Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu kabisa, Wizara ya Uchukuzi na Miundombinu na mambo yote ambayo yanahusu maendeleo na maisha ya binadamu.

Mheshimiwa Spika, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan, lakini pia niwapongeze Mawaziri wote kwa kufanya kazi nzuri pamoja na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, watendaji wa Serikali nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia mchango wangu katika Wizara hii nilipenda niongelee jambo moja kuhusiana na fedha ambazo zilipelekwa kwenye bajeti ya TARURA ya mwaka 2021/2022. Kama unavyojua kwamba hizi fedha tuliziomba mwaka 2021 na Mheshimiwa Rais akatusikiliza Wabunge akaongeza bajeti ili tuweze kutengeneza barabara zetu, kwa sababu Mheshimiwa Rais alivyokuwa anafanya ziara aligundua kwamba sehemu nyingi/mikoa mingi/majimbo mengi barabara ni mbovu ndio maana akaongeza ile bajeti kwa watu wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mimi nilipata taarifa kutoka kwa watendaji wangu wa TARURA kwamba fedha ambazo tulikuwa tunazitegemea kwenye Jimbo letu shilingi milioni 800 sasa zinaelekezwa kwenye Postikodi. Namshukuru Mheshimiwa Nape Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia alilisemea juzi kwamba hizo fedha zirudishwe kwenye miradi ya TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nilikuwa ninaomba Mheshimiwa Waziri husika wa TAMISEMI alisemee hili jambo kwa sababu kuna majimbo mengine hizi fedha zimeshachukuliwa na kuna majimbo mengine tayari zimeshawekewa mipango ya kwenda kwenye hizo Positikodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana sana hili jambo lisifanyike, wananchi wetu tumewaahidi, tumeshafanya mipango mingi na tumeshakaa mikutano mingi na wananchi kwa ajili ya hizi fedha. Mfano kwenye Jimbo langu nimeshakaa kwa ajili ya hizi fedha ambazo ninazisubiri shilingi milioni 800 na Kata ya Segerea Machimbo zinakwenda kufanya kazi hii. Kwa hiyo, zikitolewa itaonekana kama mimi Mbunge nimezungumza mambo ya uongo. (Makofi)

Lakini jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kushauri mambo ambayo tumeyapanga hapa na tukayapangia bajeti, wataalam wanapata wapi nguvu ya kutoa bajeti ambayo sisi tumepanga na tumepitisha Bungeni na kuelekeza kwenye miradi mingine? Hii inakuwa sio sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sisi tunaongea na wananchi direct ndio wametupa vipaumbele vyake na tukishaongea hapa tukipitisha tunategemea wenyewe wananchi wafanye kazi kwa ushirikiano na sisi. Sasa wenyewe wanapokaa huko na kupanga mipango yao bila kutuhusisha sisi inakuwa sio sawa. Naomba hilo lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili sasa naanza mchango wangu kwenye Wizara hii. Katika Jimbo langu la Segerea, eneo la Airport kuna wakazi wangu 1,800 tangu mwaka 1997 hawa watu wamehamishwa, wameambiwa kwamba wanatakiwa wahame hilo eneo. Wengine wamefanyiwa tathmini, wengine hawajafanyiwa tathmini mpaka hii leo, nimekuwa nikiongea hapa kwa kipindi chote nikisimama hapa kuwaongelea hawa wakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo hilo sasa Kipawa, Mtaa wa Kipunguni hakuna maendeleo yoyote. Kwanza tunavyopanga mipango yetu ya kupeleka barabara au kupeleka maji lile eneo wanaliruka wanasema hili eneo hawa wananchi wake watahama, kwa hiyo, hakuna haja ya kupeleka hii mipango ya maendeleo.

Kwa hiyo, kwa kipindi hicho chote nilichokielezea hakuna mwananchi pale anayefanya maendeleo yoyote na kama unavyojua mtu anaweza akawa ana leseni yake ya makazi, anataka aende kuchukua mkopo hawa wananchi hawawezi kwenda kuchukua mkopo kwa sababu airport wamekwenda kuweka jiwe lao la msingi pale kuonesha kwamba hicho ni kiwanja chao na wakati hawajawalipa hawa wananchi. Kwa masikitiko kabisa hili jambo nimeliongea na mwaka jana nimeliongea, lakini Serikali halilifanyii kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi hiyo sehemu imekuwa watu wanaishi hawaelewi na kibaya zaidi wamekwenda wamewalipa watu nusu, wameacha nusu. Kwa hiyo, wale nusu waliobaki pale wanaendelea kupata shida hawawezi kufuga kuku, hawawezi kupata mkopo wowote, hawawezi kufanya kitu chochote kwa sababu hilo eneo linajulikana ni eneo la airport na wameshaweka hilo jiwe lao. Kwa hiyo wanawafanya hawa wananchi waendelee kuwa masikini sio sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilitaka kuongelea ni kuhusiana na watendaji wetu wa TANROADS, nawapongeza wanafanya kazi nzuri, lakini kuna mahali inabidi warekebishe, yaani TANROADS wanapokuwa wanataka kuweka viraka wanatoboa barabara kuanzia mwanzo mpaka mwisho halafu wanaondoka wanakwenda wanakaa miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukizingatia barabara zetu ni mbovu, halafu sisi watu wa Segerea tunatumia barabara moja, barabara ya Tabata ambayo inatoka inakwenda mpaka sehemu zingine. Sasa unapokwenda unaitoboa ile barabara halafu unaondoka, unawatafutia watu matatizo kwa sababu watembea kwa miguu wanapitia hiyo barabara, magari wanapitia hiyo barabara, lakini bodaboda pia wanapita hiyo barabara.

Kwa hiyo, tunaomba watendaji wa TANROADS waongeze speed, wanapokuwa wanaparua hizi barabara au wanazichimba wazifunike haraka.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nilitaka niongelee hao hao TANROADS, kuna barabara nyingi ambazo wenyewe ndio wanaziangalia, kwa mfano barabara ya Tabata nilikuwa ninashauri ile barabara ijengwe upya kwa sababu hii kila siku kuifanyia marekebisho ni kupoteza gharama kubwa, ile barabara imeshakuwa mbovu tunaomba ijengwe upya. (Makofi)

Lakini pia barabara yetu ya Kinyerezi – Bonyokwa – Kimara; hii barabara tangu TANROADS wameanza kuifanyia upembuzi yakinifu sasa hivi ni miaka mitatu na tulikuwa tunategemea kwamba hii barabara itaanza kujengwa sasa hivi, lakini mpaka sasa hivi na mimi nilishawahi kukuambia Waziri kwamba hii barabara ni muhimu sana. Kwa sababu ndio inayotoa watu mjini wanapitia Bonyokwa wanakwenda Kimara, kwa hiyo mkitujengea hii barabara mtakuwa mmetusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama unavyojua Mheshimiwa Waziri na Wabunge wenyewe Dar es Salaam ndio inayoingizia mapato hili Taifa asilimia 70 kwa hiyo, Dar es Salaam ikiwa ina barabara nzuri ina maana hayo mapato yataongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kitu kingine sisi watu Dar es Salaam hatuna kitu kingine tunachoomba zaidi ya barabara na maji. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maji, tulikuwa tunalalamika maji Mkoa wa Dar es Salaam, lakini amefanya, nampongeza sana yeye pamoja na Naibu wake pamoja na Mkurugenzi, lakini kwenye masuala ya barabara yaani bado sana Mheshimiwa Waziri. Tunaomba mtuangalizie hizo barabara zetu ambazo tunazisema kila siku.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono. (Makofi)