Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Edward Olelekaita Kisau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya kwa wizara hii, tumeona bajeti imeongezeka; nimpongeze pia Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu nzima ya wizara hii kwa kazi wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka uliopita wafugaji walipata taabu kubwa sana kutokana na ukame; na Mheshimiwa Naibu Waziri alinitembelea tarehe 14 Januari, 2022 kuona athari za ukame kwenye Jimbo la Kiteto. Tulipata hasara karibu ya ng’ombe 25,000 kwa sababu ya ukame. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifika na aliona athari ambazo zimeletwa na ukame na nakushukuru kwa majosho Matano kwa vijiji vya Makame, Mwitikila, Lolela, Ngabolo na Katikati. Lakini kwa kuwa Kiteto ni Wilaya kubwa yenye mifugo wengi sana bado tuna upungufu wa majosho na tulitegemea bajeti hii mtatuongezea majosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukame wa mwaka jana umetokana na kukosekana kwa mvua na malisho. Kwa hiyo, tunategemea wizara hii, kipindi hiki mje mlete bajeti ambayo inaleta solution kwa ajili ya mabwawa. Na mnafahamu nimeandika barua katika kuomba mabwawa. Natamani baadaye wakati mnahitimisha bajeti yenu mtupe majibu kwa sababu wafugaji hawa wanataka kusikia majibu yenu. Kwa kuwa tayari kuna dalili kwamba mwaka huu pia ni kama kidogo hivi; natarajia kabisa wizara ituambie baadaye mmejipangaje sasa ili madhara haya ambayo yanatokana na ukame isirudi kwa namna ambayo imefanyika mwaka jana, kwa kuandaa wafugaji na kuandaa maeneo kama ambavyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Hereni ambalo limeendelea sasa. Ushauri wangu, elimu haipo sana ya kutosha kuhusu suala hili Mheshimiwa Waziri; tunawaombeni sana mtoe elimu kwa wafugaji wafahamu logic ya hii Hereni nini na pia tunaweza kusikia kelele kwamba bei hii ni kubwa kidogo kwa hiyo muangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri ulifika Kiteto na ulitoa ahadi ya vitambaa vile vya magonjwa haya ya Ndorombo, tunatarajia baadaye wakati unahitimisha kwenye bajeti yako wananchi wa Kiteto wasikie majibu, tukipata vitambaa hivi tukaweka kwenye maeneo ya malisho itasaidia kupungu magonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wizara hii inaangalia mifugo, siku hizi tumepata janga kubwa sana mahusiano siyo mazuri sana kati ya Wanyamapori, Hifadhi zetu na Wafugaji. Tunataka wizara kwa kuwa tulishazungumza hapa concept of one Government Wizara ya Maliasili na Utalii na Mifugo mzungumze ili kuondoa matatizo hayo kwa wafugaji.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango mzuri.

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru; naunga mkono hoja.