Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kusema kwamba naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi tangu tumepata uhuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa inafanya jitihada kubwa sana kujenga barabara, lakini leo naomba hotuba yangu niongee barabara kwa Tanzania, nije niongee barabara kwa Afrika Mashariki, mwishoni nitamalizia kwa Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nienze kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais ambaye ni Rais wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwamba tarehe 25 Mei, 2022 atapata tuzo ambayo niseme ukweli tuzo hiyo Mheshimiwa Rais anaistahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini naona kwamba tuzo anaistahili Mheshimiwa Rais; basi nianze kwa barabara mtandao wa Tanzania. Tanzania ina mtandao wa barabara wenye urefu wa takribani kilometa 180,792 kati ya kilometa hizo kilometa 144,429 zipo chini ya TAMISEMI ambazo zinajengwa na TARURA kilometa 36,361.95 zipo chini ya Wizara ya Ujenzi zikijengwa na TANROADS. Kilometa 11,512.9 ni barabara za lami hii ni sawa na asilimia 32 na zilizobaki ni barabara za changarawe.

Mheshimiwa Spika, sasa nije kwenye Afrika Mashariki ambapo Waheshimiwa Wabunge naomba mnisikilize vizuri. Tanzania ina mtandao wa barabara wa kilometa 36,362; za lami ni kilometa 11,513 za changarawe ni kilometa 24,549; asilimia 32 ya barabara zetu ndio zina lami, hiyo Tanzania.

Mheshimiwa Spika, twende Kenya, Kenya ina kilometa 21,583 kwa ujumla; za lami 12,220 zilizobaki kilometa 9,363 lakini Kenya ina asilimia 56 ya barabara zenye lami, lakini mtandao wake ni kilometa 21,583; Tanzania ni kilometa 36,362. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, twende Uganda, Uganda ina mtandao wa kilometa nchi nzima 21,000; kilometa 5,300 ndio zenye lami; kilometa 15,600 ni za changarawe.

Mheshimiwa Spika, twende Rwanda, Rwanda ina mtandao wa barabara kilometa 14,000; kilometa 2,662 ndio za lami. Twende Burundi, Burundi ina mtandao wa barabara kilometa 12,000 zenye lami ni kilometa 1,647.

Mheshimiwa Spika, Watanzania tunajiona kama sisi tupo nyuma, sivyo, sio hata kidogo, Tanzania inakwenda vizuri sana kwenye ujenzi wa barabara na niwaambie ukweli kama Kenya ingekuwa na mtandao mkubwa kama wa kwetu ingekuwa imetuzidi kwa asilimia 3.1; lakini Watanzania tunajiona kama nchi yetu haipo vizuri kibarabara, hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tanzania katika Afrika Mashariki tunafanya kazi nzuri sana naomba Mheshimiwa Waziri pamoja na TANROADS kwa ujumla pamoja na TARURA nitoe pongezi kubwa sana katika ujenzi wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa turudi Dar es Salaam, mimi nitaongea kwa muda mfupi, katika kipindi cha miaka sita Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS wamelijenga Jiji la Dar es Salaam vizuri sana, naomba nitoe pongezi kubwa sana miaka sita iliyopita ulikuwa unaona Nairobi ndio jiji katika Afrika Mashariki, hapana, sasa hivi jiji la Dar es Salaam ni jiji la kimataifa kwa sababu ya ujenzi wa barabara unaofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kweli Mheshimiwa Rais anakwenda kupata tuzo aliyoistahili, kaangalieni Dar es Salaam sasa hivi, nirudi kwenye takwimu Dar es Salaam ina ukubwa wa kilometa 655.6 zenye lami na gharama za barabara za Dar es Salaam ni trilioni 2.055. Naomba niipongeze sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mbarawa, naomba niwapongeze TANROADS na TARURA kuifanya nchi yetu iwe na barabara bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Watanzania muwe mnaangalia takwimu, wale mnaoweza ku-google m-google vizuri bado Tanzania katika Afrika Mashariki tupo vizuri sana upande wa barabara. Situtaka kuongea kwa dakika nyingi nilitaka kuitoa hiyo picha kamili ya nchi yetu upande wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, nakupongeza sana Mheshimiwa Mbarawa. (Makofi)