Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunifanya niwe wa kwanza kuchangia hoja iliyoko mbele yetu na kwa hakika inawezekana ni baraka za Mheshimiwa Shekilindi kwa namna ambavyo amekuwa ni mtu mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kutujalia uzima na afya kukutana na leo, lakini pili nichukue nafasi hii sauti yangu sio nzuri sana, lakini nitajitahidi hivyo hivyo.

Namshukuru sana Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kazi nzuri anayofanya kuliongoza Taifa letu hasa kwenye sekta hii ya utalii tunamshukuru sana kwa namna alivyojitoa kimasomaso, kuhakikisha kwamba anatangaza vivutio vyetu kupitia The Royal Tour ambayo kwa kweli sisi tunaona ina maana kubwa sana kama nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, The Royal Tour imeenda kuzinduliwa katika sehemu ambayo watu hawavijui vivutio vyetu, imeenda kuzinduliwa katika nchi za Ulaya. Nina amini kabisa wale ambao walishiriki na kuona vivutio vile leo tunaanza kuona matokeo yake. (Makofi)

Kwa hiyo, yule ambaye anaenda kupinga au ku-criticize suala la Royal Tour huyo ajui mambo ya utalii tumuache. Kuna nchi zimefanya kazi kubwa ya kufanya promotion ya vivutio vyao, sisi tumefanya kwa kiasi, lakini mkuu wa nchi alivyoingia na kufanya jambo hili limetupa heshima kubwa sana duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ile filamu kila mtu akiangalia anajua kabisa anatoka Ulaya anakwenda kuona Serengeti, anakwenda kuona Mlima Kilimanjaro, anaenda kuona vivutio mbalimbali ambavyo ni vya kipekee katika nchi yetu. Kwa hiyo, sisi Watanzania tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, Wizara kazi aliyoifanya Mheshimiwa Rais muendelee kui-brand vizuri, tusiibeze na tusiiache kazi hii ni kubwa ina heshima kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiongozi wa nchi kuacha kazi zake na kuingia kufanya kazi ya sekta ni jambo kubwa na la kupigiwa mfano. Kwa hiyo mimi nilitaka nianze na hili kumpongeza sana na kuhakikisha kwamba tunafanya hivyo, matokeo tumeanza kuyaona, tumeanza kuona watu wengi wanaanza kuingia nchini kwetu kwa ajili ya kuja kuanza kuangalia vivutio vyetu, hilo nataka nisema kama la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Waziri Pindi Chana...

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba huu muda tunaongea mchezaji aliyekuwa wa Manchester United ambaye sasa hivi anacheza PSG ya Ufaransa Ander Herrera yuko Serengeti na matokeo ni Royal Tour. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya, Mheshimiwa Mtaturu.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea kwa heshima kabisa hayo ndio matokeo ya Royal Tour ambayo tumeifanya, sasa katika hili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri dada yangu Pindi Chana kwa kupewa heshima kubwa ya kuongoza sekta hii. Tunakujua wewe ni mtu ambaye unajua namna ya kufanya kazi hii nzuri ya kuweza kwenye eneo la diplomasia ulifanya vizuri, lakini eneo hili ninaamini utafanya vizuri zaidi ukisaidiana na mwenzako Naibu Waziri dada yangu Mary Masanja pamoja na Katibu Mkuu na wote katika wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kabisa tutaendelea kuwapa support kuhakikisha kwamba lengo la nchi yetu kufikisha watalii milioni tano kufika mwaka huu wa fedha tunapoenda kwa sababu ilani yetu ya uchaguzi imeeleza wazi kwamba lengo letu tufikishe watalii milioni tano, hatuwezi kufikisha milioni tano bila kutangaza vivutio ambavyo tunavyo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nilitaka nishauri mambo machache ya kuweza kuongeza chachu katika eneo hili. La kwanza kumekuwa kweli kuna tozo mbalimbali zinatozwa, kumekuwa na kelele huko nyuma kwamba watoa huduma ambao ni wenzetu ambao walikuwa wanafanya kazi hii wamekuwa wakilalamikia baadhi ya tozo, niipongeze sana Serikali kuna baadhi ya tozo zimeondolewa, leo hii kuna baadhi ya watoa huduma wameanza kufaidika na kazi hiyo nzuri ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado tunawaomba mkae na watoa huduma hawa ambao wanafanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha inaleta na kusimamia na kuwaleta watalii. Lakini eneo hili wanaomba sana mtawanyiko wa maofisi ya kwenda kulipa tozo walipe TARA, waende halmashauri waende wapi imekuwa ikiwapotezea muda wanaomba wawe na dirisha moja la kuweza kulipa tozo zote wasipoteze muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tozo zinaweza karibia 50 ukasema siku tatu/nne unashughulikia tu kulipa mgeni mmoja inapoteza muda na itatuchelewesha sana kufikia lengo la kupata watalii wengi. (Makofi)

Lakini la pili ni suala la VAT; VAT kweli hamna anayekataa kulipa lakini kumekuwa na tatizo la kulipa VAT on deposit, anapolipa mgeni kule nje analipa moja kwa moja kwa yule mtoa huduma, mtoa huduma yule anakuwa anakatwa palepale VAT, ikitokea huyu mtalii ame-cancel safari yake ile VAT analipa huyu mwenzetu wa Tanzania, maana yake ni kwamba anaingia hasara na inatia hasara kampuni yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana hizi fedha zilipwe pale kwenye deposit, lakini waje kwenye maeneo ya tozo mbalimbali hiyo itakuwa umemtendea haki huyu mtoa huduma, lakini pia itakuwa ni halisia, unaweza kujikuuta unalipisha VAT mara mbili, mara tatu kitu wanachofanya destination ya Tanzania inakuwa ghali kuliko eneo lolote. Hii nayo itakuwa kikwazo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hatupati watalii wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu ni suala la viza wamekuwa wakilalamika kwamba viza yetu wanapolipia online kumekuwa na ucheleweshaji iko slow sana yuko kule anataka alipie viza ili apate ruhusa ya kukata tiketi anashindwa. Kwa hiyo matokeo yake ana-cancel safari anashindwa na ameamua kutafuta eneo lingine, hili nalo ni kikwazo kingine naomba mkalifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la wanyama hawa wavamizi kama tembo, mimi naomba nitoe pole sana kwa wananchi wangu wa Ikungi, Singida Mashariki kwenye Kijjiji cha Ntewa pale Ntuntu, juzi mtoto wa miaka miwili na nusu alikanyagwa na tembo. Eneo la Ikungi ni mbali sana na hifadhi leo hii tunaongea habari ya Ikungi sasa tunaanza kuwa na uvamizi wa tembo, lakini mnatuambia tembo wako karibu 60,000 mnasema ni tembo wachache, je, wakifika laki moja, mbili hawa tembo itakuwaje nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima wenzetu wataalam wa Wizara hii wakae wasiwe wanatuletea story iliyozoeleka ya corridor/mapito ya tembo ya miaka, leo hii watu wengi wanaumia wanakufa mali zao zinaharibiwa kwa sababu tu tembo wanazunguka kila mahali. Inawezekana kuna mazao wanahitaji kula majani fulani, inawezekana maji hakuna maeneo ya hifadhi, basi wataalam wetu watumike kupanda hata miti au mazao yanayohitajika ndani ya hifadhi ili tembo wasitoke kuja mtaani.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama haitoshi kama maji ni machache kule kwenye hifadhi, wachimbe mabwawa ya kutosha hiyo ndio maana ya kusema kuwepo kwa professional tuna wataalam wengi katika Wizara hii, tunawaamini, hebu nendeni mkakae mnapofanya utafiti fanyeni na eneo hili tusibaki kupeana story kwamba ohh haya ni mapito ya tembo miaka yote inapita, najiuliza kule Ntuntu mapito ni lini walikuwa wanaenda wapi hawa tembo, tembo wamekaa wiki nzima/wiki mbili wanafanya wananchi washindwe kufanya shughuli zao za kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutajikuta kwamba tunawahamasisha wananchi wafanye kazi, lakini hawezi kufanya kazi kwa sababu kuna tatizo la tembo wanazunguka nani hatari kwa maisha ya wananchi. (Makofi)

Kwa hiyo, nilitaka niombe sana anapokuja waziri hapa atueleze mkakati ni upi wa kitaalam, sio hoja hii ya kila siku imekuwa kama msamiati ambao haueleweki haya ni mapito, sijui ni corridor, sijui lugha zingine zinawasumbua wananchi hawajui.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana kazi nzuri mnayoifanya lakini eneo hili linatutia doa kama Taifa twendeni tukafanye kazi kwa pamoja. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)