Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi awali ya yote kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataallah kwa kunipa afya njema na kunijaalia leo angalau na mimi nimesimama kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ambayo kimsingi ndiyo kichocheo cha uchumi wa maeneo mengi nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla sijaanza mchango wangu nichukue nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa namna masikini ya Mungu ambavyo kila kukicha anahangaika kutafuta pesa mahali pole ndani na nje ya nchi ili kuweza kunusuru shughuli za kimaendeleo na shughuli kubwa ambazo zinachochea uchumi wa nchi yetu kwa ujumla wake. Hopeful na sisi tutaendelea kumuombea Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema, aendelee kumfanya awe mvumilivu na aendelee kuchapa kazi tukiamini kabisa lengo lake na nia yake ni njema kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nitachangia maeneo matatu; la kwanza nitachangia umuhimu wa Wizara hii katika uchocheo wa uchumi wa nchini kwetu. Mimi ninavyojua Wizara hii ni kama catalyst ndio maana ukiona vipaumbele vingi ambavyo vinachochea ukuaji wa uchumi kwa maana ya bandari, barabara, vivuko na maeneo mengine yapo ndani ya Wizara hii. Kwa maana ya kwamba bila Wizara hii kufanya kazi inavyotakiwa basi ninaamini kabisa uchumi endelevu wa nchi na maeneo mengi hautafikiwa kwa wakati wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili ndilo ambalo linanifanya leo nielekee kwenye mchango wangu na natambua kabisa nje ya human resource, nje ya natural resource pamoja na political stability lazima infrastructure za nchi ili uchumi wake uweze kukua kwa haraka lazima infrastructure ziwe stable, ziwe nzuri, kuwe kuna connection kati ya Mkoa mmoja na Mkoa mwingine, kuwe kuna connection kati ya Wilaya watu waweze kuwasiliana, lakini ikibidi kuwe kuna connection kati ya nchi na nchi. Sasa hili la nchi na nchi ndiyo linanipelekea mimi kuchangia barabara yangu ya Utegi - Shirati na Kirongwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Kirongwe ni mpakani mwa Kenya na Tanzania na nimekuwa nikisema sana. Kwa bahati mbaya sana Mheshimiwa Waziri wewe ukiwa Waziri wa Maji ulipita barabara hii unaifahamu. Mwaka 2020 Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa kwenye kampeni na mimi nimshukuru sana kwa namna ambavyo alikuwa amejitoa, aliahidi barabara hii kwa maana ya kutoka Mika - Shirati mpaka Kirongwe zaidi ya kilometa 44 na kilometa 12 jumla ni kilometa 56.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama toka mwaka 2005, 2010, 2015, 2020 inataja barabara hii. Mheshimiwa Rais tarehe 5 Februari, 2022 alivyotembelea ndani ya mkoa nilivyopata ridhaa mimi na Mwenyekiti wa CCM Mkoa na viongozi wengine tulizungumzia barabara hii, unaifahamu kinaga ubaga. Sasa cha kushangaza ni kwamba na hata humu Waheshimiwa Wabunge mimi nilivyoingia mwaka 2020 nilikuwa ni mtu wa kwanza kuulizia utengenezaji wa hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wa Viti Maalum mbalimbali wamekuwa wakisimama ndani ya Bunge wanauliza barabara hii. Cha kushangaza na kinachoniumiza zaidi ni kwamba pamoja na maulizo yote hayo humu ndani bado unaendelea kutenga fedha ya ujenzi wa mita 500 peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile ina urefu wa kilometa 56 mpaka Kirongwe mpakani kwa umuhimu wake, umuhimu wa Tanzania na Kenya kila mwaka mnatenga mita 500, mita 700 maana yake mpaka tufike mpakani tunahitaji zaidi ya miaka 50 ili kutimia kule maana yake hata mimi Mheshimiwa Mbunge sitakuwepo na wengine hawatakuwepo ndiyo tunafika mpakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani watu ambao wanaandaa hizi barabara za kimkakati wawe wanaangalia umuhimu wa barabara kwenye uchumi na ukuaji wa uchumi ili wapeleke fedha badala ya kila mwaka tunarudi tunatenga fedha kwenye kurekebisha na kutindua barabara kama Mheshimiwa Mbunge aliyepita alivyotangulia kusema. Tunashindwa kuweka vipaumbele kwenye barabara mpya zinazotuunganisha kati ya nchi na nchi, mkoa na mkoa ambazo tunazijua kabisa hizi barabara zikitengenezwa zinakuza uchumi wa nchi ile lakini pia zinakuza uchumi wa wananchi hawa ambao wanazunguka maeneo hayo mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapo kesho kufanya majumuisho, kwa sababu unaifahamu barabara hii waambie wananchi wa Rorya ni lini barabara hii itajengwa. Cha ajabu zaidi ambazo mimi nimekuwa nikiumia, mwaka jana wametenga mita 700 hivi ninavyozungumza kwa bajeti ya mwaka jana 2021/2022 hakuna mkandarasi yeyote ambaye yuko site. Hata hizi mita 500, mita 700 mnazoweka hakuna mkandarasi site. Sasa leo tena umetutengea mita 500, mimi najiuliza hii accumulation ya mwaka jana na ya mwaka huu itajengwa lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama bado tunaomba kilometa 56 hazijawezekana, leo tunatengewa mita 500 na hakuna mkandarasi site, inaumiza sana. Nikuombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja kwa sababu barabara hii unaifahamu, wananchi wasikie barabara ya Mika-Shirati kwenda Kirongwe ambayo ndiyo msingi wa kuunganisha kati ya hizi nchi mbili inajengwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili siyo barabara hii peke yake, kKilichoniuma ni kwamba sisi ndiyo tunaopakana na Kenya. Ukitoka Sota ukipita zile Kata za Roche, Golibe mpaka Ikoma inapakana na Tarime Vijijini ni mpakani. Hapo ulipokaa Mheshimiwa Waziri na hapa nilipokaa, hapo ulipokaa ni Kenya hapa ni Tanzania katikati ndiyo kuna barabara. Barabara ile sikuiona ikiwekwa kwenye bajeti wala sikuiona inatengewa fedha yoyote wala sikuona inazungumzwa na ndiyo barabara inayotuunganisha sisi Wakenya na Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu ukienda upande wa pili Mheshimiwa Waziri wewe ni shahidi, kule wameanza kujenga barabara zao zinazowaunganisha kutoka Kenya kuja Tanzania, sisi hata fedha tu ya feasibility study kwenye hizi barabara hamna.

Sasa mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri vipaumbele vingi kwenye barabara hizi ziende kwenye barabara ambazo zinaweza kukuza uchumi kati ya nchi na nchi, lakini zinakuza uchumi kati ya mkoa na mkoa kwa sababu sisi bidhaa yetu watu ambao wananunua bidhaa wengi wanatoka Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea kwamba kuwe kuna miundombinu imara maana yake sisi uvuvi ambao tunavua na kwa asilimia kubwa tunachofanya shughuli yetu ya kiuchumi, tunafanya shughuli ya kilimo pamoja na mifugo, watakuja Tanzania wakiwa wanaamini kabisa miundombinu iko imara. Nikuombe sana vipaumbele hivi kama ambavyo nimeona Mkurugenzi wa Bandari anahangaika kutafuta watu wengine waweze kuvusha biashara bandari. Ningetamani watu wanaohusika na barabara pia wanapotenga bajeti zao waweze kuainisha barabara za kimkakati ambazo zinaweza kukuza uchumi wa nchi kwenye maeneo yote nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili Mheshimiwa Waziri nichangie kwenye kivuko; hiki kivuko kinachoitwa cha Musoma – Kinesi asilimia 70 ya wananchi wanaokuja Musoma wanatoka jimboni kwangu, Tarafa ya Suba, Tarafa ya Loimbo, Tarafa ya Nyanje; yaani kile kivuko kwa namna moja ama nyingine kinawahudumia sana wananchi wa Wilaya ya Rorya. Hakuna sehemu unapata mahitaji kwa sababu mji uliokuwa kwenye Wilaya ya Rorya ni Musoma na ili tuje Musoma ni lazima tuvuke kupitia kivuko hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaweza ukaona population ya watu zaidi ya 50,000 wanategemea kivuko hiki ili kupata mahitaji yao Musoma Mjini. Leo ninavyozungumza na wewe kivuko kilichopo ambacho kilikuwa kinatoa huduma hii mmekitoa kimepelekwa kwenye matengenezo. Kilichobaki ambacho mmekileta ni kidogo sana, inafika mahali Mheshimiwa Waziri kile kivuko kama hawajakwambia huwa kinabebwa na upepo wakati wa mvua, kinapotea direction. Wananchi mle wamejaa, watoto wadogo, wakina mama, magari, kinapotea direction, kinakaa ndani ya maji zaidi ya lisaa lizima mvua inanyesha, mvua ya kwao, jua linawaka la kwao mpaka hali ya hewa itakapotengemaa ndiyo wanarudi kutafuta njia ya kwenda kugoha (kuegesha) sehemu moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikuombe badala ya kusubiri mpaka yowe lilie, tupate maafa kwenye maeneo yale. Kile kivuko amacho tulikichukua zaidi ya miezi sita sasa kimekwenda kutengenezwa kirudi kwenda kutoa huduma eneo ile. Lakini kivuko hicho kikija kije tayari kikiwa kina kivuli kwa sababu kile cha mwanzo kilichokuwepo mvua ilikuwa ni ya kwao, jua lilikuwa ni la kwao. Wakati wa mvua wale wananchi masikini ya Mungu wanavuka huku wameshika roho zao. Ukiwaona wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri huwezi kuamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikuombe tusiwe tunasubiri mpaka matukio yanatokea tukirudi tunapeana pole. Hili ninalokwambia ni kama tahadhari, ninaiona kabisa kwa mazingira yale ya namna watu wanavovuka kwa shida eneo lile hebu ichukulie serious. Nimesema zaidi ya watu 50,000 wanategemea huduma kuja Musoma Mjini na wanategemea kuvuka na kivuko hiki. Wakinamama wajawazito wakati mwingine masikini ya Mungu ili waweze kuvuka complication ya kituo cha afya wanatakiwa waje Hospitali ya Mkao Musoma Mjini, wanatumia kivuko hiki, lakini hakiko stable. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ili ulione hili kwa jimbo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu nataka nichangie kuhusiana na bandari. Mheshimiwa Juliana amezungumza vizuri sana bandari ya Musoma. Tunayo bandari pale Wilaya ya Rorya, bandari ya Sota ni bandari ambayo kipindi cha nyuma ikisaidiana na bandari ya Musoma ilikuwa inakuza sana shughuli za kiuchumi kwa watu kutokea Kenya kupitia pale bandari ya Sota kuja mpaka Musoma. Leo bandari zote hizi hazifanyi kazi Mheshimiwa Waziri na bahati mbaya sana bandari ya Sota niliuliza hapa mkasema kwamba kuna fedha mtaingiza kwenye mchakato angalau iweze kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye bajeti humo haimo, bandari ya Musoma Mjini haimo. Zile bandari ndiyo ukuaji na ukuzaji wa uchumi wa Mkoa wa Mara. Leo sisi tunafanya shughuli ya uvuvi hatuna watu wa nje kuja kununua Samaki, badala yake wavuvi wanatoa samaki Musoma kupeleka Kenya kitu ambacho ni hatari sana kwa maisha yao. Tunataka mtuambie ili ukuaji wa uchumi wa Mkoa na Wilaya ya Rorya nini mnafanya katika ukuzaji wa hizi bandari ili Mkoa wa Mara uweze ku-stimulate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wengi leo Mheshimiwa Waziri wanakimbia kutoka Musoma wanahamia Mwanza. Wavuvi waliokuwa wanafanya shughuli za kiuvuvi ambao walikuwa wanategemea wanunuzi kutoka Kenya, Uganda hawapo tena ni kwa sababu ya hizi bandari zimekufa.

Nikuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu sijaziona humu ndani, niombe utakapokuja kusimama useme ni nini mpango mkakati wa hizi bandari kwenye maeneo ya Mkoa mzima wa Mara, bandari ya Mkoa wa Mara ya pale Musoma Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini utuambie nini mkakati mlionao wa Bandari ya Sota ambao iko mpakani mwa Kenya, Uganda na Tanzania. Hayo ndio mambo tunayotaka tuyaone sisi kwenye bajeti yako, lazima fedha iende kwenye maeneo ambayo yanakuza, fedha inajirudia yanakuza uchumi wa eneo husika, hutakuwa unaangaika badala ya kupeleka barabara ambayo hayana uchumi inakwenda inafika mwisho inagota imekwishia hapo, sisi tunakuambia peleka barabara maeneo ambayo wale wananchi wa maeneo yale ukuaji wa uchumi utakuwa Wakenya watakuja wengi watapitia pale badala ya kuzunguka maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waganda wale wanaohangika kupitia majini watapitia pale, yaone haya Mheshimiwa Waziri kama vipaumbele vyako kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe mimi nitasema kwamba nitaunga mkono bajeti baada ya haya yote niliyoyazungumza Mheshimiwa Waziri nitakapopata majibu sahihi kuhusiana na barabara ya Mika - Utegi, kuhusiana na bandari zile, kuhusiana na hiki kivuko ambacho kila siku ninavyoongea na wewe juzi mwananchi ananipigia Mheshimiwa Mbunge kivuko kimepotea njia, tuna saa nzima tumekaa kwenye maji tumeshika roho zetu, hatujui mvua iishe muda gani tuendelee na safari, halafu leo niangalie humu nione hakuna fedha iliyotengwa, kivuko mnasema kiko matengenezo yale asilimia 73 kinakamilika lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima nipate haya majibu ili wananchi wajue nusra zake, kama nilivyosema tusisubiri majanga ili uniambie Mheshimiwa Mbunge pole kwa yaliyotokea wakati tuna uwezo wa kuchukuwa tahadhari mapema kunusuru wale wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)