Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kupata nafasi hii. Awali ya yote nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Pindi Chana, Waziri pamoja na timu yake yote ikiwa ni pamoja na Naibu Waziri kwa dhamana kubwa hii ambayo Mheshimiwa Rais amewapa ya kuongoza Wizara hii ambayo kwanza inabeba uchumi wa nchi, lakini pia inabeba taswira ya nchi yetu. Mheshimiwa Pindi Chana kwa kiasi kikubwa nakufahamu tumefanya kazi pamoja kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa, mzigo huu ni size yako kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mary Masanja dada yangu tulikuwa wote kwenye mapambano ya tembo kule kwenye Jimbo langu yalipoanza pamoja na kwamba yanaendelea nitakueleza, lakini niliona uwezo wako, mzigo huu wa kumsaidia Mheshimiwa Pindi Chana ni size yako kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongelea maeneo mawili; moja kuhusiana na Jimbo langu lakini la pili nitazungumza juu ya habari ya Royal Tour. Jimbo langu linapakana na mbuga za wanyama mbili moja, ni Tsavo ya Kenya halafu na Hifadhi ya Mkomazi ya hapa kwetu Tanzania. Tumekuwa na changamoto kubwa sana ya tembo na kwa kweli kwa juhudi ambazo Wizara imeshafanya mimi nawapongeza. Lakini mimi kwa kweli sasa hivi kilio changu kikubwa ni kwamba linapotokea janga kama hili watafiti wetu tunawasikiliza wanasema nini? Vyuo Vikuu vyetu vinasemaje juu ya janga hili ambalo limekaa muda mrefu kiasi hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama basi tumefikia hapa, mimi ningeshauri Wizara kwa kweli labda mtangaze package kama iliyotangazwa na Wizara ya Elimu juzi kwamba, atakayeweza kutoa chapisho likaenda kwenye majarida fulani mashuhuri atapata fifty million shillings basi na hapa nadhani mngetangaza boom ili watafiti wetu waingie kazini kwa sababu hali haifurahishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikwenda na Mheshimiwa Naibu Waziri kule hali haikuwa nzuri, lakini pia yako mambo ambayo tuliwaahidi wananchi wa Jimbo la Mwanga ambayo pia kwa namna fulani yangesaidia kupunguza kasi ya tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la lango la Kaskazini la Mbuga ya Mkomazi ile ahadi mpaka leo haijatimizwa pamoja na kwamba iliingia katika utaratibu wa bajeti ya mwaka uliopita. Tunaomba ile ahadi itimizwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na ahadi ya bweni la wavulana katika shule ya sekondari Kigonigoni, ili kuwapunguzia kutembea umbali mrefu kwa sababu ya tembo kwenye eneo lile. Pia kulikuwa na ahadi ya shule ya msingi ya Mbigili kwa sababu hiyo hiyo. Ahadi hizi bado hazijatekelezwa ninawashukuru wenzetu wa TANAPA, juzi juzi wamenitumia taarifa ya kuonesha kwamba zimeingia kwenye taratibu zao za bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mwakilema anatoa ushirikiano sana hasa kwenye upande wa mawasiliano namshukuru, kwa hiyo naomba sasa, ahadi zitekelezwe ili kuendelea kuwapunguzia wananchi hawa machungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kuna suala la kifuta machozi kwa waliopoteza maisha na fidia kwa waliopoteza mazao. Hilo pia bado halijakamilika, tunaomba hayo yatimie, ili tuendelee kupata ushirikiano wa wananchi wa Mwanga katika janga hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye suala la Royal Tour. Royal Tour pamoja na yote mema yaliyozungumzwa lakini ningependa kurudi kwenye historia yake kidogo kwamba ile ni series ambayo huwa inafanyika ikiongozwa na yule ndugu yetu Peter Greenberg ambaye ni mtu mwenye nishani nyingi sana za kimataifa katika eneo hili na ile inatolewa kwanza kwa nchi ambayo ina vivutio mahususi vya utalii na pili nchi ambayo inakiongozi ambaye, amethibitisha kuwa na uwezo mkubwa wa kushawishi katika masuala ya kukuza uchumi. (Makofi)

Kwa hiyo, kwa Royal Tour ile kufanyika hapa ni kwamba tume-qualify kuwa na nchi yenye vivutio hivyo na pia kuwa na Rais ambaye amethibitika kidunia kwamba anaushawishi mkubwa katika kusukuma uchumi wa nchi yake. Kwa hilo, lazima tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa ku-qualify kufikia hapo na hii Royal Tour huwa inaongozwa na wakuu wa nchi, najaribu kusema hivyo kwa sababu kuna watu wanapata shida kwamba kwa nini tusingetumia sijui ma-star wa dunia? Ma-star wa dunia u-star huwa unakwisha, lakini fikiria mpaka leo kuna mahali unakwenda unauliza unatoka nchi gani? Tanzania ni country of Nyerere? Mpaka leo Nyerere bado wanamkumbuka. (Makofi)

Sasa tunajaribu kujenga legacy nyingine ambayo itaendeleza pale ambapo pamebaki ili kuweza kuendelea kukuza uchumi wa nchi yetu. Ilipofanyika Israel aliiongoza mwenyewe Benjamin Netanyahu - Waziri Mkuu, ilipofanyika Poland aliiongoza Waziri Mkuu - Mateus, ilipofanyika Ecuador aliiongoza Rais mwenyewe Raphael Korea, ilipofanyika Mexico aliiongoza Rais Philippe na Rwanda aliiongoza Paul Kagame mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni suala ambalo linaongozwa na Wakuu wa nchi sio kila mtu hapa Mbunge wa Mwanga niende nikaongoze Royal Tour hilo haliwezekani. Nilikuwa najaribu kujibu hilo swali na katika nchi zote hizi ambazo Royal Tour hii imefanyika kwa kuongozwa na wakuu wa nchi uchumi wa nchi zile ulikua sana. Hakuna ubishi kwamba Israel pamoja na kwamba ni nchi ndogo na yenye migogoro mingi, lakini inaongoza katika uchumi na teknolojia. Rwanda hapa katika nchi za Afrika tunaingalia kabisa kwa jicho kwamba ni nchi ambayo inaongoza. Ecuador kuna programu moja imeanza pale inaitwa Four Worlds in One Place, ambapo waliigawanya ile nchi katika Zone nne tu za climate tu, Amazon, Andes, Coast na vile Visiwa vya Galapagos. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vinailetea watalii wengi na uchumi umekua kwa ajili hiyo tu. Sasa Tanzania tuna uwezo wa kugawa hata dunia 40 ndani ya nchi yetu. Ukienda kwenye culture peke yake inatosha kabisa kuvutia utalii, kuna sehemu Pwani huko, ukienda kwetu huko Kaskazini culture ziko tofauti ile peke yake ni kivutio. Hata chakula for that matter, rafiki yangu Musukuma bila ugali kwake hakuna chakula ukimletea ndizi anasema hii ni mboga. Ukienda kwa Mheshimiwa Mwigulu kule wanakula kuku wa kienyeji, lakini ukienda kwa ndugu zangu Wamasai wanasema hawa ndege sisi hatuli na kadhalika. Kwa hiyo, diversity peke yake ya culture ni kitu kikubwa sana ambacho kinauwezo wa kutuletea utalii mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nenda Zanzibar tulikwenda kule kwenye ile misitu ya Jozani, tukakuta wale nyani wekundu ambao dunia nzima unawakuta pale Zanzibar. (Makofi)

Kwa hiyo, sisi hata faru tunao wengi mpaka tuna Faru John na faru wa kila aina na sasa hivi nimeona kuna nyati weupe wamezuka. Kwa hiyo, kwa kweli kwa kutumia sasa hii Royal Tour ambayo imetufikisha hapo, tuna uwezo wa kuipeleka hii nchi next level kwa namna ambayo ni rahisi kabisa. (Makofi)

Ndugu zangu ukisoma kwenye vitabu wafalme wa zamani walitangulia wenyewe vitani, lakini wakitangulia vitani walikuwa wanakwenda pamoja na watu wao. Sasa Rais ametutangulia katika vita hii ya kufufua uchumi wetu kwa njia nyingi ambazo tumeziona hata za miundombinu na sasa ya Royal Tour, lakini sasa tunapaswa kwenda naye, tusiseme tu kwamba ameupiga mwingi sasa akishaupiga mwingi nani atafunga goli? Ameupiga mwingi watalii wamekuja je, Uhamiaji wako tayari pale airport ili kuwapitisha watalii haraka haraka tusianze kupata lawama? Ameupiga mwingi kwenye mahoteli amezungumza mchangiaji mmoja customer service yetu iko namna gani? Ameupiga mwingi watalii wamekuja, barabarani vizuizi vyetu hivi kilometa 100 vizuizi sita tunafikaje hapo? (Makofi)

Kwa hiyo, yako mambo ambayo kwa kweli tukitaka tupate faida ya hii Royal Tour inakuwa ni jukumu letu sisi sote, hasa sisi Wabunge ambao tunapita huko tukiwaona tuseme tupige kelele na Serikali iitikie ifanye kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa yako mambo kama hili nilizungumza la ripoti ya CAG ambapo imezungumzia juu ya vitalu ambavyo tayari vilishagawanywa lakini watu hawajapewa. Hiyo inaweza ikatupeleka kushtakiwa bure, tukajikuta tunalipa mamilioni kumbe tu kuna mtu mmoja ambaye baada ya mwingi kule kupigwa ameshindwa kupokea tukafunga goli. (Makofi)

Kwa hiyo, vitu kama hivyo na hata hivi vitalu bado ukiangalia ukilinganisha kwa kweli bei zake bado ni kubwa na muda ambao watu wanapewa mwaka mmoja ni mfupi sana. Ni vyema tungefikiria hata kumpa mtu miaka mitatu mpaka mitano wakati anapowekeza pale ajue anawekeza mahali ambapo kesho na kesho bado atakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia utaratibu wa kuondoka na zile trophies kwa wale wawindaji, wakati mwingine unakuwa mgumu sana tunaona hayo malalamiko katika maeneo mengi. Kwa hiyo, mimi wito wangu ni kwamba pamoja na mama kuupiga mwingi na tukapata hii boom sasa ya watalii ambayo inakuja na sekta zingine kwa sababu Royal Tour haikuzi utalii peke yake, kwenye nchi zote ambazo ilifanyika imekuza uchumi wote kwa ujumla. Sasa ni lazima tujiandae kila sekta kuhakikisha kwamba hili linalokuja tunalipokea na kuweza kufunga yale magoli ambayo yamekusudiwa, isije ikawa timu nyingine ile ya watani wako ambayo magoli kwao kidogo inakuwa shida shida na inakuwa ya kubahatisha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naunga mkono hoja sana na ninaomba tuunge mkono hoja hii, ahsante sana. (Makofi)