kingine? Kwa hiyo, hili ni lazima tuliangalie kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka nizungumzie tu kwenye Jimbo langu la Mchinga. Jimbo la Mchinga hili lina shida kubwa sana sana ya tembo, tembo ni wengi. Kila kukicha unapata adha ya tembo. Ukienda Kata ya Kiwawa tembo ndiko wanakolala, ukienda Kata ya Milola usiseme, ukienda Rukanda tembo wamejaa, ukienda Nangaru kutwa watu wanahangaika na tembo. Lakini tembo hawa tunaambiwa watu walime mazao ya chakula na biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kama tembo huyu akija kwenye eneo kazi yake kubwa ni kutingisha either mikorosho au minazi, mtu ataweza kulima? Na tembo anatingisha mnazi, nazi zikianguka kazi yake huyu tembo kula hizo nazi, anakula nazi. Kwa hiyo, matokeo yake hakuna mashamba hata kwenye mazingira yale ambayo wanalima mazao ya kawaida ya bustani, akija kwenye shamba bustani ya tikitimaji, matikitimaji yale yote yanaliwa hakuna hata moja linalobaki. Hao ndiyo nani hao, ndiyo tembo hao. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, upande ule wa kwetu kule kuna njaa kwa ajili ya hawa wanyama tembo hawa. Tembo si rafiki, tena ilifikia hatua tulipokwenda kule mchinga wanasema sasa tuambieni sisi binadamu na tembo nyie mnamtaka nani? Basi kama mnamtaka tembo nendeni kachagueni tembo sisi hatutaki. Wananchi wanafikia kusema hivyo tuchague tembo… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa hebu weka hicho kisemea chako vizuri.

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, yaani watu wamechoka na tembo, ikafikia hatua mama unatuambiaje au tuwauwe hawa tembo? Nikawaambia hapana hiyo sio sheria msiwauwe hawa tembo waacheni sheria zinatekelezwa, sasa kwa muhktadha huo tuliomba na Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja Milola tukafanya mkutano, kuangalia hali halisi ya tembo na akakuta kuna mtu ameuwawa na Mheshimiwa Naibu Waziri akaenda kumpa pole, nilikuwa naye mimi mwenyewe na baada ya hapa wakasema watatoa kifuta machozi mpaka leo kifuta machozi hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wale wanadai kifuta machozi, kwa hiyo hali ya tembo sio nzuri kwa sababu watu wengi wamezungumza kuhusu tembo nafikiri nimeeleweka lakini kubwa tuna hitaji kituo cha askari wa wanyamapori, lakini wakasema tutawapa kituo hivi unatupaje kituo, polisi wawili na tembo wako 30 hivi polisi huyo wataweza! (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, hawawezi.

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, polisi hawezi matokeo yake kituo hakijajengwa, polisi wawili, polisi hawana usafiri hawana chochote, hata pikipiki hawana. Sasa tunafanyaje?

Mheshimiwa Waziri ukija hapa unihakikishie kwamba kile kituo tutajenga na polisi mtatupa na polisi wenye silaha, sasa hivi ukienda Jimbo la Mchinga mengine haya hayazungumzwi yanazungumzwa masuala ya tembo, niishie hapo kwenye tembo.

Mheshimiwa Spika, tunakuja kwenye eneo la utalii; eneo la utalii kuna sehemu inaitwa Tendaguru, Tendaguru ndio sehemu ambako ametoka huyu mjusi mkizungumzia mjusi anafikiria kama kimo chake kama mimi, mjusi huyu ni zaidi ya hili jengo mara mbili, huyo Dinosaur asili yake ni Lindi kwenye Manispaa ya Lindi kwenye Jimbo la Mchinga eneo linaloitwa Tandagulu na Tandagulu hii iko katika Kata ya Mipingo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaishukuru Serikali leo hii wameanza kujenga information center, watu wakitoka watakuja pale kupata habari kwenda huko Tendaguru, lakini Tendaguru huko wanafikaje? Barabara ni mbovu mbovu ajabu, sasa wakati information center inajengwa tunaomba na barabara ile ijengwe. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja pale, Mnyangara daraja lile linakaribia kwisha, kwa hiyo, daraja likiisha na ile barabara ya kuelekea kwenye eneo ambako huyu mjusi amezaliwa watalii wanataka wajue Ujerumani ndiko aliko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa watu wakitoka Ujerumani wajue wapi ametoka kila mtu ana asili yake na ndio maana watu duniani wanatafuta vinasaba, kinasaba cha yule ni kule.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo yote niwashukuru wale ambao wametupa ardhi, kuna akina mama na akina baba wametoa ardhi heka nane.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)