Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge hili tukufu ili niweze kutoa mchango wangu wa mawazo ambao binafsi naamini unaweza kusaidia Taifa langu kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru awamu zote sita za Uongozi wa Taifa letu. Namshukuru Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Mwinyi, Hayati Benjamin Mkapa, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Hayati Dkt. Magufuli na sasa tuna Mama Samia Suluhu Hassan. Watu wote hawa wanaendelea kupeleka Taifa letu mbele. Mimi kama Mtanzania nina kila sababu ya kuwashukuru kwa sababu wamefanya maisha yangu yamekuwa bora kwa mambo waliyoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ambacho nimezoea kukisema kila siku, na nitakirudia tena na tena kwamba tuna Rais smart, intelligent and clever, na nitatoa sababu. Huko nyuma niliwahi kusema, alipewa fedha za barakoa akajenga madarasa. Sasa nataka niwaambie kitu kingine leo. Tanzania inauza zaidi Kenya kuliko inavyonunua, la kwanza. La pili, uchumi wetu umekua ndani ya miaka miwili kutoka Dola bilioni 69 mpaka 85. La tatu, ndani ya muda mfupi amefanya kile ambacho wengine kiliwashinda kwa upande wa demokrasia. Amefanya jambo lililokuwa linamtia hofu kila mtu la kuruhusu mikutano ya hadhara ya wapinzani. Amefanya jambo kubwa sana la kwenda mpaka kwenye mkutano wa Umoja akina Mama wa CHADEMA. Maana yake nini? Maana yake ni kwamba amebadilisha taswira ya nchi yetu Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimwona Makamu wa Rais wa Marekani amekuja hapa akatamka, Marekani ikatamka ya kwamba Tanzania is a democratic country, tumemaliza. Ile peke yake ni smartness. Nataka niwaambie, hiyo ni smartness, subirini muone misaada itakavyomiminika kuja hapa nchini kwa sababu ya kitendo hicho kilichofanyika. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais na namtia moyo aendelee kufanya kazi. Aelewe ya kwamba watu wote hawatakubaliana na anachokifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimtie moyo sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Kazi yake ni ngumu. Anafanya kazi ngumu sana ambayo siyo rahisi kueleweka. Ila tukumbuke Henry Ford alipotengeneza gari, watu walikuwa wamezoea farasi, wakakataa gari, lakini baadaye walipozoea gari, wakakataa farasi. Kwa hiyo, yapo mambo ambayo siyo lazima sisi wote tukubali, ilimradi lina maslahi ya Taifa, ilimradi jambo hilo siyo maslahi ya mtu binafsi, lifanywe hata kama wengine hawakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nashukuru sana kwa jimbo langu. Jimbo langu mimi Shigongo Eric la Buchosa limepiga hatua kubwa ndani ya muda mfupi kuliko miaka kumi yote iliyopita. Barabara zinapitika, miradi mingi ya maji, tumejenga madarasa, tuna Chuo cha VETA, tuna kivuko kipya cha kwenda Kome cha shilingi bilioni nane, haijapata kutokea. Nisipomsifia Rais wangu, nimsifie nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, niwaambie kitu kimoja, hakuna jambo baya kama kumsifia mtu sifa za uongo. Ni sawa na mimi uniambie nina six packs na wakati nina kitambi, unapunguza heshima yako. Niseme ukweli, ukisifiwa sifa za uongo unamdharau anayekupa sifa. Nami natoa sifa hizi kwa Rais kwa sababu ni mambo ya ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niendelee. Nachangia mambo makubwa mawili tu. La kwanza, kukua kwa Taifa letu. Tanzania nchi yangu ninayoipenda inakua. Ni rahisi sana sasa hivi mtu kuzunguka huko akafanya mikutano yake ya hadhara, akawaaminisha watoto wetu kwamba hakuna kinachoendelea na watu wakaamini. Mimi ni wazamani kidogo, nimeshuhudia Marais wengi, lakini ngoja nitoe takwimu chache hapa kuonesha kwamba Taifa letu linakuwa ili kusudi tutembee kifua mbele, tusitembee kwa unyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1961 tulipopata uhuru barabara za lami zilikuwa kilometa 1,300. Leo ninavyoongea tuna kilometa 14,000. Mwaka 1961 life expectancy, umri wa Mtanzania kuishi ilikuwa miaka 38, leo tuna miaka 68. Tulikuwa tuna chuo chetu kimoja, leo tuna vyuo vikuu 47. Tulikuwa na hospitali za wilaya na mikoa 96, leo 1,030. Tulikuwa na vituo vya afya 22 nchi nzima, leo tuna vituo vya afya 4,030. Tulikuwa na zahanati 1,332 leo tuna zahanati 7,458. This country is growing. Hii nchi inakua. Tufike mahali tukubali kwamba nchi yetu inakua, asije mtu hapa kutuaminisha kwamba hakuna kinachoendelea, that is a lie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua tunaweza kutofautiana kuhusu speed, wengine wanaona tunaenda polepole, lakini this country is growing. Watoto wetu wanaonisikiliza huko nje, wasidanganywe na mtu yoyote, nchi yetu inakua tuendelee kufanya kazi, muda siyo mrefu tutakamata uchumi wa Afrika na hatimaye kuheshimiwa zaidi ya tunavyoheshimika hivi sasa. Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni umaskini wa kipato. Mimi nimetoka katika familia maskini sana, na kwa kweli nauchukia sana umaskini kwa sababu ulinitesa sana nikiwa mtoto. Mungu kanitoa huko, lakini mimi peke yangu kutoka siyo kwamba umeisha, kuna watu nimewaacha wengi huko nyuma. Ndiyo maana napambana na umaskini kila siku. Kwa miaka 23 nimezunguka nchi hii kwenye vyuo, kwenye Makanisa, napambana na umaskini, kuwaelimisha watu mbinu za kutoka kwenye umaskini. Nimeandika mpaka vitabu kwa sababu siupendi umaskini practically kwa sababu una mateso. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili ni Tajiri. Tanzania nchi yangu ni tajiri. Ngoja nikupe data kidogo. Tanzania kwa makaa ya mawe ni ya 87 duniani; Tanzania kwa gesi ni ya 82 duniani; Tanzania kwa Helium ni ya kwanza duniani; Tanzania kwa dhahabu ni ya 19 duniani; Tanzania nchi yangu kwa almasi, ni nchi ya 17. Nchi hii tajiri, hatutakiwi kuendelea na umaskini wa kipato. Ilitakiwa tuwasaidie watu wetu kubadilisha utajiri huu uweze kuwa pesa na maisha ya watu yabadilike. Tunahitaji pesa kwenye mifuko ya watu wetu. Unapowaambia Watanzania wanajilipia shilingi bilioni 85, wakati mchele ni shilingi 3,500 hawaelewi. Tufanye nini? Muda ni mchache. Tufanye nini kuwasaidia Watanzania wawe na kipato? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza, let us invest in agriculture. Nataka kumsifia sana Mheshimiwa Rais wangu, kumsifia Mheshimiwa wangu Waziri Bashe kwa jinsi ambavyo Tanzania imeamua kuwekeza kwenye kilimo. Ni kilimo pekee yake kitawasaidia Watanzania kutoka kwenye umaskini wa kipato. Naomba tuwekeze kwenye mbegu, tuwekeze kwenye masoko, tuwekeze kwenye teknolojia, watu wetu waweze kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ya kwamba, tuwekeze kwenye kilimo hasa cha mazao ya chakula (food crops). Unaweza ukalima maparachichi, it is okay, ukilima pamba it is okay, ukalima chai it is okay, lakini Wazungu wanaweza wakaweka sera zao za ushoga hapa, ukakataa sera zao wakasema unajua maparachichi ya Tanzania yana Sodium Bicarbonate, wakasema hatuyanunui, lakini tukilima chakula na tukawa ni soko la chakula cha Afrika nzima, nataka kuwahakikishieni, hatuna sababu ya kufunga mipaka. Kwa nini tusiwe soko la chakula la Afrika nzima, watu waje wanunue chakula Tanzania? Tukifanya hivyo, watu wetu watakuwa na pesa mfukoni. Agriculture. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili la muhimu sana, nataka kuona Watanzania wazawa wanawezeshwa kiuchumi. Bajeti ya mwaka huu, shilingi trilioni 44, natamani fedha hizi zibaki kwa vijana wa Kitanzania. Nilishaongea mara nyingi, Watanzania wamechoka kuona wageni wakija hapa wanatajirika wao wanaendelea kubaki maskini, that is not right. Siwezi kwenda India leo nikapewa tenda ya kuchapa vitabu vya sekondari. That is a lie, lakini Wahindi watakuja hapa watachapa vitabu vya watoto wetu wa shule. Kwa nini? Nataka kuona wazawa wanawezeshwa kushikiklia uchumi wa nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo Sheria ya Manunuzi. Hebu sikiliza sasa uone. Sheria ya Manunuzi ambayo nailalamikia kila siku, inasema eti kwenye ku-supply tender ikifika shilingi bilioni moja, hiyo tender inabadilika inakuwa international. Hebu ona sheria hiyo. Mmetunga humu humu ndani kwamba tender ikifika Shilingi bilioni moja, inaenda international. Eti mimi nipambane na Mturuki, nipambane na Mchina, nipambane na Mwingireza, haiwezekani. Nataka hiyo sheria ibadilishwe. Watanzania hawawezi kushindana na watu wenye mikopo ya dola mbili, sisi tuna mikopo ya dola 22 ya CRBD. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie.

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa, sekunde 30.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kuisaidia nchi yetu tuwasaidie Watanzania washike uchumi wa nchi yao. Mambo ya kuwa mashuhuda, wamechoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie jambo la mwisho kabisa kwa upendeleo ulionipa. Namwomba Mheshimiwa Waziri apanue wigo wa kodi. Naomba nikushauri, kutegemea kodi pekee yake kama chanzo cha mapato, haiwezekani. Nataka uwezeshe sekta zetu kwa pesa za kodi ili sekta ziingize fedha kwenye pato la Taifa. Kwa mfano,…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Eric.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)