Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Awali yayote nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama mbele ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Dada yangu Pindi Chana pamoja na Naibu wake Waziri Mary Masanja, Katibu Mkuu wa Wizara hii Dkt. Francis Michael na Naibu wake Juma Mkomi kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, nitapenda kuanza mchango wangu kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan juu ya suala zima la Royal Tour. Royal Tour imeifungua na kuitangaza zaidi nchi yetu, vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini lakini pia sambamba na hilo Royal Tour imeweza kuongeza fursa za uwekezaji na utalii hapa nchini kwetu. Hivyo ni muhimu sana Royal Tour ifanyike kwa kasi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matokeo ya Royal Tour leo tumeweza kuongeza watalii wengi zaidi, tunaambiwa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Kilimanjaro kwa miezi mitatu ijayo hoteli zipo full booked kwa ajili ya kupokea watalii kuingia nchini. Lakini kwa upande wa ndege wameongeza flight mfano, Emirates kutoka tatu kwa wiki mpaka saba kwa wiki, Qatar kutoka saba kwa wiki mpaka 15 kwa wiki. Hii ni hatua kubwa sana ama ni matokeo makubwa sana ya Royal Tour. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ingawa lengo la Royal Tour si kuongeza tu watalii pia tunahitaji investment pamoja na biashara ili kukidhi mahitaji ya watalii wetu hapa nchini. Kama hivyo ndivyo watalii wetu hapa nchini watahitaji hoteli nzuri, rest house, vivutio vya huduma muhimu, barabara nzuri, usafiri wa ndege wa uhakika, wahudumu wazuri interms of customer care. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vema Bunge lako likafahamu utalii ama Wizara hii ya Utalii can’t stand alone ili kuweza kufikia mkakati sawasawa wa masuala mazima ya utalii hapa nchini. Hivyo basi Wizara kama Miundombinu, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Mawasiliano na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ni lazima zizungumze lugha moja ili tuweze kufikia malengo tarajiwa ya sekta nzima ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa na kazi nzuri sana ya kuhakikisha milango ya utalii inafunguka na imefunguka kwelikweli. Tumeona kwenye filamu ya Royal Tour kupitia hapo kisiwa chetu cha Zanzibar kimeweza kupata watalii wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, alternative ya utalii hapa nchini ukiacha Kisiwa cha Zanzibar ni Kisiwa cha Mafia Mkoani Pwani, Kisiwa cha Mafia Mashallah Mwenyezi Mungu amekijalia kina beach ama fukwe nzuri sana, lakini pia kuna samaki yule wa ajabu mwenye madoido anaitwa whale shark ama papa potwe ambaye wazungu wanampenda sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna sport fishing, nikisema nielezee vivutio vilivyopo katika kisiwa chetu cha Mafia nitapoteza ama nitachukua muda mwingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, isipokuwa kwa masikitiko makubwa kabisa as we are speaking here over 90 percent ya ardhi ya Kisiwa cha Mafia hakijapimwa. Leo tunazungumzia suala la uwekezaji, tunazungumzia suala la biashara; ni mfanyabiashara gani, ni mwekezaji gani atakuja kuwekeza kwenye ardhi ambayo haijapimwa. Tunajua wazi hakuna mwekezaji wa namna hiyo, wenzetu wanavyotaka kuwekeza wanahitaji wawe na title, sasa kama hatuna title, kama eneo hatujapima tusifikiri kama tunaweza kupata hao wawekezaji.

Kwa hiyo, mimi nataka niwaombe sana Serikali hususani Wizara ya Ardhi iangalie namna ya kupima maeneo haya mahususi kama vile Kisiwa cha Mafia ili tuweze kukifungua kwa upande wa utalii. Hakuna biashara ya utalii isiyoendana na hoteli, migahawa pamoja na fukwe nzuri za beach. Sasa kama hatujapima ardhi yetu itakuwa tunapoteza wakati na ndiyo maana nikasema ni vema Wizara hizi zikazungumza lugha moja ili tuweze kuufungua utalii pamoja kisiwa chetu cha Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukizungumza habari ama biashara ya utalii mimi nitaomba Serikali ikija inieleze mipango na mkakati wa kuhakikisha inakipanua kiwanja cha ndege cha Mafia. Kiwanja cha ndege cha Mafia ni kidogo chenye runway ya mita 800 kimsingi ndege kubwa haziwezi kutua pale na tunafahamu watalii wanapotoka eneo la utalii wanataka waende straight kwenye destination na wakitoka hapo waongoze moja kwa moja kwenda eneo wanalotaka kwenda kutalii. Wazungu hawapendi mambo ya transit, kwa msingi huo tunaweza tukapoteza baadhi ya watalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nataka niombe sana Serikali ije na mipango ya kuhakikisha kwamba inapanua kiwanja hiki cha ndege, lakini pia tuweze kujenga barabara ya lami iliyokuwa kule Mafia ya Ras Mkumbi kilometa 55. Mtalii anapoingia, ametua kwenye ndege anapoingia kwenye gari kuelekea hotelini barabarani vumbi tupu. Kwa hiyo, lazima tujenge miundombinu yetu ili tuweze kuifungua sekta hii ya utalii. Lakini kisiwa cha Mafia kina visiwa vidogo vidogo kama Chole, Jibondo na vinginevyo, kwa hiyo, mtalii kutoka kisiwa kimoja mpaka kwenda kisiwa kingine tunahitaji tupate vyombo vya kuwachukua kama speed boat. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwahiyo, nitaomba sana Serikali ije na majibu ya kujibu hizi changamoto ya namna gani tunakifungua kisiwa cha Mafia kwa ajili ya kuchochea utalii. Niombe sana kwamba Royal Tour inaendelea, episode ya pili ama season ya pili, nataka kuomba sana ipige jicho lake kwenye kisiwa chetu cha Mafia ili na yenyewe iweze ku-appear kwenye hii filamu ya Royal Tour.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi mwisho nimalizie na ombi ama ushauri kwa Serikali. Royal Tour kwa ushauri wangu mimi ni vema ikakabidhiwa ama ikawa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na si kule Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo licha ya kwamba Serikali ni moja tunakubali, lakini ili iweze kusimama vizuri ni vema ikawa mikononi mwa Wizara ya Maliasili na Utalii na si kwenye michezo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)