Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kwasababu ya dakika tano nitajielekeza moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na usafiri wa Ziwa Tanganyika, Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Katavi tunaishukuru Serikali imewekeza kwenye bandari, lakini tunajiuliza sana Serikali kuwekeza kwenye bandari ilikuwa inataka ku-achieve nini, tunategemea soko la Congo, Burundi pamoja na Rwanda lakini hatuna usafiri wa uhakika kupitia Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kitendawili ambacho hakina majibu, tunaomba Mheshimiwa Waziri ukija hapa utupe majibu kwenye Mikoa hiyo MV Liemba imefikia wapi ukarabati wake? Lakini ni lini sisi Ziwa Tanganyika tutapata meli mpya kama ile ya zamani imeshindikana tunaomba utakapokuwa una windup utupatie majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini leo tupo kwenye ushindani, tunapozungumzia wafanyabiashara wanaopeleka mazao yao Congo na Burundi kama wanapitia kwenye hizi bandari tukiwa na meli kwa maana nyingine pia tutawafanya wao wasitumie kwenda kupita Zambia, tutawafanya wao wapite kwenye hizi bandari watatokea Kalema na kupeleka mizigo yao Congo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kama Serikali imewekeza kuna shida gani kujenga ile barabara kuja kufika hadi kwenye bandari ya Kalema. Tunaiomba Serikali kwa nia njema hiyo hiyo ambayo imewekeza fedha kwenye bandari hizo basi iweze kutengeneza hizo barabara ili kuwasaidia hao wananchi ambao wanapeleka bidhaa zao Congo, Burundi pamoja na Rwanda.

Mheshimiwa Spika, bado kuna kero kidogo kwenye hizi bandari, ni vizuri tukaziangalia kwasababu tupo kwenye ushindani wa kibiashara zile kero ambazo tunafikiri tunawafanya wafanyabiashara wengine wasitumie bandari hili tuziondoe ili tuweze kupata matokeo chanya kama ilivyokuwa malengo la Serikali ya kuwekeza kwenye hizi bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine Rukwa mpaka leo hatuna uwanja wa ndege, inatufanya sisi tunapokwenda kwenye mikutano tunaulizwa hivi Serikali Rukwa inatuonaje na mimi leo ninakuuliza Mheshimiwa Waziri kila wakati mnaiandika, mnakuja mnasoma hapa, kwenye utekelezaji hakuna, mara upembuzi umefikia hatua gani tunataka majibu leo, Mkoa wa Rukwa ni lini uwanja wa ndege wa Sumbawanga utakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine pamoja na kujenga bandari ya Kabwe lakini kuna changamoto ya ile barabara ya kutoka Lyazumbi mpaka Kabwe na Lyazumbi - Kabwe ni kilometa 60 na hii ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na viongozi wengi.

Mheshimiwa Spika, kuwe na utaratibu mzuri tunapoandaa mpango mnapopeleka kwenye Ilani wawe wanaangalia pia ahadi za viongozi wa Kitaifa, ziwekwe kwenye record ili kwenye utekelezaji inakuwa inaendana na zile ahadi ambazo viongozi wa kitaifa wanazitoa. Kwa hiyo tunaomba tupate majibu juu ya barabara hii ya Kabwe - Lyazumbi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara nyingine ni ya Namanyere – Kirando - Kipili ambapo kuna bandari na ile bandari mtuambie mna mpango wa kuiendeleza au mnataka ife? Watu wa Kipili wanataka kujua. Ile bandari kipindi meli ipo ilikuwa inawasaidia wakulima wa Mkoa wa Rukwa na mikoa mingine ya jirani, leo hatupati majibu na maana ya hizi bandari kwa sababu moja, imezama kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa, lakini mpango wa Serikali ni upi mpaka sasa hivi? Mnataka kuiendeleza au mmeamua kuiacha tu.

Mheshimiwa Spika, leo wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanapokuwa wanapata changamoto ya masoko si kwamba nchi za jirani soko halipo lakini changamoto kubwa ni usafiri na wakati bandari zipo ni suala la commitment na ninyi Serikali mmeminiwa ni lazima tupate usafiri ambao utawasaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tulikuwa tuna MV Liemba na MV Mwongozo ni bora mkaanza na meli moja ya uhakika ikatusaidia Mikoa mitatu kama ilivyo kwenye mikoa mingine na sisi tuweze kuinua uchumi wa Mikoa yetu kupitia usafiri na hizo bandari tulizonazo. Kwa sababu ya huo muda nashukuru kwa muda huo, ahsante. (Makofi)