Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana, kazi anazofanya matunda yake tunayaona. Leo nimefarijika sana kusimama mbele ya Bunge hili na kutoa shukrani za dhati kabisa kwake kwa kazi kubwa anayofanya hatimaye leo tuna bajeti nzuri sana ya Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, wamejipanga vizuri, wanafanya kazi nzuri na ni wasikivu. Niliwaomba Bunge lililopita tuna tatizo Mvumero, mvua zimenyesha na daraja limekatika, moja kwa moja hawakuwa na kigugumizi waliniambia twende na siku ya Jumamosi niliondoka nao tulienda Mvomero. Waziri alitoa maelekezo ndani ya siku saba daraja lile kingo zote zilitengenezwa. Hii ndiyo kasi ya Magufuli, nawapongeza sana kwa kazi kubwa wanayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ambalo napenda kuchangia ni Kurasini, upande wa bandari yetu. Eneo la Kurasini kuna msongamano mkubwa sana wa malori. Malori yale sasa hivi yanasababisha msongamano ule unaendelea hadi Kibaha. Niwaombe wenzetu watafute namna bora na kutafuta eneo lolote kujenga haraka dry port kati ya Kibaha na Morogoro ili tuondoe msongamano ule, tuboreshe miundombinu na uchumi usonge mbele. Bandari na barabara zinapanuliwa lakini bado malori yale yanaleta msongamano kubwa sana. Malori ya mafuta na makontena hali imekuwa mbaya. Tunaomba wenzetu walifanyie kazi, nina imani wanalifahamu hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba pia nizungumzie kidogo tu daraja la Kigamboni. Kazi iliyofanywa ni kubwa sana, daraja zuri na la mfano. Nimuombe Waziri katika maeneo mawili, tunajua gharama iliyotumika pale ni kubwa, magari ya abiria hususani daladala wanaovuka kwenye daraja lile wanalipa shilingi 7,000, daladala ambayo imepakia watu 30, akimtoza abiria shilingi 400; anapata shilingi 12,000 akilipa shilingi 7,000 kabaki na shilingi 5,000. Serikali hii ni sikivu jaribuni kulifanyia kazi jambo hili, kwa magari ya abiria tariff ipunguzwe. Tunaweza tukaweka shilingi 2,000 au shilingi 1,500/=, magari mengine yote Lexus, VX, hata shilingi 10,000/= watu watalipa, lakini magari ya abiria tuyaangalie. Tupunguze kidogo ili wananchi wetu waweze kufaidika na matunda ya daraja lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala la baiskeli, kuna mtu ana madafu na machungwa yake anatoka Kigamboni anafika pale anatozwa hela nyingi. Naomba baiskeli nazo zisaidiwe wengine wote waendelee kulipa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri haya mawili naomba uyafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie suala la uwanja wa ndege wa Dar es Salaam (Terminal II). Pale kuna msongamano mkubwa, wakati tunaendelea kusubiri Terminal III upande wa arrival, kuanzia saa saba mchana mpaka saa tisa au saa kumi, ndege ni nyingi, mizigo ina-delay sana kutoka kwenye ndege kuja eneo la abiria. Tunaomba juhudi za haraka zifanyike ili abiria wasikae muda mrefu. Ndege zinagongana, moja inaingia saa saba, nyingine saa nane na nyingine saa sita, naomba sana suala hili lifanyiwe kazi, wakati tunaendelea kusubiri matunda mazuri ya Terminal III. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niingie Mvomero. Mvomero tuna daraja ambalo nimemshukuru Mheshimiwa Waziri kazi nzuri imefanyika. Sasa hivi tuna mradi wa barabara ya lami kutoka Magole – Turiani - Handeni. Mpango wa barabara hii tokea mwanzo ilikuwa lami iwekwe Korogwe - Handeni, Handeni-Turiani, Turiani-Magole ili Magole pale magari yote yaelekee Dodoma na Kanda ya Ziwa, abiria wa Mombasa, Tanga na maeneo mengine wapite barabara ile ya shortcut. Naishukuru sana Serikali mwaka huu Mheshimiwa Waziri ametenga fedha nyingi kumalizia kilometa 48 za awali kutoka Magole – Turiani, hilo tunalishukuru sana na wananchi wanasubiri kazi ianze.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hili mkandarasi anadai fedha za nyuma, naomba Mheshimiwa Waziri ili aanze kazi mngekaa naye mkamaliza madeni ya nyuma. Kampuni ya Kichina inadai fedha kidogo za nyuma, hapa mme mtengea fedha nyingi, malizaneni naye aanze kazi mara moja. Naomba barabara ya kutoka Turiani - Mzia - Handeni ambayo tayari mmeshafanya upembuzi yakinifu, tengeni fedha tufungue mlango wa lami Korogwe mpaka Magole kuelekea Dodoma na Kanda ya Ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, barabara ya kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, wanaita Sangasanga – Langali - Mgeta. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alituahidi barabara ile itajengwa kwa kiwango cha lami. Naona mwaka huu wametenga fedha shilingi milioni 700 kwa kilometa mbili, sijui lami nyepesi au nzito sielewi. Naomba suala hili Mheshimiwa Waziri nikukumbushe kwa niaba ya wananchi wa Mvomero ili ahadi ile ikamilike tuendelee kupata matunda mazuri ya Serikali ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la minara ya simu nimeshakwenda kwa Mheshimiwa Waziri mara nyingi na aliniambia kuna mpango wa kupeleka mnara Kibati. Kwenye kitabu chake cha mawasiliano, ukurasa wa 18, namba 272 na 273 ameonesha kuna mnara Kanga na Kibati na minara hii imetengewa fedha nyingi, mnara mmoja anasema haujawaka, mwingine umewaka. Mheshimiwa Waziri minara yote haipo, hakuna uliowaka na hakuna ambao umezimwa. Mheshimiwa Waziri nilimpa kilio changu cha wananchi wa Kibati na akaniunganisha na watu wa Halotel…
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja mia kwa mia.