Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Asya Mwadini Mohammed

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuweza kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii muhimu ya Wizara ya Uvuvi kwa maslahi mapana ya Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitoe pongezi zangu za kipekee kwa Rais wa Zanzibar Daktari Hussein Mwinyi kwa kuja na sera ya uchumi wa bluu. Ukisoma randama ya Uvuvi bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa uvuvi wa bahari kuu ilitengewa bilioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya uvuvi lakini kwa masikitiko makubwa mpaka Aprili mwaka huu hawakupewa chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii imeendelea tena kurejea yaleyale mambo wame-copy na ku-paste wameomba tena kwa Mwaka 2022/2023 bajeti hii ambayo leo tunaijadili wameomba tena Bilioni 50 kwa ajili wa ujenzi wa bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna ambaye hahitaji kuona maendeleo ya Taifa hili na tupo hapa kwa ajili ya kuitumikia Taifa letu, Mheshimiwa Waziri alipokuja kutoa hutuba yake alizungumza mambo mazuri sana na ukweli yakitekelezeka Tanzania itakuwa imepiga hatua kwenye Sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu. (Makofi

Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza wanao mpango madhubuti kwenye hotuba yake kwamba wataweza kutoa vibali vya leseni vipatavyo 21 kwa meli za nje na za ndani kwa wawekezaji ambao watawekeza kwenye Bahari Kuu. (Makofi

Mheshimiwa Naibu Spika, kama leo tunajielekeza kutoa leseni, yaani tunatoa leseni ili tuweze kuingiza vyombo nchini lakini parking ya vyombo hatuna, hili ni jambo la kusikitisha ni sawasawa na kutoka kwenda Mjini kununua furniture lakini huna nyumba ya kuviweka, maana yake hivyo vyombo utaishi navyo barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali kama tumeamua na tumejidhatiti kweli tunahitaji kwenda kwenye uvuvi wa Bahari Kuu ni lazima sasa tutumie nguvu za ziada ili Wizara hii iwezeshwe wapewe fedha haiwezekani vipindi viwili vya bajeti watu wanaomba kujenga bandari kitu ambacho ni maslahi ya mapana ya Taifa, kitu ambacho kitaingiza mapato kwenye Taifa hili halafu wanachinjiwa baharini hawapewi chochote, haiwezekani! Ukweli kwenye suala hili nitarudi kulishikia Shilingi Mheshimiwa Waziri alete-commitment hapa anawapa fedha kujenga bandari ama hatawapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma taarifa ya ZAFICO kwa sababu tukizungumza wavuvi wa Bahari Kuu ni sehemu ya Muungano. Kwa hiyo, kuna mashirika mawili ambayo yana-practice uvuvi wa bahari kuu ambao ni ZAFICO na TAFICO kwa Tanzania Bara, ZAFICO lipo kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia kuna changamoto mbalimbali ambazo ZAFICO wamezi-mention kwenye taarifa yao, kwanza wamezungumza issue ya leseni, wamezungumza issue ya leseni kwamba, kuna leseni ambazo zitatolewa kwa kipindi cha miezi Sita ambapo meli ziwe zina urefu wa mita 24 na leseni hizo wanasema kwa wawekezaji wazawa residential watalipa Dola 4,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo na mkakati wa kwenda Bahari Kuu ni kuwanusuru wavuvi wetu wadogo ambao wanavua uvuvi ambao hauna tija wanapotea hovyo, wanapoteza mali zao na maboti yanazama na wanapoteza maisha yao, ndiyo maana tunataka ku-move kutoka kwenye huu uvuvi mdogomdogo watu ambao hawaeleweki waende kwenye uvuvi wa Bahari Kuu. Sasa huyu mwekezaji mdogo mvuvi mlalahoi anayetoka kwenye mazingira magumu kama aliyetoka Asya, kwamba leo unamwambia leseni kwa muda wa miezi Sita akalipe Dola 4,000 ambayo sawa na pesa ya Kitanzania 9,268,000.00. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza anakwenda baharini hakuna utaratibu maalum ambao umeandaliwa ndani ya bahari maana yake hakuna GPS ambazo zinasoma hapa kuna samaki au hapa hakuna. Kwa hiyo, anakwenda yaallah Insha’Allah maana yake anamuomba tu Mwenyezi Mungu nikipata hewala nisipopata mashallah, kwa hiyo, anakwenda tu moja kwa moja lakini atakapofika kule baharini pili akifika baharini muda ambao atautumia hawezi kuvua kwa siku moja akarudi wakati alipokuwa anaenda na kidau, leo atakaa pengine muda wa wiki moja ama zaidi ya wiki moja anasubiri kutafuta samaki ili aweze kurudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nje tu na hiyo gharama ya leseni maana yake wiki nzima anavyoingia baharini kutafuta hao samaki kuna gharama za mafuta ambazo meli inapaswa ikae itulie na isizimwe hata kwa muda wa dakika moja ndani ya wiki nzima. Mafuta ambayo wanayatumia hawa ndugu zangu wavuvi wawekezaji hawa ambao wanakwenda Bahari Kuu kwa chombo chenye urefu wa mita 24 maana yake mafuta hayatapungua kuanzia lita 9,000 na kuendelea, tena hapo watakaa kwa muda wa wiki moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mafuta mtu anayejaza, masikitiko mengine ni kwamba mtu anayejaza mafuta mwenye Prado yake nje anauziwa lita 3,000 lakini na mwenye meli ambaye anakwenda kufanya kazi anauziwa naye lita ile 3,000, hii siyo sawa! Kama kweli tunao mpango wa kuwasaidia wavuvi wetu, maana yake lengo la ku-move kwenda Bahari Kuu na watu wakajipige wakakope, wakafanyaje, tunahitaji kuwasaidia tujiandae hata tukafanye mazungumzo kwenye suala zima la mafuta, kuwe at least kuna ahueni wa tofauti ya mtu ambaye anayejaza gari kipande cha kawaida na huyu ambaye anaenda kufanya hii kazi kwa wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna gharama ambayo hiyo lita 9,000 wanayosema mafuta haya ili akae wiki nzima aweze kufanya kazi, ana uwezo maana yake lita 9,000 ukizidisha na 3,000 ya lita ya mafuta anaweza akatumia milioni 27 kwa wiki. Sasa milioni 27 hiyo jiulize kwa chombo chake cha mita 24 ndani ya wiki moja anao uwezo kweli wakupata samaki zaidi ya milioni 27. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali kwa namna bora, kwanza kabisa wakatengeneze bei za mafuta za kuwasaidia wavuvi wetu ambazo ziwe tofauti na za magari. Pili, kiwango cha kodi ambayo ni leseni ambayo nimeshaizungumza nayo kwa wazawa kama kweli tunahitaji kuwasaidia nayo ikapunguzwe. Kwasababu ukitoa hivi vitu vya mafuta maana yake kuna gharama nyingine za uendeshaji, wafanyakazi lazima awepo ndani ya wiki anunue chakula, lazima awe na chambo ambacho nacho ni changamoto nyingine. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi mengine nitayaandika kwa maandishi. (Makofi)