Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na leo niko hapa nawakilisha Bunge kupitia Jimbo la Mlimba kwa tiketi ya CHADEMA. Ahsante sana wananchi wa Mlimba kwa kunipa heshima hii na ahsante Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwa kuniteua kuwa Mbunge bila kujali jinsia yangu na nitawakilisha na nitatoa heshima kwa chama na nchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitaunga mkono Kitaifa Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara hii. Sasa kwa kuwa chama changu kimeniamini na kunipeleka Jimbo la Mlimba, niwatendee haki wananchi wa Jimbo la Mlimba kwa sababu ni Jimbo jipya na mambo mengine yote yanakwenda kiupya upya. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliuliza swali Bungeni na nikapata jibu zuri kutoka kwa Wizara husika kwamba mwezi Juni kwenye ile barabara ya Ifakara mpaka Madeke-Njombe, inayounganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe inakwenda kumalizika kwa ule utaalam wanasema feasibility study. Sasa, baada ya feasibility study wananchi wengi wakisikia wanadhani ikimalizika hiyo ndipo wanakwenda kujenga barabara, kumbe kuna ile detailed design ambayo itahusika na mambo ya michoro, ujenzi, gharama halisi na mambo kadhaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kupata majibu ya Serikali, inifahamishe na iwafahamishe wananchi, baada ya kumalizika mwezi wa Sita hiyo michoro ya ujenzi na gharama halisi ya ujenzi ni lini Serikali itakwenda kufanya na itachukua muda gani? Baada ya hapo je, Mkandarasi Mshauri atapatikana wakati gani na ujenzi wa barabara hii utaanza lini? Pia je, Serikali imejiandaa vipi kutenga fedha katika kujenga barabara hii yenye urefu wa kilometa 124.2. Nikipata majibu haya ya Serikali itanipa furaha na itanipa kujiandaa ni namna gani barabara hii itakwenda kujengwa, siyo kila wakati nilete maswali Bungeni, maana nitajua ni muda gani barabara hii inaweza ikaanza kujengwa. Naomba nipate majibu haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoingia katika kitabu cha randama cha Waziri nimekwenda kwenye ukurasa wa 100 inaonyesha miradi ya maendeleo ya barabara Mlimba haimo. Nimekwenda ukurasa wa 111, miradi inayotekelezwa kwa miradi ya barabara Mlimba haimo. Nimekwenda ukurasa wa 116, mchanganuo wa miradi ya barabara za mikoa inayoendelezwa kwa kutumia Mfuko wa Barabara 2016/2017, imo Ifakara – Tawete – Madeke including crossing of Mngeta. Si Mgeta, kwenye kitabu chenu mmeandika Mgeta, mgeta si Mlimba, Mgeta iko Morogoro, iko Mvomero, naomba mrekebishe wekeni Mngeta, siyo Mgeta.(Makofi)
Sasa nimekwenda ukurasa wa 136, nikaona matengenezo ya muda maalum kutumia fedha za Mfuko wa Barabara Mlimba hakuna. Nimekwenda ukurasa wa 139 mpaka 147, barabara za mikoa za changarawe, udongo Ifakara – Taweta – Madeke, kilometa 57.59 makadirio mmetenga milioni 594, hapa kuna shida! Hii barabara naijua, naipita mara nyingi, matengenezo hayo bora mngechanganua, kama ni changarawe weka changarawe kilometa kadhaa, kama udongo weka udongo kilometa kadhaa. Mkiweka jumla hivyo hii barabara inatengenezwa kwa udongo asilimia 100. Kwa hiyo, ni vyema kuchanganua ili tujue kilometa ngapi changarawe, kilometa ngapi udongo ili wananchi wapate kufuatilia na mimi mwenyewe kama Mbunge nipate kufuatilia wakati napita hiyo barabara maana tunadanganywa sana na wakandarasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 157 mpaka 163, maeneo korofi; kutumia fedha za Mfuko wa Barabara za Mikoa Mlimba hakuna, eeh! Hapo ndipo nikashangaa. Hii barabara muda wote haipitiki na mpaka mje kujenga itachukua miaka kadhaa. Sasa kama hamtengi pesa katika barabara hii katika maeneo korofi huyu Mkuu wa TANROAD Mkoa wa Morogoro mnayempigia simu kila kukicha wakati matatizo yanapotokea atapata wapi hela za kwenda kutengeneza maeneo korofi katika barabara ya Ifakara – Mlimba mpaka Madeke-Njombe? Naomba mrekebishe vitabu vyenu, iingizeni na hiyo barabara ili tunapopata matatizo tupate kutibu haya maeneo korofi. (Makofi)
Barabara za mikoa na madaraja mmeweka, tuna madaraja saba, yaani ni hivi, katika Mkoa wa Morogoro na nchi hii, kama kuna mkoa wenye madaraja mengi basi ni Morogoro. Hata mkiangalia kwenye ile list ya madaraja utakuta tumekwenda mpaka 291, hakuna mkoa mwingine Tanzania wenye madaraja mengi. Madaraja hayo ukiangalia mengi yako katika Wilaya ya Kilombero na Jimbo la Mlimba, kwa hiyo, ni bora mtuangalie kwa umakini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na mambo hayo, ngoja nieleze hali halisi ya Jimbo la Mlimba, najua Waziri hajafika, Naibu Waziri hajafika, naomba mfike mkaangalie ili mnapopanga mipango yenu muone ni namna gani mtasaidia Jimbo la Mlimba. Jimbo la Mlimba kuna kilimo kikubwa cha mpunga, mradi unaitwa KPL, uwekezaji, karibuni hekta elfu tano na kitu! Magari yanayotoka pale kupeleka mchele si chini ya tani 30 na barabara hiyo ni ya udongo. Kwa hiyo, muone hali halisi ya Jimbo la Mlimba na ni namna gani mtaiwekea, kama barabara zitapelekwa kwenye eneo la uwekezaji, basi Mlimba ingepewa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Jimbo la Mlimba lina mradi mkubwa wa umwagiliaji pale Kijiji cha Njagi, wasilianeni na watu wa Idara ya Umwagiliaji wa Kilimo. Kuna mradi mkubwa, Serikali inaingiza mabilioni ya fedha, sasa kama hatuna barabara ina maana hizo hela mnazowekeza Serikali ni bure. Naomba mlipe kipaumbele Jimbo la Mlimba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mlimba kuna kilimo kikubwa cha ndizi, kokoa, ufuta, kila aina, kuna mradi wa umeme Kihansi, kuna mradi wa RUBADA, unakwenda kulimwa kule katika Kijiji cha Ngalimila, hekari na mahekari. Hebu angalieni miradi inayopelekwa Mlimba na hali halisi ya barabara, barabara ni mbovu, hazipitiki mwaka mzima, sasa utajiri wa Mlimba na kuhusu miundombinu haifanani kabisa, naomba muipe kipaumbele.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niingie katika masuala ya usafiri wa treni ya TAZARA, ingekuwa treni ya TAZARA imeimarika angalau wananchi wangepata fursa ya kusafiri, lakini TAZARA bado iko kwenye mgogoro mkubwa, wafanyakazi wa TAZARA wako kwenye shida kubwa. Ni namna gani mafao yao, ni namna gani mishahara yao, kwa kweli, naomba muangalie suala la TAZARA hasa katika Jimbo la Mlimba, imepita karibuni jimbo zima, wapeni mafao yao, imarisheni reli, najua itachukua muda mrefu, basi muwaimarishe, muwape mafao yao ili wananchi wale wapate kuishi maisha yanayostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mawasiliano, nimekwenda nimeangalia katika kitabu cha mawasiliano ukurasa wa 18, ni kweli mmesema, kuna kata mbalimbali ambazo hakuna mawasiliano, lakini mmesema mnara haujawashwa, naona sasa, ni vyema mkawashe, kwa sababu hatuna barabara, simu hatuna, jamani, sisi tuko kwenye dunia gani? Naomba sasa mtuimarishie mawasiliano ya simu, mpeleke minara, muharakishe ili tupate mawasiliano ya barabara, maeneo korofi tupate hela na vilevile mawasiliano ya simu ili yaani ni shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ukiona akinamama na watoto wanakufa, basi wanatokea Jimbo la Mlimba kwa sababu hakuna barabara, hospitali kubwa hamna. Matatizo ni makubwa mno. Naomba mtembee, mje katika Jimbo la Mlimba muone hali halisi ili wakati mwingine mnapokuja na bajeti muiangalie kwa jicho la huruma, jicho la kweli katika Jimbo la Mlimba ili tupate maendeleo na sisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina maneno mengi, mambo mengine nitaleta mwa njia ya maandishi katika ofisi yako, maana mnakosea majina ya maeneo yangu na vijiji, ili muone kwamba mwaka ujao nikija angalau nije sasa na mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kuwasilisha.