Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Juliana Didas Masaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufanyakazi njema kwa Taifa letu, lakini pili ningependa kupongeza Chama changu cha Mapinduzi kwa kuendelea kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa viwango vya hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende moja kwa moja kwenye mchango, nitaanza kuchangia kuhusu barabara. Pale Musoma tuna barabara ambayo inaanzia Musoma Mjini kupitia Makojo mpaka Busekera ambayo ina urefu wa kilometa 92. Lakini nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri wameanza kujenga kilometa tano tu kwa kiwango cha lami, kilometa takribani 87 hawajazieleza zitajengwa lini. Sasa Mheshimiwa Waziri akija ku-windup hoja yake ningependa kujua commitment ya Serikali ni lini watamalizia kujenga hizi kilometa zilizobaki kwa kiwango cha lami, kwani barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa Musoma Mjini mpaka Musoma Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; ningependa kuongelea kuhusu airport yetu ya pale Musoma, kwanza naishukuru Serikali kwa kufanya ukarabati wa ile airport, lakini Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi ile runway ambayo ndiyo uwanja wa ndege wenyewe ni ndogo sana. Kwa hiyo, itasababisha ndege kubwa kutoweza kutua. Ningependa kuishauri Serikali iweze kwenda pale kuongea na wananchi ambao wanakaa karibu na maeneo yale na kuyanunua yale maeneo ili kupanua ile airport ili ndege kubwa ziweze kutua. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa mdogo wangu kwa mchango wake mzuri, uwanja wa ndege wa Musoma ni muhimu sana kwa wananchi wa Mkoa wa Mara na Serikali imekuwa ikiahidi mara nyingi lakini hawaujengi huo uwanja wa ndege na hasa ukizingatia Mkoa wa Mara unahistoria ya kumtoa mpiganaji wa uhuru wa nchi hii, lakini uwanja wa Musoma haupo kwenye hadhi yake. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Juliana Masaburi unaipokea taarifa hiyo.

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo kutoka kwa dada yangu, senior, Mheshimiwa Ester Bulaya.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tungependa sana huu uwanja uwe ni uwanja wa viwango vya hali ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu; ningependa kuongolea bandari kuu ya pale Musoma Mjini; Mkoa wa Mara ni moja ya mkoa mkongwe sana lakini maendeleo yake ni maendeleo hafifu na duni, yote hii inasababishwa kwasababu hakuna mzunguko mkubwa wa kibiashara. Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako hapa sijaona umeongelea kuhusu ile bandari, ningependa ukija kuhitimisha hoja yako pia uniambie mkakati wako wakuifufua ile bandari kwani bandari ile ni muhimu hasa kwa vijana italeta ajira, lakini ita-stimulate… (Makofi)

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri sana wa mdogo wangu wa Mheshimiwa Juliana Masaburi, ni kweli kabisa hii bandari ile kipindi cha miaka ya nyuma Wakenya, Waganda walikuwa wanakuja kuchukua samaki zinazovuliwa na maeneo ya wavuvi wote wa Mkoa wa Mara, lakini si hivyo tu, tulikuwa tunamali ambayo ilikuwa ikitoka Mwanza, Bukoba inapita pale Musoma inatua kwenye bandari ile kwenda Kenya. (Makofi)

Kwa hiyo, anachochangia Mheshimiwa Juliana ni kwamba bandari ile ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa Mkoa mzima wa Mara. Kwa hiyo nafikiri nataka nimuongozee kwenye hilo ili Mheshimiwa Waziri naye ali-consider hili kama mchango wa Mheshimiwa Mbunge.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Juliana Masabauri unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kaka yangu, Mheshimiwa Chege, napokea taarifa yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Waziri anajua umuhimu wa hii bandari nanaomba ukija kuhitimisha hoja yako utuambie mkakati wako watu wa Mara ni nini unategemea kufanya kufufua bandari hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nianzie alipoishia kaka yangu Mheshimiwa Jerry kuhusu Kampuni ya Sinohydro. Mheshimiwa Waziri Mbarawa hii kampuni ni thuma amanu, thuma kafaru, haitufai Watanzania, hii kampuni ni danganyifu, haimalizi miradi, hailipi madeni yaani sijui hata ipo akhera, sijui wapi mimi hata sielewi, lakini hawa Wachina hawatufai na kwa ufupi hii kampuni inahujumu nchi yetu na bado tunaendelea kuipa kazi nyingi.

Kwa hiyo, Mheshimwia Waziri mimi ningependa ulichukulie hili suala serious na una vyombo vya kuchunguza, mchunguze hii kampuni kwa nini mnaing’ang’ania? Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbarawa kwa kipekee kabisa ningependa pia ukija kuhitimisha hoja yako nadhani utakuwa umeshachunguza na umeshaambiwa. Utuambie nini mpango na hii kampuni? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)