Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia bajeti hii ya Serikali. Kwanza nianze na kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kazi nyingi zinazofanyika vizuri katika nchi yetu. Sisi kule watu wa Mpwapwa tumepata miradi mingi sana, haijawahi kutokea katika historia ya jimbo letu. Tumepata miradi upande wa barabara, tumejenga madaraja ambayo yalikuwa yanasumbua kwa kipindi cha miaka mingi. Vilevile tumepata madarasa mengi kama ambavyo Wabunge wengine wamepata, na hivi karibuni tumepata shilingi zaidi ya bilioni 735 kwa ajili ya upanuzi wa shule yetu ya wasichana pale Mpwapwa Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunapanua shule yetu ya wavulana Mpwapwa Sekondari, tumepata milioni 295, tumeendelea, tumepata vituo vya afya. Kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa ajili ya juhudi hizi ambazo amezifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nimpongeze sana Waziri wa Fedha. Bajeti hii amegusa karibu maeneo mengi sana yanayohusu wananchi, nawapongeza sana Waziri, Naibu Waziri na timu yake nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na bajeti nzuri kama hii mimi naona ni jambo moja lakini utekelezaji wake ni jambo lingine. Ninataka kumshauri Waziri waitekeleze katika mapana yake kama ambavyo wameileta. Haya mengine tuliokuwa na shida kwamba bajeti inakuwa nzuri lakini utekelezaji wake unakuwa haufikii malengo ambayo yale tulikuwa tumekusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuchangia upande wa ukusanyaji wa kodi kupitia ETS au Electronic Tax Stamps. Utaratibu huu mimi nauunga mkono sana uendelee kutumika kama ambavyo umekuwa ukitumika kwa kuwa unatusaidia kuongeza mapato, stamp hizi zinabandikwa kwenye bidhaa zinazozalishwa. Kwa hiyo kwanza tutajua ni bidhaa kiasi gani zilizozalishwa na inakuwa rahisi sasa kukata kodi. Ingawa kuna malalamiko machache yanaendelea dhidi ya mkandarasi anayetekeleza mradi huu. Naishauri Serikali mkae na huyu mkandarasi muweze ku-resolve matatizo yote ambayo yameonekana katika utekelezaji wake lakini utaratibu huu nauunga mkono ningeshauri Serikali iendelee naoi li kuongeza mapato ya Serikali yetu hivyo kufadhili miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni upande wa kilimo. Kilimo kama walivyosema wengine ndio uti wa mgongo, na tunajua kabisa zaidi ya asilimia 65 ya ajira za nchi hii zinapatikana kutokana na kilimo. Nimeona Wizara ya Kilimo; niwapongeze sana; wamekuja na mkakati wa kuhakikisha kwamba sasa tunaondokana na kilimo cha kutegemea sasa tutakuwa tunafanya kilimo cha umwagiliaji. Mabwawa yanajengwa sehemu nyingi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nishukuru kwa sababu kule Mpwapwa tuna bwawa kubwa lenye thamani ya shilingi bilioni 27.9 ni bwawa kubwa ambalo naamini litaleta ukombozi mkubwa sana kwa wananchi wa Mpwapwa. Sasa kitu ambacho ningeomba Serikali izingatie sana hapa ni kutengeneza miundimbinu tunaweza kuwa na maji mengi sana lakini kama miundombinu ya umwagiliaji haipo bado tutaendelea kukutana na shida nyingi za uhakika wa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kilimo hicho niwapongeze sana ile mamlaka ya kuhifadhi chakula NFRA mwaka huu kulikuwa na shida ya chakula katika maeneo mengi katika nchi yetu ni pamoja na Jimbo langu la Mpwapwa. Walifanya vizuri sana kutusaidia. Wakati wanaanza kusambaza chakula bei ya debe moja la mahindi ilikuwa imefikia shilingi 25,000 lakini wao walipoleta mahindi yakaanza kuuzwa kwa shilingi 16,000. Ulikuwa ni ukombozi mkubwa sana kwa wananchi lakini shida ambayo niliiona ni kwamba hawakuwa na uwezo wa kufika maeneo yote ya Wilaya ya Mpwapwa kwa sababu ya nguvu ndogo ya bajeti ama idadi ndogo ya wafanyakazi. Kwa hiyo, ningeomba sana Serikali izingatie hili jambo iwaongezee nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yako Mheshimiwa Waziri umesema mna mpango wa kununua tani 400,000. Mimi nadhani hizo tani ni ndogo kwa sababu ya uhaba wa mvua iliyotokea mwaka huu bado tunafikiria kwamba kutakuwa na shida ya chakula mwaka unaokuja. Kwa hiyo hawa watu wawezeshwe wawe na chakula cha kutosha. Zinunuliwe hata tani 700,000 ili ikiwezekana basi shida hii ya chakula itakapotokea Serikali iwe na uwezo wa kupambana na hii shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni kwa upande wa ardhi. Ardhi ni jambo moja kubwa sana ambalo linaleta maendeleo kwa watu wetu. Serikali mmezungumza habari ya kupunguza kodi na tozo mbalimbali kwa wamiliki wa ardhi na mimi naungana nao hilo jambo ni zuri ili watu wengi waweze ku-afford kumiliki ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo bado hatujafanya vizuri kwa upande wetu wa Serikali ni kupima ardhi kwenye miji ya wilaya na miji ambayo inakuwa kwa kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu akipimiwa ardhi yake akawa na hati ya kumiliki ardhi kwanza faida yake ni kwamba miji itajengwa kulingana na mipango miji. Kwa hiyo upimaji wa ardhi kwa kawaida unapendezesha miji, miji inaonekana imejengwa vizuri. Faida ya pili yule mwenye kumiliki ardhi ambaye ana hati ya kumiliki ardhi anaweza kuwa na access ya kupata mikopo kwenye vyombo vyetu vya fedha, na akishapata mikopo itamsaidia kujitafutia biashara na kufanya ujasiriamali. Kwa hiyo itakuwa ni ukombozi mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo watu wengi hawawezi kupata mikopo katika vyombo vya fedha kwa sababu tu hawana dhamana na dhamana kubwa ambayo inatakiwa kwenye vyombo vingi vya fedha ni umiliki wa ardhi, yaani mtu lazima uwe na hati ya ardhi. Kwa hiyo ningeomba sana maelezo yaliyoelezwa kwenye bajeti ni mazuri na namwomba Mheshimiwa Waziri jambo hili Serikali ilitilie maanani. Watu wapimiwe ardhi waweze kumilikishwa ardhi ili waweze kufanya maendeleo ya maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia nimeona kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia mpango huu wa kunusuru kaya maskini (TASAF). Mpango huu ni mzuri na umeleta tija katika maeneo mengi ya nchi yetu, na kwamba sasa pia waweza kutambua maeneo kama 186 ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, ambalo ni jambo zuri. Malalamiko yangu, niliwahi kusema hata huko nyuma, utaratibu wa kutambua hizo kaya maskini bado hauko sahihi. Katika Jimbo langu la Mpwapwa wako watu ambao mimi nawajua ni maskini kabisa wana sifa zote lakini hawajaingia kwenye huu mpango wamekuwa wakilalamika. Kwa hiyo maana yake nni kwamba kuna kasoro katika utaratibu mzima wa kutambua nani ana sifa, kaya ipi ina sifa ya kuingia kwenye huo mpango na ipi haina sifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii imefanywa na watendaji wachache wasio waaminifu wamekwenda wamechukua watu wasio na sifa kuingia kwenye huu mpango wamewaingiza wameacha watu ambao kwa kweli wana sifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imefanywa na watendaji wachache wasio waaminifu, wamekwenda wamechukua watu wasio na sifa, wamewaingiza kwenye huu mpango, wamewaacha watu ambao kwa kweli wana sifa. Kwa hiyo Serikali ningeomba pia tunapotekeleza bajeti hii ya 2023/2024, Mpango huu wa TASAF ni mpango mzuri, kama hatuwezi kuusimamia vizuri tutanufaisha watu ambao hawastahili, tutaacha wale wanaostahili. Matokeo yake, lengo na madhumuni ya mpango huu yatakuwa hayajatimia kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo pia ningependa nichangie ni kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia nadhani amevunja rekodi ya kutoa fedha nyingi sana kuliko wakati mwingine wowote ambazo zimeenda katika ngazi zote za Serikali. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, lakini lengo lake na madhumuni yake bila shaka angetarajia kuona ustawi wa wananchi wake, angetarajia kuona yale ambayo tumekusudia, yale ambayo yeye mwenyewe anawaza mpaka anapeleka hizo fedha yanatokea katika uhalisia wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hii miradi mingi ambayo Mheshimiwa Rais ameipeleka katika maeneo yote ama haijakamilika ama imekamilika, lakini iko chini ya kiwango, kama ni majengo hayana ubora, ni kwa sababu ya usimamizi hafifu. Naomba sana Mheshimiwa Waziri kama msimamizi wa bajeti, Waziri wa Fedha, fedha hizi anapozipeleka kwenye maeneo mbalimbali kuwe na mpango mahususi wa kusimamia fedha hizi. Maeneo mengi fedha hizi zinachezewa vibaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ujenzi wa madarasa, unakuta hayako kwenye kiwango. Fedha ile ambayo wengine wanakamilisha kabisa kwa kiwango bora, lakini wengine hawakamilishi kabisa. Vituo vya afya, ukifuatilia utakuta vingine havijakamilika kabisa, fedha ni ile ile ambayo wengine wamekamilisha. Hii ni kwa sababu ya usimamizi mbovu. Haitakuwa na maana yoyote kama Mheshimiwa Rais atatafuta fedha, ataleta katika maeneo ya wananchi akitarajia kujenga hospitali, kujenga zahanati, kujenga shule imara na bora, halafu yote hayo yasitokee. Pia wananchi wanatarajia sana kuona kwamba mambo yao yanaenda vizuri, kama ni miradi inaenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tusimamie fedha za Serikali...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa George Malima, ahsante sana kwa mchango wako. (Makofi)

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)