Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Mwanakhamis Kassim Said

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Magomeni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Kuna msanii Zanzibar alisema, “Mungu akitaka kukupa hakuletei barua, hukupa usingizini pasipo mwenyewe kujua.” Kuna msanii mwingine akasema, “Mpewa hapokonyeki, aliyepewa kapewa.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nikasema hivi? Nafasi ya uongozi ikiwemo Rais na viongozi wengine nafasi hizi hupangwa na Allah Subhannah Wataala. Mwenyezi Mungu kama hataki uwe Rais basi utavaa makoti kila siku ukajitazama kwenye vioo mimi nitakuwa Rais lakini huwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. Samia Suluhu Hassan cheo hichi alitangazwa na Mwenyezi Mungu ndiye aliyempa. Vyeo hivi kuna leo kutenda kuna kesho kuulizwa lakini Mheshimiwa Samia ni mcha Mungu. Mheshimiwa Samia anafanya mambo makubwa kuwatumikia Watanzania na Watanzania wote ni mashahidi na sisi Wabunge ni mashahidi. Siku zote binadamu tunapofanya mazuri tunakuwa hatusifii na lile zuri halisifiwi baya ndiyo linasifiwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamzungumza Dkt. Samia tunampigia makofi sana muda wote nafikiri Wabunge wote wanamzungumza Mama Dkt. Samia kwa imani yao na imani ya Mama Dkt. Samia anayafanya lakini Mheshimiwa Dkt. Samia ana jeshi lake. Ana jeshi linalomsaidia kazi ya kumpongeza Mama Dkt. Samia na miaka miwili aliyoifanyia kazi na jeshi hili ni Mawaziri wetu na Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu na Wakurugenzi. Hilo ndiyo jeshi la Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyonge mnyongeni lakini Mawaziri wetu wanapambana. Wanafanya kazi kubwa sana kuwafanyia Watanzania na kazi hizi zinaonekana. Kwa nini tusiwapongeze, kwa nini tusiwaombee? Mawaziri hawa wakiongozwa na Kamanda wao Waziri Mkuu kwa kweli wanastahili sifa zote. Tumpigieni makofi Rais wetu lakini na Mawaziri wetu wanafanya kazi kubwa sana, wanastahili sifa. Kuna jeshi la ardhini na jeshi la angani. Naibu Mawaziri ni majeshi wa ardhini, Mawaziri wenyewe ni majeshi ya angani wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliposoma Bajeti yake aliisoma kwa madaha lakini kwa uelewa mkubwa na tulimuelewa tukamfahamu hata Watanzania waliifahamu Bajeti hii. Sasa basi kazi iliyobakia jeshi la Mama Samia wakaitekeleze bajeti hii ifanye kazi kwa weledi zaidi. Miradi hii ikakamilike fedha zifike kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nimuombe Ndugu yangu Comrade Waziri wa Fedha kwa kweli kwenye makusanyo huko kumechafuka sana bado kazi hii hatujaifanyia kazi. Tuendelee kupambana na ukusanyaji wa kodi. Tunapokwenda kukusanya kodi, wale tunaowafuata ni binadamu na binadamu siku zote ana mbinu nyingi. Kwa hivyo twende kwa nasaha, kwa maridhiano tukawashauri lakini tuwaambie. Tusiende kwa vishindo kuwatukana, kupambana nao itakuwa hatufanikiwi. Letu tunalotaka itakuwa hatufanikiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sehemu za makusanyo rushwa ni nyingi, kunanuka rushwa. Udanganyifu ni mwingi, unakwenda kununua kitu anakwambia unataka cha shilingi 100,000 ukimwambia nakitaka nipe risiti anakwambia basi shilingi 150,000, itakuwa hatufiki. Mimi naomba jeshi la Mama Samia tushirikiane na Wabunge tukafanye kazi ya makusanyo jamani ndiyo tutapata maji, barabara na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite moja kwa moja suala la Muungano. Viongozi wetu Hayati Karume na Hayati Nyerere walipoungana Muungano huu waliungana kwa makaratasi wakatiliana saini lakini hawakuridhika, ukachukuliwa udongo wa Zanzibar na udongo wa Tanganyika ukaja ukachanganywa. Leo udongo ule nadhani hakuna Mtanzania wala mzungu atakayekuja kuubagua udongo ule kwa muda huu uliofika kwa awamu hii, sisi hatukuungana tena kwa karatasi wala kwa udongo, tumeungana kwa damu. Sisi tumeshachanganya damu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uduvi unaupekecha pekecha Muungano huu lakini tunawaambia ole wao jeshi litakuwa ni la Mama Samia lakini wanawake tu ndiyo tutakaopambana nao. Hatuwezi ukavunjika Muungano huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite moja kwa moja kwenye maliasili. Wabunge wengi wanawake, wanaume wanalia kuhusu tembo. Tembo huyu anatupatia faida, tunapata fedha za kigeni lakini tembo hii pia ni dawa kwa binadamu. Niiombe Serikali tembo sasa hivi anaua watu ni hatari. Tusiachie hii tembo ikawa inaua watu ni hatari na hatuwezi kuwaua tembo hawa kwa sababu tunapata faida nyingi sana. Nadhani hili janga liwe la Kitaifa wa kuisimamia hii tembo isiue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la maadili ya nchi yetu. Kuna watu kama ni kutoka ughaibuni, kama ni kutoka Afrika, kama Ulaya wamekuwa wanawadhalilisha viongozi wetu wanawatukana kwenye mitandao. Tunasema hii haikubaliki wala hatukubali na tunashangaa leo mwanamke utachukua simu utamtukana mwanamke mwenzio, iweje na lipi unalomtukania? Kama uko Ulaya basi shuka uje huku Afrika tukutane uso kwa uso tutukanane sisi na wewe na kama wewe unatukana uko Ulaya hayo matusi unayoyatukana basi yawe yako mwenyewe siyo ya kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)