Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukushukuru kwa kupata nafasi hii. Kwanza kabisa ningependa nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anafanya kwa bajeti hii ya kihistoria ambayo ameipatia Wizara hii ya Kilimo, Pili napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na crew nzima ya Wizara ya Kilimo kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita katika masuala makubwa matatu. Suala la kwanza ni suala la motisha kwa Maafisa Ugani. Wiki chache zilizopita umefanya jambo kubwa sana kugawa pikipiki 7,000 kwa Maafisa Ugani, haijapata kutokea toka Wizara ya Kilimo imeanza. Hili ni jambo la kutia moja kwa maafisa wetu wa ugani ambao wanafanya kazi kubwa kabisa katika kuinusuru sekta hii ya kilimo nchini. Vilevile nilikusikia ulimuomba Mheshimiwa Rais kwamba pikipiki zile wakizitumia kwa muda wa miaka miwili basi wazichukue ziwe mali yao, hili ni jambo kubwa sana na jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba isiishie hapo tu hawa Maafisa Ugani sasa hivi wanatakiwa wapangiwe utaratibu kwa mazao yote ya kimkakati katika Mikoa, wanatakiwa sasa hivi waambiwe kabisa kwa mfano, ile sehemu ambayo wanatakiwa walime alizeti wapewe kiwango au target kwamba tunataka Mkoa fulani mzalishe tani fulani na mtakapozalisha tani fulani za alizeti basi mtapata percent fulani itakuwa mali yenu, ninakuakikishia hao watafanyakazi usiku kucha hawatalala kwa sababu ya kufukuzia hizo percent ambazo utawapatia na mambo yatakuwa mazuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu umwangiliaji, nimeona bajeti kubwa sana ya umwangiliaji imeongezeka kutoka Bilioni 46.5 mpaka Bilioni 361.5 haya ni mageuzi makubwa sana. Lakini kuna sehemu ambazo umezisahau katika miradi ya umwagiliaji, kwa mfano pale kwangu Bangamoyo kuna skimu ya umwangiliaji ya Ruvu maarufu kama JICA haimo kabisa katika mpango wako, siyo tu Bangamoyo nimesoma almost hotuba yako yote, Mkoa wote karibu skimu niliopata ni moja tu ambayo iko Rufiji inaitwa Ngongoro ambayo iko katika upembuzi yakinifu, lakini katika skimu za umwangiliaji zilizofanyiwa upembuzi yakinifu hakuna, skimu za umwangiliaji za Mwaka wa Fedha 2022/2023 hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyotambua Bangamoyo kuna mradi mkubwa sana, sasa hivi tunawaandaa outgrowers kwa ajili ya kilimo cha miwa ili waweze kulisha shamba la Bagamoyo Sugar lakini hakuna utaratibu wowote na wala hakuna mpango wowote wa kujenga bwawa au kuweka miundombinu ya umwangiliaji kwa ajili ya kunusuru wakulima hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la mwisho ni la uboreshaji wa masoko, tutakuwa tunasema kilimo tunapanga mipango ya kulima kwa bidii zote lakini tusipokuwa na masoko kwa bidhaa zetu tunazolima tutakuwa tunajisumbua. Lazima tuwekeze nguvu zetu sasa hivi kuhakikisha kwamba tunapata masoko kwamba wananchi wanapohamasishwa kulima wanalima lakini baadaye inakuja wamelima kwa nguvu zote, masoko hakuna wanarudi nyuma, mwaka unaofuata hawalimi tena Taifa linakuwa kila siku linapiga mark time tu haliendi, kwa hiyo tuelekeze nguvu zetu katika Maafisa wa Masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ikiwezekana hawa Maafisa wa Masoko waambieni kabisa mtu atakayetutafutia soko la bidhaa fulani nchi fulani tutampa kamisheni kutokana na mauzo yatakayofanyika ya yale mazao ambayo yataunzwa katika nchi husika. Kwa hiyo hapa kutakuwa na jitihada kubwa sana ambayo inafanyika watajitahidi, vilevile tusisite tuongee na Wizara ya Mambo ya nchi za Nje, tuwatumie diaspora kule watutafutie masoko ya bidhaa zetu kwa sababu tunalima. Tumeona miaka miwili iliyopita anguko la mbazi, mbaazi ilikuwa bei yake kubwa sana, mimi niliwahi kulima mbaazi, niliuza kilo Shilingi 2,300 shamba kipindi cha nyuma, lakini baadaye mbaazi ikashuka ikawa inauzwa mpaka Shilingi 300 kwa kilo na wanunuzi hakuna. Sasa lazima tujipange kuhakikisha kwamba masoko yanafanyiwa kazi na hawa Maafisa Masoko waandaliwe ili waweze kuinusuru Wizara na kulinusuru Taifa ili liweze kufanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)