Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi nimefika na mambo mawili tu ya kuzungumza leo; jambo la kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa Royal Tour ambayo imefanyika Tanzania, kazi ambayo ameifanya Mheshimiwa Rais ni ya kuitangaza nchi, lakini pia kuisemea, lakini amefanya kazi kubwa sana ya kuutangaza Mlima Kilimanjaro kwa sababu kuna watu waliaminishwa kwamba Mlima Kilimanjaro hauko Tanzania upo Kenya lakini kwenye kupanda mlima ule ameitangaza nchi, lakini vilevile sisi watu wa Serengeti wakati ule wa nyumbu anapokuwa anavuka Wakenya wanapanga ratiba wanasema nyumbu ni wa Kenya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Rais alienda Serengeti na akaonesha kwamba ile ni sehemu ya Tanzania na Mbuga ya Serengeti inaendelea kushamiri. Lakini vilevile ni muhimu watu wakajua kwamba kitendo cha Mheshimiwa Rais pia kuweka wazi mikakati ya kupambana na Covid-19 ilisaidia sana kufungua nchi, lakini pia na watalii kuongezeka. Wenzetu wanataka kujua kama kuna tatizo namna ya kuweza kuliondoa na kupambana nalo, hiyo pia ilisaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini zipo faida mbalimbali ambazo pia tumepata kama nchi na Mheshimiwa Rais amesaidia ndege nyingi za kitalii na za kimataifa kuongezeka kuja hapa Tanzania kwa mfano tarehe 4 Juni yaani kesho Eurowings Discovering wataanza kutoka moja kwa moja Ujerumani kuja hapa KIA na watabeba watalii 300 kwa wakati mmoja watakuja mara mbili kwa wiki, lakini tarehe 20 Juni, 2022 Dutch Airlines watatoka direct kule na kuja moja kwa moja KIA na kuongeza idadi ya watalii, kwa hiyo ni faida ambazo zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, abiria wameongezeka lakini pia miruko ya ndege imeongezeka katika eneo hili, lakini vilevile mashirika mapya yameongezeka kuleta ndege zao pale, lakini mapato ya Serikali yameongezeka katika eneo hili na ajira rasmi na ambazo sio rasmi zimeongezeka, hiyo ni baadhi tu ya faida ambazo tumepata kutoka kwa hao watalii. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana tunaomba aendelee nayo.

Mheshimiwa Spika, lakini sisi watu wa Tarime tunamshukuru Mheshimiwa Rais ametoa fedha kujenga kilometa 89 kutoka Tarime mpaka Mugumu Serengeti, kwa hiyo hata kama kuna watalii kutoka Kenya kule watavuka pale wataenda pale Kibaso na Marariet na kuweza kutoa huduma na fedha itaongezeka na uchumi utaongezeka katika eneo lile.

Mheshimiwa Spika, ninachoomba katika eneo hilo la Royal Tour Wizara iongeze package ya Kiswahili kama sehemu ya utalii, kama inawezekana wale wenzetu wakija hapa kwetu tu wapate crash program ya kufundishwa Kiswahili ili wakienda wajue kwamba Kiswahili kipo Tanzania na sisi ndio wataalam wa Kiswahili, kwa sasa ilivyo katika somo huko duniani Wakenya wanapata ajira kubwa sana ya Kiswahili kana kwamba wanakijua kuliko Watanzania, kwa hiyo tutumie fursa hiyo kutangaza Kiswahili chetu, vijana wapate ajira lakini pia ipatikane ajira ya ukalimani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo kwa kweli mambo yote mazuri hayo ya Royal Tour yanaharibiwa na migogoro iliyopo katika maeneo yetu. Kule kwangu Tarime Vijijini Mheshimiwa Rais alikuta Tume ambayo ilikuwa imeundwa na mtangulizi wake Mheshimiwa Magufuli akafanya maamuzi akaelekeza Mawaziri nane waende kwenye maeneo yetu kutatua changamoto. Nasikitika kusema mpaka leo tangu nimezungumza hapa hotuba ya Waziri Mkuu, Wizara hatujawasiliana wala wahusika na kule katika eneo la mgogoro hawajafika kwa hiyo, watu wangu wanalalamika, lakini vilevile kuna vijiji 975 ambavyo vinahusika katika maeneo mbalimbali zaidi ya mikoa 10 na kitu ambayo ina mgogoro wa ardhi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni jambo kubwa ambalo Wizara lazima ilibebe na ilifanye, kama Mheshimiwa Rais amesimamia Royal Tour imeanza inafanya kazi, watalii wanakuja, ndege zinaongezeka, lazima tutatue migogoro ya wananchi wetu, itakuwa haina maana sana kama tunapata faida ya watalii kuongezeka halafu migogoro ipo katika maeneo yetu, inatia doa katika kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais amefanya, hivyo Mheshimiwa Waziri unayo kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ningechangia tofauti sana kama mwenzako mtangulizi angekuwa amekaa hapo, nilimuomba mara kadhaa tangu mwaka 2020 aende pale Tarime aende pale Nyanungu, aende Gorong’a aende Kwihancha, hawajawahi kwenda kuwasilikiza wananchi wangu na wanalalamika katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Tarime ina kata tatu ambazo zina mgogoro na Hifadhi ya Serengeti na tuna vijiji saba, huu mgogoro pia unagusa watu wa Bunda, inagusa watu wa Serengeti, inagusa watu wa Butiama inaenda mpaka Rorya utaona ni sehemu kubwa sana ambapo tungepanga haya mambo…., ukienda Kijiji cha Masanga, Kenyamosabi, Kegonga, Nyandage, Karekatonga, Kibaso, Nyabirungo huku kote kuna migogoro mikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hawaishii hapo, nataka niseme tu kwamba yapo mambo ambayo yamefanyika katika eneo la Tarime yametesa sana watu wangu, kwa mfano kuna maeneo ambayo watu wameuawa, unashangaa mtu analishwa mizoga, watu wanalishwa pilipili mpaka wengine wamekuwa vipofu, lakini pia wanachoma nyumba wa watu, wanaharibu mazao ya watu. Hili jambo sio jambo zuri. Kwa mfano ukienda Kata ya Gorong’a kuna watu 10 wameuawa, Wanene Masyaga, Chacha Nyahiyo, Nchakwa Chacha Mahanga, Chacha Mwita Magori, Lucas Gasaya Marwa, Manga Wankyo, Wambura Chacha Mwaisori, Mwita Ryoki, Woryo na Manga Karumanga hii ni kata moja tu watu 10 wameshauawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kata ya Nyanungu kuna watu watano; Nyang’anyi Chacha, Mwita Nyangaya, John Sensema, Marwa Sasi, Mwita Chacha Mugesi hii miili mingine ilipotea ili kupoteza ushahidi, na Tume zimeundwa nyingi sana hapa sio sawa waliokufa, waliopigwa risasi, tunao watu hapa saba Chacha Magalya, Woryo, Seerya Magaiwa, Matiko Gesabo, Emaru Moseti, Boke Waisiko, Chacha Mwiniko hawa wamepigwa risasi wapo ni walemavu.

Mheshimiwa Spika, Tume zimeundwa nyingi, bahati mbaya katika eneo hilli unaunda Tume ambayo gari lenyewe tunawalalamikia watu wa TANAPA Serengeti wanatoa gari, wanatoa posho, wanatoa hoteli, wanaandaa chakula, ripoti zote hazijawahi kutoka, nikisema hayo mambo utafikiri natunga. Ningeomba Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili aende katika Jimbo la Tarime Vijijini aone kwamba mambo haya ni ya uongo au ni ya ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya ninayoyazungumza yapo na nimewaandikia barua wahusika wa Wizara hii kwamba nendeni mkawasikilize, ukienda kwenye mipaka ya hifadhi nililalamika kwamba mmechukua greda, mmelima barabara katikati ya mashamba ya watu, lakini mashamba yale…

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mwita kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

T A A R I F A

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nimshukuru mchangiaji anayechangia, naomba tuweke kumbukumbu sawa, nampa taarifa kwamba anaposema Mawaziri hawajafika katika mikoa iliyotembelewa mara mbili kwa ile timu ya Mawaziri Wanane mkoa wake ni mmojawapo ambao tumeenda mara mbili, timu ya kwanza ilienda ikiongozwa na Mheshimiwa Lukuvi walienda mpaka vijijini, ile ya pili tumeenda tumeongea na ule uongozi wa mkoa na maelekezo yote yametoka. (Makofi)

Kwa hiyo, anaposema hawajaenda aweke kumbukumbu vizuri kwa sababu tunaweza tukapotosha kwa kitu ambacho sio sahihi sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sina nia ya kutaka kubishana na Mheshimiwa Waziri dada yangu Dkt. Mabula, ninachosema kwamba walienda Musoma wakaishia Musoma Mjini hawakwenda Nyanungu, hawakwenda Gorong’a, hawakwenda kwa wananchi, na mgogoro uliopo ni kwamba beacon ambazo zinatangazwa GN 235 ya mwaka 1968 wananchi wanabishania kwamba siyo kweli. Kwihanja walipokwenda wataalam wakakutana na viongozi wa wananchi wale wazee, wakawaonesha na beacon, leo mgogoro umekwisha pale Kwihancha, hapa sehemu ya Gorong’a na Nyanungu ni kwamba beacon wanasema ni za kwao, ni eneo la hifadhi, wananchi wanasema hapana tunakaa hapa, watu wamezaliwa pale miaka 80 unaishi hapo, ukienda ukakaa nao watakuonesha document zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri eneo hili kuna watu ambao wamezaliwa wameongoza miaka 20 Udiwani wapo hadi leo. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri na wenzake wa Maliasili na Utalii watume watu waende waongee na wale wazee au niwalete hapa uwasikilize ndio hoja iliyopo.

Mheshimiwa Spika, lakini ipo mifugo imekamatwa, kwa mfano Nyangage watu 20 wameathirika na kukamatwa mifugo yao…

SPIKA: Mheshimiwa Waitara ngoja, kabla haujahamia kwenye mifugo unajua nilikuwa naisikiliza hoja yako ili nielewe unaelekea wapi, umetaja hapo watu waliouawa, umetaja hapo watu waliopigwa risasi kwa maana ya kwamba wameumizwa. Huyo anayeyafanya hayo ni nani maana hayo mambo ni mazito sana, anayeyafanya hayo ni nani?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, mambo yote hayo ya risasi na mauaji watuhumiwa wanaolalamikiwa ni wa Hifadhi ya Serengeti kwa sababu watu wanapotea kwamba wameenda kuchunga halafu hawaonekani na ilikuwa ng’ombe wamekamatwa, lakini mtu haonekani, kwa hiyo wanaotuhumiwa hapa ni Hifadhi ya Serengeti, sasa nani specific kwa maana ya majina…

SPIKA: Ngoja, ngoja, kama hizo ni tuhuma mbona wewe umezisema kana kwamba inajulikana kabisa kwamba ni nani aliyefanya hayo mauaji na ni nani aliyepiga hizo risasi.

Kwa sababu hili ni Bunge, ukisema mambo mazito kama hayo na kwamba kuna Tume hazijawahi kufanya chochote na hayo mambo hayajatokea jana wala leo, sasa hebu liweke vizuri ili mimi nijue nini cha kuiagiza Serikali hapa.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sijataja majina ya watu hapa, ninachoomba hapa ni kwamba haya ni malalamiko ya wananchi na majina yapo na Tume zimeundwa kwa mfano huyo Manga Kahurumanga ni mwaka jana, Mkuu wa Mkoa aliunda Tume na mimi nilikuwepo, ripoti mpaka leo hayajatoka. Kwa hiyo, hayo yote yamefanyiwa kazi majibu kwa wananchi pale hakuna.

Kwa hiyo, nitaomba utusaidie kwamba viongozi wa Serikali na hasa wa Hifadhi ya Serengeti haya malalamiko wayafanyie kazi yakome yasiendelee, yaani watu wasipotee katika mazingira ya kutatanisha, ndio ombi langu.

Mheshimiwa Spika,...

SPIKA: Ngoja, ngoja.

Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu tuhuma hizo ni nzito sana na tuhuma zinaelekezwa kwa chombo cha Serikali.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, tuhuma anazozitoa Mheshimiwa Mbunge katika kuchangia ni nzito kwa kweli na mimi nakuelewa kwa nini unataka upate angalau nini ambacho Serikali inasema.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ni kiongozi tena wa muda mrefu na uwakilishi wetu sisi kama Wabunge sio kusema tu ndani ya Bunge, ipo mifumo mbalimbali ambayo tunakutana na Wabunge na Serikali. Sasa kulileta hapa jambo zito kwa maelezo ya namna hiyo mauaji, risasi, hakuna kinachofanyika ni tuhuma nzito ambazo kwa kweli pengine zinahitaji tafakari, lakini pia kwa nafasi ya humu niseme tu kama anazo tuhuma mahsusi si vizuri kuzisema kwenye chombo hiki kikubwa badala ya kuwa tumekutana na tukapata hizi information na utafiti ukafanyika, tukajua kweli ni vipi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu mtu akipotea haina maana mtu ameuwawa kuna watu chungu mzima hapa wana ndugu zao wamepotea. Hata mimi mwenyewe kwetu kuna watu wamepotea, sasa sio akipotea ameuawa na mtu fulani au na watu fulani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nadhani ama atuhakikishe hilo analolisema na kama anaweza kuonesha ushirikiano na Serikali katika kueleza hayo yote anayoyasema au afute maelezo haya yasiwe sehemu ya mchango wake. (Makofi)

SPIKA: Sawa, sasa Mheshimiwa Mbunge yeye ameeleza kwa kirefu na mimi nilikuwa ninamsikiliza ili nielewe hoja yake inaelekea wapi na kabla hajahamia kwenye mifugo kuna hoja nzito ya watu waliopigwa risasi ambao maana yake kwa maelezo yake yeye na amewasoma hapo majina maana yake wapo waliopigwa hizo risasi kwa maelezo aliyoyatoa yeye, lakini pia amesoma hapo majina akisema hawa watu wameuawa. Maana yake kwa maelezo yake yeye anao ushahidi kwamba wameuawa kwa sababu hauwezi kusema mtu ameuawa kama amefariki, wanaofariki wapo wengi watu wanaumwa malaria na nini ukisema mtu ameuawa maana yake lazima kuna ushahidi unaoashiria kwamba kuna mtu amemuua mtu mwingine.

Sasa kwa sababu hili jambo ni zito kwa kweli na tupo kwenye Wizara hapa wakiwa wameleta hoja hapa ili tuwapitishie jambo lao, sasa Mheshimiwa Waitara huo ushahidi ulionao kuhusu mambo haya, wewe niletee mimi huo ushahidi ulionao, halafu huo ushahidi ulionao ukishaniletea mimi nitaiagiza Serikali kwa sababu siko nao huo ushahidi hapa. (Makofi)

Kwa hiyo, niletee ushahidi ili mimi niiagize Serikali kuhusu jambo hili kwa sababu tuhuma hizi ni nzito sana ulizozitoa hapa ndani. Malizia mchango wako. (Makofi)

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na nitafanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa ninasema kuna mifugo ya watu inakamatwa kwa mfano nimesema Kata ya Nyandege watu wameathirika mifugo yao, Tyegonga watu 18; Korong’a watu 17; na hayo yote ya mifugo kuna malalamiko makubwa sana, jambo baya lililofanyika pale ni kwamba wanakamata mifugo ya watu hawa ni jamii moja; mjomba, shangazi, sisi ni wale wale, halafu wanapeleka pale Kibaso kwenye uwanja wa wazi wanapiga mnada ng’ombe za watu.

Mheshimiwa Spika, unajua katika maisha yetu kama mtu alikuwa analimia ng’ombe zake halafu wamekamatwa wakaenda wakauzwa, mwenzake akachukua unatangaza watu waanze kuuwana.

Mheshimiwa Spika, ningeomba pia hata kama ni faini au hata kama ni kuuza wasiuzie pale pale katika maeneo yale yale ya jirani wapeleke sehemu nyingine kama ni lazima wauze mifugo ya watu. Nitaomba sana hapa kwamba watu wa Hifadhi ya Serengeti wanatakiwa watoe huduma na ushirikiano kwa watu wale wanaokaa karibu na Hifadhi ya Serengeti, waliahidi CSR lakini maeneo haya hakuna maji, hakuna malambo hakuna zahanati...

(Hapa kengele ililia kuahsiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Mwita Waitara kengele ya pili imegonga, nakupa dakika mbili umalizie mchango wako.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kwamba kwa kuwa hawa watu wa hifadhi wanafanya shughuli pale, ugomvi ulipo kwenye kata yangu na ni ugomvi mkubwa ni kwamba pale wakati wa kiangazi hakuna malambo, yamekauka, hakuna mito tofauti na Mto Mara, hawa wa hifadhi waliahidi kwamba wangechimba malambo katika eneo lile ili wakati wa kiangazi mifugo ipate maji, wasiende kwenye Mto Mara, katika hali ya kawaida kama hakuna alternative wakati wa kiangazi watu wataenda kwenye Mto Mara, wataenda kulisha ng’ombe na kuchota maji, ugomvi unaanzia pale, wanakamatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho ningeomba kwamba yapo mambo mengi katika Hifadhi ya Serengeti, tunapenda kuunga mkono Serikali kwa kazi nzuri, lakini naomba Mheshimiwa Waziri kwa dhati kabisa ni mpya kwenye Wizara hii, lakini ningeomba jambo la kwanza twende pale mambo ninayozungumza hapa siyo kwa kwangu, wanipe nafasi ya kwenda kukaa na wananchi, awasikilize, aone hata hizo familia azitembelee, utagundua kwamba kuna shida kubwa pale Tarime na kwa kweli naomba msaada wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba ulibebe jambo hili kama mzazi. Kule kuna kilio kikubwa sana, migogoro ya ardhi hapa ni karibu kila Mkoa, Waziri lazima ajipange. Kazi nzuri ya utalii ili ifanyike vizuri lazima migogoro kwenye majimbo itatuliwe, twende tuwasikilize watu, kama ni kusogeza mipaka bahati nzuri Mheshimiwa Rais ameonesha njia jambo hili siyo jema, tunataka mapato ya utalii, lakini watu wetu pia waendelee kuishi kwa amani na kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)