Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo. Nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii, kuna mtu mmoja ananiambia nisimame, nimesimama. Kama hawanioni nina mpango wa kununua vile viatu vinavyoitwa raizoni ili niwe navivaa wawe wananiona vizuri. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayoifanya, pia kwa kuwasilisha hotuba yao hapa Bungeni. Nchi yetu kijiografia imejaliwa katika maeneo mbalimbali ya kuzalisha kiuchumi. Kuna maeneo ya uvuvi ambayo katika Maziwa yetu Makuu wananchi wetu wanategemea uvuvi. Kuna maeneo ya bahari wanaoishi katika Visiwa vya Bahari na pembezoni mwa bahari wanategemea uvuvi. Leo hii tuna maeneo pia ya Mikoa ambayo yanategemea mifugo, Mikoa ya Kaskazini na Katikati hapa. Kuna Mikoa pia inategemea kilimo, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa na Mwenyezi Mungu kutupa jiografia ya namna hii ni kwamba ili tuweze kuzalisha chakula, tuweze kufuga, tuweze kuvua pia na Samaki, sasa katika eneo letu la Mkoa wetu wa Ruvuma na hususan Wilaya ya Namtumbo ni wakulima. Tunategemea sana kilimo ndiyo kipato chetu cha uchumi wa wananchi wetu, sasa katika miaka hii ya karibuni, miaka miwili ya karibuni hapa kumetokea na mfumuko wa mifugo kuja katika Wilaya yetu ya Namtumbo, pia kumekuwa na Mikoa ambayo inatoa vibali vya kusafirisha mifugo hiyo itoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanatoa vibali vinavyosema ameruhusiwa aende bila ya kushirikisha mamlaka za Mikoa ambayo mifugo hiyo inakwenda kama wana mipango gani ya ardhi katika eneo lao la Mikoa hiyo. Sasa Mikoa ile inayokwenda mifugo hii, Serikali au Mamlaka ya Mikoa ikiwakamata wanaonesha vile vibali na wanasema kwamba, Katiba inaturuhusu, binadamu yeyote raia wa Tanzania unaweza kuishi mahali popote pale, lakini wanashindwa kusema kwamba, bila kuvunja sheria, sasa wanapozuiliwa wanasema wanaonesha vile vibali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, kuwe na utaratibu mzuri wa mawasiliano ya ng’ombe au mifugo inakotoka kule wanaoomba kibali na mamlaka ya Mkoa ule iwasiliane na mamlaka ambayo yule mfugaji anataka kuhamishia ng’ombe wake kule ili waweze kuelewana, nafasi ipo au hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika Wilaya yangu ya Namtumbo wamejaa ng’ombe wengi sana. Sisi ni wakulima, mwaka jana tu 2021, tumezalisha zaidi ya tani 157,000 ya mazao ya nafaka, ni mazao ambayo yanategemewa katika Taifa hili, lakini sasa kumekuwa na taharuki mwaka huu wa ng’ombe kulisha katika mazao hayo. Mkulima anaandaa shamba, analima anatafuta mbegu dukani, anapanda, anapalilia; anaenda kununua mbegu ambayo mwaka huu imezidi zaidi ya Shilingi 100,000/= anatia shambani, mahindi yanatoka ya kijani, mtu analeta ng’ombe analisha kwa dakika 20 au usiku mzima. Kwa hiyo, hii inaleta tafarani kati yetu sisi wakulima tusiozoea kuwa na mifugo, tuliozoea kuzalisha chakula kwa ajili ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana, Serikali itambue kwamba sisi ni wakulima, lazima mje mtutambue kwa sababu hamjatambua kuna mifugo kiasi gani, kuna mifugo mingi sana kule Wizara haijafika kutambua shida hii ya mifugo kule. Kuna vuguvugu la magongano haya kati ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu mifugo ina thamani, lakini chakula pia kina thamani. Sasa unapohamisha mifugo kutoka eneo moja; kutoa tatizo mahali na kupeleka eneo lingine, ni sawasawa na kidonda, unakitoa mguuni, unakihamishia tumboni, kitakuua tu. Kidonda lazima ukitibie. Kwa hiyo, lazima tutafute utaratibu wa kutibu hili tatizo kuliko kukihamisha kidonda mguuni ukakiweka tumboni, kitakuua tu. Sasa Serikali au mamlaka ya mkoa fulani inapotuhamishia sisi tatizo, kama wao wana ugomvi kati ya wakulima na wafugaji, wanatuhamishia sisi ambao tulikuwa hatuyaelewi hayo, sasa wanatuhamishia tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Wizara ya TAMISEMI na Ardhi washirikiane waone jinsi gani ya kuwagawia maeneo wafugaji wasije wakaingiliana na wakulima ili sisi tuendelee kuzalisha chakula, tuendelee kupata maslahi yetu na kuendelea kuweka usalama wa chakula katika nchi yetu. Sisi sasa ndiyo watunga Sheria katika Bunge hili. Ni wakati sahihi sasa wa kuweka utaratibu na mkakati endelevu utakaowezesha wafugaji na wakulima kufanya shughuli zao bila migongano yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo letu pia wafugaji wanaingia katika hifadhi. Kule tuna Hifadhi za Jamii na Jifadhi ya Taifa. Hifadhi ya Jamii WMAs zile tuliziweka kwa ajili ya kuhifadhi, kwa maana nyingine sisi ni wakulima na wahifadhi. Katika maeneo yale ya uhifadhi wa WMA, wakulima tulikuwa tunawazuia kabisa wasiingie kule, wakiingia wanapata adhabu kali sana. Sasa wafugaji ndio wameingia huko. Wakulima wanauliza, sisi mlikuwa mnatuzuia, wafugaji mbona wamekaa kwenye hifadhi na wanatuharibia vyanzo vya maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetengeneza miundombinu ya umwagiliaji, lakini wafugaji wanaenda kwenye vyanzo vya maji kutumia maji yale. Kwa hiyo, kazi yetu ya kilimo inakosa maji wakati wa kiangazi, tunashindwa kufanya kazi yetu. Kwa hiyo, ni jambo ambalo Serikali lazima ije Namtumbo, ije Mkoa wa Ruvuma kuangalia shida hii, ni kubwa. Tusingoje mpaka watu waanze kuuana kama Morogoro ndiyo Serikali ianze kuingia pale. Tunawaomba sana Serikali ije kuangalia tatizo hili tulionalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 13 Novemba, 2020 wakati anafungua Bunge hili la 12 Marehemu Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli alisema, Serikali itaongeza hekta kufikia milioni sita kutoka 2,788,000/= kwa ajili ya maeneo ya wafugaji, malisho na maji. Serikali mmefikia hatua gani katika hilo? Alisema mwaka 2020 tarehe 13 Novemba; Serikali ni ile ile Serikali ya Awamu na Sita, mama alipokuja alisema, “Kazi Iendelee.” Kwa hiyo, moja ya kazi inayoendelea ni hii. Nawaomba sana Wizara mhakikishe kwamba tunatenga maeneo ili wasiingiliane wakulima na wafugaji, tuishi salama. Sisi wote ni Watanzania, lakini lazima tuwa-guide hawa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara katika ukusasa wa 47 imesema, Wizara kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imetenga jumla ya hekta 128,000 kwa mwaka huu na Mkoa wa Ruvuma umetengewa hekta 1,696 basi, kati ya 128,000 na kuna ng’ombe hatari huko. Ng’ombe wote waliokuwa huko kama sehemu hizi ambazo migogoro imetulia, ndiyo ng’ombe wote wale wamekuja Namtumbo Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana mje mtuangalie. Mkoa wa Ruvuma umetengewa hekta 1,600 kwa ajili ya wakulima. Tunawaomba mwingiliano huu kati ya sekta ya maliasili, wana maeneo makubwa; ardhi, mifugo, TAMISEMI, mkae pamoja mtupangie ili hao wafugaji wapewe maeneo, wasiingiliane na wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)