Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hii Bajeti Kuu pamoja na Mpango wa Taifa. Kwa kuanza tu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Wizara yake, lakini shukrani za dhati kwa Mama Samia kwa suala ambalo tumelipigia kelele, lile suala la bureau de change ambalo wamelifanyia kazi nimeona kwenye ukurasa wa 53 na 54 wa Hotuba ya Bajeti Kuu, lakini inaonekana wamefanyia kazi Arusha peke yake na ameahidi kuendelea kuondoa au kurekebisha vile vigezo ili na maeneo mengine basi waweze kufanya hii biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaipongeza Serikali kwa namna inavyoendelea kusimamia uchumi wetu, uchumi wetu umekua sasa karibu bilioni 85 ikilinganishwa na bilioni 69, ni hatua kubwa na mengine mazuri yanakuja mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mapendekezo maeneo matatu kabla sijaendelea na maeneo yale ambayo nafikiria kuyachangia. Kwenye eneo la mazao nimeielewe vizuri sana nia ya Mheshimiwa Waziri wetu wa Kilimo Mheshimiwa Bashe, nia yake ni njema kabisa na tukimsikiliza tutaona haya ambayo anakusudia ili mazao haya yaje kuonekana kwenye export zetu kwa maana ya thamani zake. Niendelee kumshauri yale masoko ya ukanda huu wa pembezoni wayawekee nguvu sasa, ina maana upande ule wa Namanga upande huu wa kila maeneo yenye mpaka ambayo kunapitisha mazao waimarishe yale masoko na kule Kilimanjaro tulikuwa tuna eneo lile la Lokolova ili haya mambo ambayo ambayo amekusudia ambayo Mheshimiwa Rais amekusudia yaweze kufanyika kwa uzuri zaidi bila kuleta usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa pili ni kwenye kodi inayotaka kuwekwa kwenye cement. Mimi nadhani ukiangalia sensa yetu inaonesha uwiano wa watu na umiliki wa makazi, kwa sababu kwenye dodoso kulikuwa kuna umiliki wa makazi pale, sasa na makazi yaliyoandikwa pale ni makazi ya aina gani, sidhani tumefikia mahali pa kuweka kodi kwenye cement, watu bado wanalala nyumba za tembe ni viizuri tuangalie chanzo kingine hii ya cement tena ilitakiwa tu-subsidies ili watu waendelee kujenga nyumba tutoke kwenye nyumba za Tembe tuwe tunalala kwenye nyumba za cement. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mafuta pia natoa ushauri, sioni kuweka shilingi 100 kwa wote inaleta tija. Hebu Wizara ikae na wataalam waangalie ni namna gani tunaweza tukawa na bei uniform ya mafuta nchi nzima. Kwa sababu kule Kigoma wanalipa bei ghali sana mafuta na wanakipato kidogo, wakati Dar es Salaam wanalipa kidogo sana na Tanga kwa sababu wapo karibu na bahari. Ni vizuri tuangalie uwezekano wa kuzifufua zile depot za maeneo kule Moshi kulikuwa kuna depot, sijui huko Mwanza depot na Serikali iangalie uwezekano wa kuisimamia tuwe na bei moja kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama CocaCola na kampuni za maji wanaweza, kwamba nchi nzima kuna bei moja na kama bei ya usafiri ndiyo inaleta shida Mheshimiwa Bashe alitoa zile pikipiki kwa Maafisa Ugani zimewekwa GPS zote tunaweza kufunga magari yote yanayosafirisha mafuta GPS kuhakikisha kwamba ile gharama haiwezi kutuletea utofauti mkubwa wa bei, tukawa na bei moja ya mafuta nchi nzima ninaamini linawezekana badala ya kuongeza shilingi 100 kwa watu wote wakati watu wa Dar es Salaam mafuta ni bei rahisi, huku Kigoma Mikoani Arusha huko tunapata mafuta ni bei ya juu. Kwa hiyo, nimesema hayo masuala matatu nitoe ushauri ili tuweze kusonga mbele tuone namna ambavyo tunaweza kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la utalii. Ninakumbuka kwenye semina ambayo tulifapewa na Wizara ya Utalii walisema Tanzania inategemea maliasili tu kwenye utalii. Pamoja na maliasili ambayo inaleta mpaka conflict kwa baadhi ya maeneo kwa maana ya wakulima sijui na wafugaji na maeneo ya hifadhi maana yake bado tuna nafasi ya kuweka vivutio ambavyo ni man-made. Dubai vivutio vyake asilimia kubwa karibu vyote ni man-made na wanapata watalii milioni 14, 16 kwa mwaka. Sisi na hii Maliasili pamoja na zile changamoto ambazo zimetajwa tunapata 1,400,000 ambayo ndiyo the highest tumepata mwaka 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kwa yale maeneo ambayo tunaweza kuongeza vivutio ambavyo ni man-made ambavyo havina madhara negative kwa jamii yawekwe na ndipo hapo niliposema kwa mfano suala la cable car kuna argument kwamba haina madhara na kuna argument kwamba ina madhara, msimamo wangu na msimamo wa wananchi ni kwamba kama cable car haipunguzi mapato ya Serikali, haiharibu mazingira, haipunguzi ajira, haina madhara negatively kwa mapato ya Serikali wanaihitaji ili iongeze mapato. Kwa hiyo, kama negative impact hazipo tunaihitaji lakini kama zipo basi hilo tunaona haina tija kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kidogo ambacho ninadhani Wizara inatakiwa ikifanyie kazi na ni Wizara ya Viwanda na Biashara, inaingia Wizara ya Afya tuliondoa TFDA tukaweka TMDA lakini aspect ya chakula hasa kwenye import na export TBS hawawezi kuifanya lakini ukiacha TBS hawawezi kuifanya pia siyo international practice, ni vizuri suala dogo kama hili ni suala la uamuzi leteni sheria hapa turudishe TFDA watu wakiweka miguu chini nje kwenye vyakula tunavyo-export hatuwezi kabisa kusimama kwa sababu hatuna TFDA. TMDA hifanyi ile kazi ilikuwa inafanya TFDA na badala yake TBS pia hawawezi kupima vitu kama maziwa haya ya watoto hizi formula, kwa hiyo tufanye tu mara moja siyo kila kitu mpaka Rais aseme ndiyo tufanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mitumba ya nguo viatu ambavyo ni second hand kwenye nchi yetu. Kwa hali ya sasa mitumba inayokuja Tanzania ni ya hali ya chini sana, kwanza wale wafanyabiashara wanapoteza fedha kwa sababu wanafungua mtumba wanakuta nguo zinazouzika ni chache lakini wananchi wetu wananunua nguo nza mitumba za bei kubwa ambazo hazina ubora. Kuna watu wananunua mitumba Kenya wanaileta mpaka Tanzania Mikoa mingi tu, tumeona wana-advertise ni mtumba wa Kenya una ubora zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu katika usimamizi wa eneo hili, hebu Serikali iende iangalie namna ya kulisimamia ikiwa ni pamoja na hizo hatua ambazo mnazifikiria mbele za kuondoa hii, lakini wakati mnai-ban mitumba mhakikishe kuna nguo zinazotoka kwenye hizi nchi zinazo-import zina quality, kwa sababu sasa hivi tuna-import vitu kutoka baadhi ya nchi, zikija hapa tunaambiwa ni Ngozi lakini vikivaliwa siku mbili vimechanika huwezi kulinganisha na vile vya mtumba ambavyo vipo, kwa hiyo hatua ya ku-ban mitumba iangaliwe sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Moshi kuna Kiwanda cha Karanga Leather. Serikali ime-invest billions of moneys zaidi ya bilioni mia moja lakini Serikali haijaweza kusimamia kile kiwanda, kiwanda kinategemea kiajiri watu 10,000 wale wa moja kwa moja 3,000 lakini mpaka sasa hivi kimeajiri watu 250 na hela imeenda pale. Rais kila siku anasema mumwambie Mashirika na Makampuni ya Serikali ambayo hayafanyi vizuri sasa tusiendelee kutengeneza matatizo, kama kuna hao Wabia waletwe waingie kwenye kile Kiwanda cha leather pale Moshi kiweze kuleta ajira, tulete Pato la Taifa na kodi iweze kukusanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kodi ambayo bado sijaweza kupata mantiki yake, kodi tunazotoza kwenye magari chakavu. Ukiangalia dumping ya kwetu haiakisi kusudio la kuanzishwa kwake. Maana ya dumping ilikuwa magari ambayo ni ya zamani sana yasiingie nchini na kwa bahati mbaya dumping yetu ina-charge percentage ya value. Sasa gari linavyozidi kuwa la zamani zaidi, value yake kule inazidi kuwa ndogo kwa hiyo hata kukata percentage maana yake gari ya zamani utaikuta bei ya kufika hapa ni rahisi kuliko gari ya mwaka jana. Hebu tuangalie tutafute dumping ambayo itasaidia magari ya karibuni yawe na bei nafuu kuliko magari ya zamani sana ili ilete tija. Kwa hiyo, magari hapa Tanzania yamekuwa aghari bila sababu na maana yake ni kwamba hatumsaidii Mtanzania, lakini gari lina faida lina mafuta, kuna mambo ya gereji, kuna udereva hapo leseni zinakatwa, kwa hiyo ni vizuri mliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)