Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza awali ya yote nami naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya, lakini nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima kwa kazi kubwa aliyoifanya pamoja na Naibu wake shemeji yangu hapa Mheshimiwa Mwanaidi Khamisi, kwa kweli Wizara hii wanaitendea haki.

Mheshimiwa Spika, yangu mimi ni machache tu; kwanza kifupi tu kabla sijakuja katika hoja ya ufafanuzi naomba Wabunge tuungane kwa pamoja wa pande zote, wanaume na wanawake, katika kuisaidia hii Wizara kwa sababu naona kuna mambo ya msingi mengi sana na yanataka ushirikiano wa kila mmoja wetu, sio kazi ya Wizara peke yake. Ni jambo la kila mmoja, aidha mwanamke ama mwanaume, kuisaidia jamii yetu kwa hiyo, tunakazi kubwa sana kuisaidia nchi yetu na dada yangu Mheshimiwa Gwajima naomba nikwambie, sisi wote tutakupa ushirikiano na timu yako ilimradi kazi ya wananchi iweze kufikiwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, niltaka nitoe ufafanuzi wa jambo moja tu hapa, kaka yangu Mheshimiwa Profesa Shukrani hapa alizungumza suala zima la kelele na mitetemo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli, jambo hili limeleta kero maeneo mengi na tumezungumza athari zake mwaka jana tulipokutana takribani Mawaziri tusiopungua nane. Leo hii kuna watu wengine ambao wana magonjwa ya pressure wanapoteza maisha kwa ajili ya kelele za muziki katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya taarifa za kiafya zinasema kuna watoto wengine wanakuwa viziwi kabisa, hawawezi kusikia kwa ajili ya kelele, lakini kwa bahati mbaya nyingine kuna watu wengine wametafuta ujauzito kwa nguvu kubwa sana, lakini mwisho wa siku ujauzito unapotea kwa ajili ya kelele na mitetemo. Bahati mbaya sana jambo hili tumelipigia kelele wakati wote na hata ninyi wengine mnafahamu, wote humu ni watu wazima, hata watu wengine network hazifanyi kazi vizuri kwa ajili ya kelele na mitetemo, tulilizungumza hili wazi tukasema hivi ilimradi watu waelewe nini madhara ya kelele na mitetemo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaamini watu kwa ujumla ni kwamba tutaungana pamoja. Kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, Sura Namba 191 ambapo kifungu cha 230(2) na Kanuni zake za Januari, 2015, tumetoa maelekezo jinsi gani jambo hili sasa tuweze kulirekebisha.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2020 takwimu zinaonesha kwamba taarifa ziliripotiwa za maeneo sumbufu zaidi ni 840. Mwaka 2021 tulikuwa na taarifa rasmi 450 na mwaka huu toka mwezi Julai, 2021 mpaka leo hii tumekuwa na taarifa 156; kwa hiyo, trend inaonesha kidogo angalao kidogo sasa watu wameanza kufanya compliance ya sheria, lakini hata hivyo bado changamoto ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie forum hii kumuelekeza mkurugenzi wetu wa NEMC na timu yake kanda zote waendelee kuchukua hatua. Hatua hizi ziko za aina mbili; kwanza, tumetoa melekezo kwamba taasisi yetu iendelee kutoa elimu jinsi gani madhara ya kelele na mitetemo ambavyo yanaweza yakaleta athari kubwa sana katika jamii yetu, hili ni moja.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili, natoa maelekezo hapa tena kwa mara nyingine kwamba taasisi yetu sasa ifuatilie maeneo yote yaliyokuwa sumbufu hasa majengo ya starehe. Tumewaambia watu kwamba hata ukiwa na nyumba ya starehe unapaswa kuhakikisha unaweka sound proof. Kwa hiyo, Mkurugenzi wa NEMC, Dkt. Gwamaka hakikisha maeneo yote yenye baa zote ambazo ni open bars zinapiga muziki funga na chukua hatua, sheria lazima ichukue mkondo wake, lazima tuliokoe Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tulikaa na viongozi wa dini tukiwaomba kwamba kupitia taasisi zote za jumuiya za kidini, sasa kuna bahati mbaya sana baadhi ya taasisi chache za dini zimekuwa zikiwa zinaleta usumbufu wa hali ya juu zaidi. Katika hili tumeelekeza wenzetu viongozi wa dini kupitia jumuiya zote hizi sasa wahakikishe na waendelee kutoa maelekezo kwa sababu, tuna imani taasisi za dini ndio zingekuwa za kwanza kurekebisha katika maisha ya watu.

Mheshimiwa Spika, imani yetu kubwa kwa sababu, tumeamua kusimamia sheria, nikuhakikishie kama maoni ya wajumbe wote waliozungumza, tutaendelea kusimamia sheria na sasahivi tunaona trend inapungua. Imani yetu tutafika mahali pazuri, niwaombe Watanzania tutekeleze Sheria ya Mazingira ya mwaka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)