Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema nami niweze kuchangia Wizara hii ya Fedha kwa maana ya Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa Rais mwanamke wa kwanza East Africa. Ninampongeza sana hiyo ni heshima kubwa sana kwetu lakini pia amekuwa Makamu wa Rais wa kwanza Tanzania. Pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kuwa Dkt. Tulia Ackson agombee nafasi ya Urais IPU. Pongezi nyingi sana kwako Dkt. Tulia namna ambavyo unakwenda kugombea hii nafasi tunakuombea sana kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu atasimama na wewe atakwenda kutimiza haja ya moyo wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa. Alifanya kazi kubwa sana pale Dar es Salaam, alisimama kwa muda mrefu sana akiongea na wafanyabiashara. Yote hiyo ni kwa ajili ya kuweka nchi sawa sawa, kutengeneza amani, upendo na mshikamano. Alituliza mioyo ya wafanyabiashara wa Tanzania. Pongezi nyingi sana kwako Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa Mwenyezi Mungu aendelee kuwa nawe katika majukumu yako popote unapokuwa awe pamoja na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaingia kuchangia kwenye Mpango huu wa Serikali. Nipongeze TRA, TRA wanafanya kazi nzuri ya kukusanya kodi ndipo ambapo maeneo mengi wanatimiza malengo yao ni kwa sababu ya utiifu na nidhamu waliyonayo wafanyabiashara kuchangia ama kulipa kodi kwa sababu wanajua kodi ndiyo maendeleo ya Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani wafanyabiashara hawa wanapata changamoto hasa pale wanapokuwa wamejipanga na kujiandaa kwa ajili ya kwenda kulipa kodi kuna tatizo kubwa la mtandao kwa maana ya control number. Control number ni tatizo kubwa. Serikali kwa maana ya TRA wanakuwa na operation ya kukamata vyombo vya moto. Utakuta wamekamata bajaji, magari na wafanyabiashara wale wako tayari kulipa lakini anafika TRA mtandao unasumbua uko chini, wanakwama kulipa kwa wakati lakini bado wanaendelea kushikiliwa vyombo vyao kiasi kwamba wanashindwa kuendelea kufanya biashara kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na wakati huo kwa wafanyabiashara hawa wadogo wa bajaji inawezekana kabisa amekopa hiyo fedha kwa ajili ya kwenda kulipa. Sasa pale akikwama kulipa mtandao uko chini, control number inakwama kutolewa ndipo ambapo shida inapoanzia. Anauhitaji kwa ajili ya kutumia fedha kwa ajili ya familia yake lakini inashindikana sijajua, tatizo liko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Jeshi la Polisi, Jeshi la Polisi akikamata gari akiona lina makosa, control number inatoka hapo hapo kwa kosa alilonalo anatakiwa alipie lakini nikiangalia na tukiangalia Watanzania kwenye Wizara hii ndiyo wenye kihenge, ndiyo mmeshika fedha zote za nchi. Mnashindwa nini kuboresha utaratibu TRA wa control number kutoka kwa wakati ili Watanzania walipe wakaendelee kufanya majukumu yao? Ni nini kinakwamisha hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mbunge wa Wanawake wa Mkoa wa Mbeya. Wakati fulani napata simu za malalamiko hata nje ya Wananchi wa Mkoa wa Mbeya. Nataka nitoe jambo hili ambalo nilipigiwa simu kutoka Dar es Salaam ni kero za wananchi. TRA wanakuwa na operation, siku moja walisimama TAZARA pale wakakamata gari ya mfanyabiashara, ile gari ilikuwa inaenda kupakia mzigo kwa bahati mbaya sana tajiri alikuwa hana taarifa kwamba ile gari inadaiwa kumbe kuna makosa ameyasababisha dereva ambaye wakati huo hakuwa kwenye hiyo gari. Tajiri yuko tayari kulipa hiyo fedha, anamwambia kwamba natuma hiyo fedha ilipwe sasa hivi muachie gari ikafanye kazi, TRA wanamwambia wanasema, “Hiyo gari lazima iende yard Tabata, ikipaki Tabata urudi hapa uende Vingunguti ndipo ukalipie kodi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa muda wa nani, kwa gharama za nani na kule yard inatakiwa ikalipe kodi? Sasa mfanyabiashara huyu anachelewesha muda, yuko tayari kulipa na pale siyo majembe wapo ni wahusika wa TRA, maafisa wa TRA wako pale wanasema hawawezi kutoa control number kwa wakati, tatizo linakuwa wapi? Mbona Jeshi la Polisi linafanya haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi wenye kihenge ambao ndiyo mnashika fedha za nchi kunakuwa na tatizo gani kulipa, kutoa control number papo kwa papo ili kazi zingine ziendelee? Nashauri sana Serikali mlitazame hili la ukusanyaji kodi, yamkini mapato mengine yanapotea kwa sababu ya kutokupokea fedha kwa wakati, kutokupokea mapato kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo kidogo imekuwa changamoto. Wafanyabiashara hawa ni wasikivu kwa kulipa kodi. Kuna tatizo moja, kaka yangu pale Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri sana. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu anafanya kazi nzuri sana, kuna kipengele kimoja kaka yangu ninaomba sana utazame hili. Kuna hii service levy; service levy inakwenda kukata mtaji wa mfanyabiashara. Wafanyabiashara hawakatai kulipa service levy kwa sababu wanajua kodi ndiyo kila kitu. Ninaomba sana service levy mfanyabiashara analipa 0.3. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi, tunaomba yaani ingefaa angalau basi iwe 0.1 kulipa ni ndani ya Wizara yako hizo fedha zinakusanywa zinakwenda zote kwenye kihenge kimoja. Mkiliangalia hili kwa undani tunaomba msaidie hawa wafanyabiashara najua hili liko ndani ya TAMISEMI ndani ya upande wa leseni lakini hili jambo kwa sababu ni Serikali na huu ni mchango wa Bajeti ninaomba mkalitazame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba amefanya kazi nzuri sana pale alipokuwa akisoma na ipo kwenye maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amewaonea huruma sana, amewajali sana wafanyabiashara ameamuru wasifungiwe maduka yao badala yake wanatakiwa waelimishwe ili waende kulipa kodi. Kwa sababu mfanyabiashara huyu akifungiwa duka lake atatafuta fedha wapi za kwenda kulipa kodi.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeliona hili kwa undani sana.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina taarifa hapa.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea nimekatishwa kidogo hapa maana mimi nilikuwa naendelea kufafanua namna gani umewatendea haki wafanyabiashara wa Tanzania. Mheshimiwa Mwigulu Nchemba umewatendea haki sana. Na mimi kwa niaba ya watanzania, wafanyabiashara ninakupongeza na kukushukuru kwamba hili umefanya vizuri hasa wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya wanakwenda kufanya kazi zao bila kutishwatishwa bila vitisho…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, na muda wako umekwisha.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa muda ulionipatia lakini niseme kwamba Mungu abariki sana mpango huu, na ninaunga mkono hoja, ahsante sana, nakushukuru. (Makofi)