Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nishukuru kwa nafasi hii ya kuichangia Wizara hii ya Utalii, Wizara ambayo tuna interest nayo sana kwenye Mkoa wetu wa Kilimanjaro, lakini nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa lile tukio la Royal Tour. Wapo watu wengi ambao bado wanabeza, lakini na mimi niungane na wale wanaomtia moyo Rais kwa sababu tayari amethubutu na amefanya na matokeo yameshaanza kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu kwa kazi ambazo wanaendelea kufanya katika Wizara yao ambazo zinaleta matokeo chanya kwa nchi yetu. Mimi nina mambo machache ya kuchangia, nianze na jambo ambalo nilishalileta kwenye swali, la CSR.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yale yenye migodi zile halmashauri zinazozunguka ile migodi zinapata kiasi cha fedha asilimia fulani ambayo ni CSR kwa ajili ya maendeleo yao pale pembeni kwa wale wanaozunguka ile migodi. Sasa maeneo yanayozunguka haya mapori pamoja na vivutio vya utalii ni muhimu sana na wao waweze kupata kiasi fulani katika yale mapato ambayo yanapatikana kwenye utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakupa mfano, Mkoa wa Kilimanjaro kuotesha mti ni hiyari, lakini kukata mti ni mpaka uwe na kibali cha Mkuu wa Wilaya na ni kwa nini tunafanya hivyo? Ni kwa sababu miti kule inahitajika sana kwa ajili ya kutunza uoto ule wa asili na kutunza mazingira ya ule mlima ikiwa ni pamoja na theluji yake. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema asilimia 85 ya nishati inayotumika nchini inatokana na mazao ya misitu ikiwa ni mkaa, kuni na vinginevyo. Sasa kule Kilimanjaro haturuhusiwi kukata hiyo miti hata kama unataka kuangukia nyumba, process yake ni ndefu. Sasa mkitusaidia CSR itawasaidia halmashauri kuangalia namna mbadala ya ku-subsidize maisha ya hawa watu ili wasitumie hiyo nishauti na badala yake watumie nishati mbadala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie maneno ambayo wameyaongelea Waheshimiwa wawili, Mheshimiwa Neema Mgaya pamoja na Mheshimiwa Swai kuhusiana na kodi nyingi na mimi hili silifunganishi tu kwa kuwaongezea faida wale wadau wa utalii, lakini zaidi ninafikiria kwamba tukiwapunguzia mzigo na biashara hii ya utalii ni seasonal, ina maana na wao wataongeza maslahi kwa wale watumishi wao kwa mfano wapagazi ili waweze kwa sababu, watu hawa wamekuwa wakipata mishahara kipindi ambacho ni high season, kipindi ambacho ni low season wanakuwa wanatangatanga na maisha yao yanakuwa magumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ili hawa wanaojihusisha na kazi hizi za utalii kama wapagazi, waongoza watalii, waweze kupata kipato hasa kipindi cha low season ni vizuri tuwapunguzie mzigo hawa wafanyabiashara ya utalii ili na wao waweze kuishusha hiyo faida chini na wale watu waweze kupata mafao yao bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na debate kali kwenye mitandao na mengine makongamano yamefanyika mpaka kule Moshi kuhusiana na cable car. Na mimi niwasilishe mawazo ya pande zote mbili, upo upande unaosema cable car ije na wao wanasema ni aina mpya ya utalii na inahusiana na watu ambao hawapandi mlima na nia yake sio kupeleka watu kileleni, bali ni kuwapeleka eneo ambalo wanaona mandhari nzuri na kuwarudisha. Kwa hiyo, kwao wao ni nyongeza kwenye pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini upande wa pili wapo ambao wanasema cable car inatakiwa ipandishe watu mpaka kileleni, itapunguza ajira, itapunguza siku ambazo mtalii anakaa kule mlimani, itapunguza kipato cha Serikali; na mimi nasema kama ni cable car ya namna hiyo basi hatuna budi kuisimamisha, lakini ninaomba Wizara ifanye tathmini nzuri, ifanye mawasiliano na makongamano pamoja na wafanyabiashara na wadau wengine tuone ni kitu chenye tija, hata ikibidi sio lazima aje mtu kutoka nje kuwekeza kwenye cable car, kama haidhuru mazingira yetu na kama ni kitu ambacho kitatuongezea kipato badala ya kupunguza, kitaongeza ajira badala ya kupunguza, Serikali inaweza kufanya yenyewe badala ya kuachia mtu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunaweza kujenga reli ya SGR, kale ka-cable car sidhani kama ni kitu ambacho tunashindwa. Na mifano iko maeneo mengi duniani ambapo calbe cars zimekuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niongelee park fees ambazo nimeziongelea pia kidogo hapo nyuma. Inashangaza kwamba park fees zetu upande ambao uko busy kama ile Northern Circuit bado hazitofautiani sana nah uku Southern Circuit. Mimi naishauri Wizara ili kuongea idadi ya watu kule maeneo ambayo watalii hawaendi kwa wingi kule Southern Circuit na maeneo mengine kile kiingilio (park fees) kingeshushwa sana ili kuvutia watu wengine; kipandishwe pale ambapo tutaona watalii wamekuwa wengi ili kifanane nah uku kwingine. Kwa hiyo, kuna haja ya kuangalia yale maeneo yaliyoko busy warekebishe kidogo, lakini maeneo ambayo hayako busy washushe kabisa kiingilio. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niishauri Wizara suala la conference tourism, inajulikana kama MICE, ni sekta ya tourism ambayo basically inafungamanishwa na sekta nyingine, ni utalii wa mikutano. Sasa najua wao kama Wizara hawahangaiki na suala la mikutano, lakini wanaweza wakafungamana na Wizara nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano NSSF wanajenga majengo makubwa tu, lakini ni dhahiri wakijenga kumbi za kisasa za mikutano kwa mfano pale Moshi itaongeza idadi ya watu wanaokuja kwenye mikutano na huo ni utalii, lakini watu hao wakimaliza mikutano wanaenda kwenye vivutio vyetu kutalii. Ni sehemu ambayo inakua sana, utalii wa mikutano unahitaji kufungamanishwa. Ni vizuri sana Wizara ianze kuangalia namna ya kuwasiliana na Wizara nyingine kuiwekea hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili haliwahusu utalii peke yao, suala la intellectual property na copyrights. Magari haya ya utalii ambayo yamekuwa modified yalianzia Moshi kwenye kampuni ambayo inaitwa Rajinda Motors na walitaka wapewe copyright na intellectual properties za ubunifu wao, lakini Serikali imekuwa ikiwapiga chenga, sasa hivi yanakuwa duplicated kila mahali na sisi hatupati kitu chochote cha ziada. Nilikuwa nashauri inapotokea mtu amebuni kitu, hata kama sio kwenye utalii, lakini kwenye idara yoyote, aweze kupewa nguvu na Serikali, alinde ule ubunifu wake kama ilivyo kwa wale Rajinda Motors ambao walibuni haya magari ambayo ni extended kwa ajili ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la rescue services kwenye Mlima Kilimanjaro. Kuna wafanyabiashara walikuwa na helicopter pale Moshi Airport na ilifanya vizuri sana kwa sababu watu wakija wanachangia, incase akipata shida ile helicopter inafanya rescue. Sasa hivi haipo kwa sababu, baada ya uvico mfanyabiashara yule ilibidi ashindwe ile biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa nashauri Serikali, kama inaweza inaweza kuifanya hii huduma kwa kushirikiana na NHIF pamoja na kampuni nyingine ambazo zinaweza zikafanya ile huduma. Ni huduma muhimu inaweza ikatumika hata nje ya huo utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)