Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia fursa hii kuweza kuchangia Wizara hii.

Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya Taifa letu, jinsi anavyotuongoza, namna anavyolipeleka Taifa letu mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa namna hiyo hiyo niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya na Naibu Waziri na timu yake yote kwa ujumla. Kazi wanazozifanya ni kubwa, kazi wanazozifanya ni za kupigiwa mfano. Jitihada zao zitatupeleka pale ambapo Rais wetu ana malengo ya kuifikisha Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uongozi siku zote ni dhamira, uongozi ni maono, uongozi ni wito. Niwapongeze na niwaambie kwamba tunaona kazi kubwa wanayoifanya na kwetu sisi umekuwa ni ufahari mkubwa hasa pale alipokuwa Katibu Mkuu wa Wizara hii ni mwanamke. Wizara inafanya vizuri, Waziri na timu yako mnasimamia vizuri, lakini sisi wanawake kwetu ni ufahari kumuona mwanamke mwenzetu yuko pale na anafanya vizuri, tunaamini na imani yetu kwake ni kwamba, yeye ni miongoni mwa wanaosababisha wewe ukafanya vizuri pia kazi zako kwa sababu mara nyingi mwanamke ana namna ya kipekee katika kuongoza. Tunashukuru na tunampongeza Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kulipongeza Shirika letu la TRC kwa kufanya vizuri, kwa kufanya kazi nzuri. Kwanza kabisa nianze pale kwenye makusanyo yao, wamekusanya kwa mwaka wa fedha 2020/21 shilingi bilioni 50 kutoka shilingi bilioni 30, ni kazi nzuri ya kupigiwa mfano. Kwetu sisi tunasema ni pongezi tunampongeza. Sisi viongozi tuna namna, kuna muda hatuna jinsi hatuwezi kujizuia hisia zetu, kama watu mnafanya kazi vizuri lazima Waziri tuwapongeze, mnafanya kazi vizuri, tunawaona mkifanya kazi vizuri. Kama mnavyotuvumilia pale mnapoharibu tukiwaambieni mnaharibu na mpokee pongezi zetu mnapofanya vizuri hatutasita kusema mnafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitegemea kwenye shirika letu kipindi hiki tulichoingia kwenye misukosuko ya covid, kwenye misukosuko ya mfumuko wa bei ya mafuta ambayo imetawala takribani dunia nzima ambapo pia tumpongeze Rais wetu, kwa upande wa Serikali yetu ya Tanzania Rais amechukua fursa ya kipekee akitupunguzia bei ya mafuta na kubana maeneo mengine. Mheshimiwa Waziri tulitegemea shirika hili kwenye mradi wa SGR ungekuja na mambo ya ajabu, tulitegemea tukaona fedha zote na upigaji kipindi hiki ndio ungeingia; kwenu imekuwa tofauti, mambo yanakwenda, yanaserereka kama nyoka yuko kwenye majani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado mmekuwa wazalendo, mmekuwa waungwana, mnamsaidia Rais, mnafanya kazi nzuri. Bado mikataba yenu imesimama palepale kwa fedha zilezile ambazo mmekubaliana na ujenzi huu. Mnamsaidia Rais, mnastahili pongezi, mnastahili sifa. Endeleeni kuwa wazalendo, Tanzania haitajengwa na kila mtu, Tanzania itajengwa na wenye uchungu wa Tanzania na wenye uzalendo wa Tanzania. Mheshimiwa Waziri kwenye eneo hili niendelee kukupongeza na timu yako, lakini usisahau mwisho wa pongezi mwanamke mwenzetu tunampongeza zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye suala la bandari; tunawashukuru watendaji wanaendelea kufanya vizuri, wanasimamia bandari vizuri. Tunawaona wanatafuta, Mtendaji Mkuu wa Bandari anatafuta kila namna ya kuona bandari yetu itafanyaje ili iweze kufanya vizuri. Tunawaona wakishiriki maeneo tofauti, wanashiriki katika maeneo ya matangazo, wanaitangaza bandari yetu ipasavyo, kwa sababu bandari yetu pia, imepakana na nchi jirani nazo pia kuna nchi zina bandari, wachukue fursa hiyo kuangalia bandari za wenzetu wapi wamefanikiwa, nini kwetu kinakwama, lakini Mheshimiwa Waziri tushauri. Sisi hapa tuko Wabunge tunakushauri, lakini usisite chukua pia na ushauri wa watu wa chini. Kuna watu tunaweza tukawadharau, lakini wanaweza wakakupa ushauri mzuri na mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chukulia watu ambao wanaendesha ma-container wanaopeleka ndani ya mipaka yetu, kuna muda pata muda kaa nao kikao, wasikilize, changamoto, maeneo gani, kuna tatizo gani? Utakapowasikiliza kuna watu wako nje hawajapata fursa ya kuwepo hapa kwa sababu, kuna wachache wanaoweza kuingia, lakini wana michango mizuri ya kuweza kuisaidia nchi hii, wana michango yenye afya. Ukitumia fursa hiyo ukitaka kuwasikiliza, Mkurugenzi wa Bandari mkitumia fursa hiyo kaka yangu ukawasikiliza utavuna kitu, utapata mabadiliko. Jitihada zako tunaziona na haziendi bure, tunaziona na tunazithamini unafanya kazi nzuri, ili iendelee kuwa nzuri zaidi shuka na chini sikiliza maoni, wasikilize wale ambao wanatumia zile bandari, utapata mambo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini miradi maeneo makubwa ya bandari yanayosimamiwa ni kwenye changamoto kubwa. Na tunaona kwa asilimia kubwa changamoto zimepungua na zinatatuka kwa jitihada ya wasimamizi waliokuweko pale. kuna changamoto nyingine ni ndogo ndogo, sisi tukisimama hapa tunaowakilisha wanawake lazima tuziseme. Bandari yetu pamoja na changamoto kubwa zinazoendelea kutatuliwa kuna changamoto ya wanawake kwenye utumiaji wa bandari yetu, matumizi ya ndani ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, boti imekwenda kule imerudi kule; kuna watu nitawazungumzia kwa wakati huu, kuna watu pale wenye mahitaji maalum; kuna wanawake wajawazito, kuna wanawake watu wazima/wazee, lakini tuboreshe. Mkurugenzi wa Bandari boresha lile eneo, ona wanawake wale wanahudumiwa vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninatamani tukitoka hapa tukimaliza Bunge la Bajeti mwezi wa sita nifuatane kwenda Zanzibar tutumie bandari, Waziri, Naibu Waziri, Mkurugenzi na watendaji wako wote tuone mifumo ambayo inatumika bandarini. Mwanamke mjamzito anafika kushuka boti anasema anakwenda Dar es Salaam lazima asukumwe, apitishwe msukosuko ndio aweze kupita. Kabeba Rais wetu, kabeba Waziri kama ninyi, kabeba Wakurugenzi kama ninyi, mnafanya vizuri na ninaamini mmejielekeza zaidi kutatua matatizo makubwa, lakini watizameni watendaji wenu wa chini wanaowafuatia, waambieni haya matatizo madogo madogo ambayo hatupaswi kusimama hapa kuyaelezea wayatatue nayo, kwa sababu kwetu sisi ni kero.

Mheshimiwa Spika, sisi tunawakilisha wanawake. Mimi mtumiaji wa bandari ninaona utofauti mkubwa wa bandari ya kipindi cha nyuma na sasa. Zamani tulikuwa tukishuka boti kutoka Zanzibar mpaka tusubiri ma-container yatoke, sasa hivi hayapo hayo, kila kitu kinakwenda kwa wakati. Mheshimiwa Waziri na watendaji wako tuboresheeni sisi tunaotumia bandari ili tuweze kutumia bandari yetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa namna ya kipekee naomba nimpongeze Mkurugenzi wa Shirika la ATC kwa kazi kubwa anayoifanya, shirika lilipokuwa sipo sasa lilipo, unajitahidi, mnafanya kazi nzuri. Si kazi ndogo kufanya shirika lipande juu.

Mheshimiwa Spika, na kwa namna ya kipekee kwetu shirika limekuwa la ufahari maana kwa sasa tunaitangaza Tanzania ipasavyo, kati ya ndege zake basi kuna ndege nayo imeandikwa Zanzibar, tunaamini siku moja kama kuna ndege zina twiga zina nani iko siku tutauona na mkarafuu wa Zanzibar nao upo kwenye ndege zile. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, kwetu imekuwa ni ufahari tunaamini tunatangaza utalii, lakini pia kwenye ndege zile tunatangaza nchi yetu kwa ufahari mkubwa. Nichukue fursa hii kuendelea kuwapongeza...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, muda wako umeisha.

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)