Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia katika Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi. Kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa nia njema ya kutaka maendeleo katika ufugaji, uvuvi na maendeleo kwa ujumla katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya pekee nimpongeze sana Waziri, Mheshimiwa Mashimba Ndaki; Naibu Waziri, Mheshimiwa Abdallah Ulega kwa kazi nzuri mnayoifanya kwa kushirikiana na Katibu Mkuu, Tixon Nzunda, Naibu Katibu Mkuu; Wakurugenzi wote wa Wizara; watumishi wote wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi zake, mahsusi pia na watumishi wote wa Halmashauri 184 ambao wanasimamia eneo hili la Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais kupitia wizara yetu hii kwa Wilaya ya Misenyi kututengea milioni 350 kujenga mnada wa mpakani boarder market na sasa hivi mnada huo unajengwa kwetu ni faraja kwa sababu utainua uchumi wa wana Misenyi uchumi wa wana Kagera lakini pia na soko la mifugo ndani ya Mkoa wa Kagera litakuwa limepatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kidogo kuhusiana na mazingira ya upangishaji katika Ranchi zetu za Taifa kupitia NARCO, kwanza kwa nafasi ya pekee nimpongeze Meneja wa NARCO Profesa Peter Msofe pamoja na watumishi wote wa NARCO kuanzia ngazi ya Taifa lakini mpaka ya ranch wanaposimamia katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera ni mkoa ambao una Ranchi nyingi kuliko mikoa mingine yote nchini Tanzania, tunazo Ranchi sita tunayo Kagoma, Kitengule, Kikukura, Mabale, Mwisa na Misenyi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia wingi wa Ranchi hizi maana yake idadi ya mifugo ambayo iliyoko Tanzania mingi imekuwa based katika Mkoa wa Kagera. Lakini cha kushangaza Mkoa wa Kagera ni mojawapo mkoa maskini kuliko mikoa yote Tanzania kwa taarifa za GDP ambazo zimetolewa na sababu zake ni nini ambazo zimetolewa na sababu yake ni nini kama alivyosema kaka yangu Mheshimiwa Mwijage ufugaji unaoendelea ndani ya ranchi zetu ni uchungaji na sio ufugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ambayo sio malengo mahususi ya Serikali tukijiringanisha na nchi jirani Uganda sisi tunafanya kazi kwa ushirikiano na wenzetu wa Uganda, tunatembeleana kuangalia anachofanya mwezetu wa Uganda na wanachofanya watanzania, katika nchi ya Uganda hatuongelei ukubwa wa eneo hatuongelei uwingi wa idada ya mifugo tunaangalia productivity katika eneo ulilonalo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaangalia mfugaji ndani ya nchi ya Uganda anazo heka 400 tu mle ndani ana ng’ombe 150 productivity inayotoka katika eneo hilo ni kubwa kuliko mfungaji wa Tanzania ambaye ana hekta 6000 ana ng’ombe 1000, wapi tunakwama?

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwapenda wafugaji wetu, kupitia NARCO wamekodisha kwa utaratibu mzuri wanaandika business plan lakini kuna mambo ambayo kama Taifa kama Serikali tunahitaji kuyasimamia ili hawa wafugaji sasa ndani ya Ranch zetu wawe wafugaji kweli na sio wachungaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwanza, zipo changamoto mbalimbali katika eneo hili ambazo ziko silent kwa Serikali yetu au kama inazifanyia kazi basi si kwa kiwango kile ambacho kingeweza kuwasaidia wafugaji wetu wakapiga hatua kubwa. Suala la kwanza tunalo suala la wizi katika ranchi zetu wizi ni mkubwa sana na wizi asilimia 90 mifugo inaibiwa kwenda nchi za jirani kama mnavyojua Mkoa wa Kagera tumepakana na nchi zote lakini n’gombe wanaibiwa lakini Wakuu wetu wa Wilaya zinazozunguka mahali pale wanajitahidi kadri wanavyoweza lakini wamewezeshwa kiasi gani na wizara yetu kuhakikisha sasa wanalinda mifugo yetu wanalinda wananchi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya tunaielewa lakini hakuna sehemu ambayo toka inatoka wizarani kupeleka katika wilaya zetu ili vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viweze kufanya kazi kwa ufasaha, nitafika sehemu ambayo nitashauri hizo fedha zitoke wapi kwenda katika kusaidia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili wananchi waendelee kufuga.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie miundombini mfugaji anatakiwa kuwekwa bwawa anatakiwa kuweka josho ni mfugaji gani wa Tanzania ataweza kununua excavator ang’oe miti yote katika hekta zake alizopewa achimbe mabwawa sasa Serikali inatakiwa kuja na utaratibu ambao inaweza kuwatafutia mikopo kwa kuwapa vifaa, lakini naweza kutafuta vifaa vya Serikali tumeona Wizara ya Ardhi, walinunua vifaa vya kupima Tanzania nzima, ukitaka kupima halmashauri unaenda pale Wizara ya Ardhi wanakupa vifaa unapima halafu unarudisha sasa na Serikali hapa kupitia Wizara ya Mifugo walitakiwa wawe na vifaa kama ni ma-excavator wanayo watu wakitaka kuchimba mabwawa wapewe wachimbe mabwawa halafu watakataka katika hela zinazotokana na uuzaji wa mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili halipo inakuwa ni ngumu sana kuelewa ni wakati gani anaweza kufanikiwa. Lakini zipo changamoto za mbegu, dawa za kuongeshea mifugo, chanjo zote hizo ningeomba Serikali ije na majibu ya kuhakikisha kwamba inakuwa na mkakati madhubuti kwamba wananchi wetu basi wanapewa ruzuku au inaweka utaratibu mzuri waweze kufanikiwa katika hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushauri eneo lingine ni upimaji mpya ambao ulifanyika ndani ya vitalu unajua wakati wa upimaji mpya kuna maeneo mengine Serikali ilisaidia sana kutatua migogoro. Nimwambie Mheshimiwa Waziri kuna maeneo mengine ambapo tumeleta mgogoro zaidi tumechukuwa maeneo ya vijiji yakaingia kwenye Ranch za Taifa, tuangalie kwa mfano ukienda kule kwangu nenda Kijiji cha Bunga utaona vitongoji cha Rwambogo na Shantabwa vyote vimeingia katika Ranch ambapo awali haikuwa hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nenda pale Kakuyu uangalie Kitongoji cha Katangiliza chote kimingia kwenye Ranch ninacho kitalu namba kumi Mheshimiwa Waziri unakijua kiko na kesi lakini kesi ikiisha wananchi wameshaomba hekta 2000 wapeni walime mifugo na wananchi vyote vinategemeana tusipende sana mifugo tukaacha wananchi wakilima na mifugo yenyewe basi inakuwa ni rahisi kuweza kutumia kwa hiyo, niombe kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la uvamizi wa tembo mimi naomba mshirikiane na Wizara yetu ya maliasili na utalii kwa mfano kwenye Ranch za Misenyi na mabahi ni nusu na nusu na ng’ombe. Kwa hiyo, niwaombe sana, kila siku napigiwa simu za kuhakikisha kwamba tunaenda kufukuza hao tembo, Mkurugenzi wangu hana resource za kutosha bunduki sijui tunazo mbili risasi lakini Wizara ya Mifugo ni lini mmetuchangia angalau risasi au bunduki kule hamna naomba tu hiyo inawezekana na wizara inakusanya fedha nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kidogo kwenye tangazo la GN namba 35 la mwaka 2018 kupitia tozo za minada tunayo minada ya aina tatu tunao mnada wa awali primary market tunao secondary market wa pili tunao na boda. Niombe wizara hii iangalie vizuri eneo hili Wizara ya Mifugo katika ng’ombe mmoja kwa mfano nikiongelea mnada wa boda inachukuwa kibali cha kusafirisha ng’ombe kwenda nchi ya jirani shilingi 25,000 inachukuwa tozo ya ushuru shilingi 4,000 halmashauri inaambulia shilingi 1,000; buku tu Wizara inachukuwa shilingi 29,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ardhi ile iliyoko pale yote ni halmashauri watumishi hata kama wote ni watanzania ni wa wizara wote wako chini ya Mkurugenzi resource anazotumia kwenda kusimamia pale ni za halmashauri elfu moja Mheshimiwa Waziri kitu cha kwanza naomba ukiangalie hicho gawana mapato yale angalau ile elfu nne ya tozo mnaweza mkaigawa katika halmashauri ikachukuwa elfu tatu nyie mkabaki na 2,000 na kibali cha kusafirisha unakuta wewe unachukuwa 27,000 halmashauri inachukuwa elfu tatu itasaidia na hiyo mnaweza mkaitolea maelekezo kamati ya ulinzi na usalama inapata fedha za kwenda kufanya dolia lakini pia majosho yanajengwa kupitia halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe hilo wana Misenyi walinituma kwa dhati niwashukuru kwamba leo mmetuanzishia mnada wa boarder market lakini niombe sasa Serikali kupitia wizara yetu hii mje na majibu kwa wana Misenyi kwamba tunaingia MoU uendeshaji.

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Kyombo kengele ya pili.

MHE. FLORENT L. KYOMBO Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi hii, naomba kuunga mkono hoja; ahsante sana. (Makofi)