Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi kuchangia kwenye Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi; awali ya yote kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri wa Mifugo na Naibu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wizara hii sote tunaijua kwa nyakati nyingi imekuwa ni wizara ambayo haipewi kipaumbele, lakini wizara muhimu sana katika nchi yetu kwa maana inachangia pakubwa katika pato la Taifa. Nimeona jitihada nyingi sana za Mheshimiwa Waziri ambazo anazifanya katika sekta ya mifugo ikiwa kwenye ujenzi wa majosho. Wilaya yangu ya Bahi tumeweza kupata majosho nane katika mwaka wa fedha 2021/2022 na huko nyuma ilikuwa ni nadra sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuja na mfumo wa kuwa na hereni za kieletroniki jambo hili limefanyika sana katika nchi ya Botswana kwamba mifugo inavyopata electronic tag tayari tunakuwa tunajua taarifa ya mfugo ule lakini unaungamanisha na maeneo mengine kwa mfano TRA wanaweza kuwa wanajua taarifa za mifugo ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasaidia sana kwa maana ya kwamba mfugaji wetu sasa anaweza kwenda kukopesheka. Maana yake ana mifugo inayotambulika na utaratibu wake akiuza inajulikana kwamba ng’ombe mwenye Serial Number hii sasa ameuzwa. Kwa hiyo, haya ni mapinduzi makubwa na Mheshimiwa Waziri kwa dhati kabisa nakupongeza kwa initiative hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuchangia katika maeneo matatu; la kwanza nianze katika suala zima la uuzaji wa nyama nje ya nchi. Nimefanya biashara hii kwa kiasi kukibwa lakini hatujawekeza vizuri katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumezuiliwa kuuza nyama yetu katika baadhi ya nchi, tumezuiliwa kwa sababu ya uchakavu wa machinjio ya Serikali, kwa sababu ya kuwa na hali mbaya ya mazingira. Hatuwezi kuuza Saudi Arabia, hatuwezi kuuza Falme za Kiarabu na maeneo mengine, lakini unavyokosa soko la Saudi Arabia ina maana umekosa fursa yote ya Middle East. Unavyokosa soko la Falme za Kiarabu ina maana umekosa kuuza Middle East yote, tatizo liko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda chetu cha machinjio cha Kizota walikuja wataalam kukagua wakakuta kina hali mbaya, lakini kwa muda mrefu na wataalamu walishafanya tathmini hata tathmini ya hivi karibuni inatakiwa Bilioni Mbili na Milioni Mia Tano tu. Sasa Shilingi Bilioni Mbili na Milioni Mia Tano imetugharimu kwa kiasi kikubwa. Nikitaka mimi kuuza mbuzi au kondoo nje ya nchi au ng’ombe natumia viwanda vya watu wengine hapa, lakini itaonekana lebo ya mwenye kiwanda kile na siyo kampuni yangu, sasa huu ni unyanyasaji. Naweza nikafanyiwa fitina muda wowote nikanyang’anywa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Serikali na Mheshimiwa Waziri jambo hili uliahidi bajeti iliyopita, sasa Bilioni Mbili na Milioni Mia Tano kweli Serikali? tumekaa miaka Sita? Eneo lile la Kizota halikarabatiwi? Kama Serikali imeshindwa nipeni basi hata mimi! Shilingi Bilioni 2.5 ni kitu ambacho kinawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali kwenye jambo hili Bilioni Mbili na Milioni Mia Tano ni kitu cha aibu kukaa muda wote huo Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, tunalazimika kwenda kuchinjia ng’ombe wetu Kenya, mbuzi tunachinjia Kenya, kondoo Kenya. Export ya Kenya inaonekena sasa ndiyo kubwa kwenye mifugo, lakini ng’ombe wanavuka Namanga wanaenda kuchinjiwa kule na tunafanyiwa udalali mkubwa haijawahi kutokea na masharti makubwa. Sasa Mheshimiwa Waziri kweli Bilioni Mbili zinatufanya tuwe hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nisiseme sana na mengine yanayotokea kwenye viwanda vyetu vya hapa ndani, lakini Mheshimiwa Waziri kwenye hili kwa kweli, tusaidie kukarabati kiwanda chetu cha Kizota.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunauza ng’ombe au nyama ya mbuzi na kondoo ikiwa ni katika hali ya kawaida ya caucus, lakini hatu-process. Tanganyika Packers tulikuwa nayo, nyama yetu hatupeleki iliyo-processed, tunapeleka kama tunavyopeleka mahindi ya kwenda tu kusaga nje. Sasa Mheshimiwa napata shida na mimi niliseme sana hili la ku-process nyama kama tu kiwanda hiki cha machinjio tu ya Bilioni 2.5 tunashindwa sasa nikianza kusema na habari kiwanda cha ku-process nitakuwa naongea kitu kikubwa. Hebu na hili nalo liangalieni sasa kwamba, tuweze kuuza mazao ya mifugo nje ya nchi badala ya kupeleka ng’ombe, nyama, ambazo wenzetu wanaenda ku-process upya kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu malisho. Wafugaji wetu ni wakimbizi ndani ya nchi yao, na tunalaumu kwamba, kwa nini wanahamahama, wanahamahama kutafuta malisho, lakini umiliki wa ardhi kwa ajili ya malisho bado haujakaa sawa. Mheshimiwa Waziri jambo hili liangalieni. Nchi ya Zimbabwe imepiga hatua kubwa sana na walipata mkopo kutoka AU kwa ajili ya kuzalisha malisho, ukienda nchi nyingi za Ulaya wenzetu wameshafika hatua hiyo ya kulima malisho, habari ya kuacha ng’ombe azurure ajitafutie chakula ni kitu cha kizamani sana. Kwa hiyo, tuanze wafugaji wetu kuwatafutia maeneo kwa ajili ya malisho, pia wamiliki ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ng’ombe wetu na wanyama wetu katika soko la dunia nyama yake ni ngumu sana. Sote tunajua ng’ombe atoke Shinyanga mpaka Katavi kwa kuhamahama kwa hiyo, tunaharibu hali ya mifugo yetu, lakini kosa kubwa ni kwamba hatufanyi uwekezaji kwenye malisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni miundombinu. Ng’ombe na mifugo mingine hawapati maji, hatuna majosho. Sasa wekeni utaratibu na kama Serikali haiwezi kwenye hili, basi tuweke utaratibu wa wafugaji wetu wawe sehemu moja waji-organize waweze kufanya utaratibu wa kujenga miundombinu. Kwa hiyo, bado tuko katika karne ya kizamani. Kuna watu wengine wanasifia kwamba ng’ombe wetu hatuwatibu sana na madawa kwa hiyo ni ng’ombe wazuri. Dunia ya wapi nani anataka kula ng’ombe wana magonjwa? Anataka kula nyama ina magonjwa? Wanasema kwamba, kuku wetu wa kienyeji ni watamu, hiyo ni wrong perception. Nani anakula kuku anaumwa, anapona mwenyewe, anajitibu mwenyewe, hiyo ni nyama gani mtu anataka kula? Kwa hiyo, kwa sisi Kanda ya Kati msitupeleke kwenye hiyo habari kwamba, kuku wa kienyeji ni wazuri, tunakula wenyewe tu, lakini nani anaenda kula kuku hajawahi kutibiwa hata siku moja halafu unakula? Hivyo, nataka niseme jambo hili, hebu tutoke na mawazo ya kiufugaji wa kizamani. Dunia inabadilika, dunia inakimbia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala zima la vyuo vyetu vya mafunzo kwa ajili ya mifugo. Vyuo vina hali mbaya havipati bajeti zake, bado vinafundisha teknolojia ya kizamani, bado wana nadharia kubwa. Ukienda maeneo yale unashangaa tangu alivyojenga Mwalimu Nyerere majengo yale hayajaongezeka. Sasa kama hatuna Training Institute, hatuna researching centers nzuri za mifugo, tutabaki kusema Tanzania ni nchi ya pili katika Afrika kwa kuwa na mifugo wengi, basi ni nyimbo, lakini ukija kwenye uhalisia hali yetu ni mbaya sana, hatujawekeza kwenye mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya Wizara hii imekuwa inapata fedha kidogo sana. Nami kwa kweli, siwezi kumlaumu hata Waziri, mwaka jana ilikuwa Shilingi Bilioni 243.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)