Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi nichangie katika Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kurudisha Tume ya Mipango ambayo kwa kweli tumekuwa tukiipigania kwamba irudi na iweze kufanya kazi yake sawasawa. Ukiangalia katika mpango wa maendeleo wa tatu wa 2022/2023 ulitengewa trilioni 15.0 ambayo ni sawasawa na asilimia 36 ya Bajeti Kuu, hadi tunafika mwezi Aprili 2023 Serikali ilikuwa imeshatumia trilioni 11.5 ambayo ni asilimia 76.5 ambayo kwa kweli ni asilimia nzuri, ninaipongeza na ndiyo maana nimesema napongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nashukuru kwa kuondoa zile ada za vyuo vya ufundi ambavyo ni DIT, MUST pamoja na ATC. Wananchi wengi walikuwa watoto wetu wanapata shida kule lakini kwa kuondoa hiyo wanafunzi wengi watasoma na tunaendeleza elimu ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Waziri kwa usikivu ameleta katika misingi yake sita, kuna msingi mmoja wapo wa ongezeko la ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji. Hiki ndiyo kitu cha msingi ambacho tulikuwa tukikipigania kwamba Serikali peke yake haiwezi kufanya kazi bila kuwa na PPP, hii itasaidia kwenye masuala mengi kuondoa umaskini lakini pia kuleta ajira, kwa kufanya hivyo unakuta kwamba ni nchi nyingi, Serikali siyo Mwajiri Mkuu, Mwajiri Mkuu ni hizi private sector.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta kuna kitu ambacho concept hii haieleweki vizuri, tuna shida kubwa sana ya kutokuielewa kwa nini? Wakati tunakusanya labda kodi tunaagalia vyanzo vya kodi kwa mfano tuna vyanzo 50 vya kodi, tunataka bilioni moja mwaka huu, lakini mwakani tena tuna vyanzo hivyohivyo 50 tunataka bilioni tatu, badala ya kuongeza vyanzo viwe vikubwa ili tuweze kupata kodi nyingi. Kodi nyingi tutaipata tukiwa tumeweza kuweka mazingira wezeshi kwa vijana na watu wengine kuweza kupata mikopo kwa bei rahisi ambayo itawawezesha kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidi sana. Nazungumzia hivi kwa sababu kodi imekuwa kubwa. Kodi ikiwa kubwa, wananchi wengi wanashindwa kujiajiri, wanashinda kuajiri wenzao. Nitatolea mfano. Kwa mfano, mtu ana biashara yake, ameagiza kontena, labda la shilingi milioni 300 limefika pale bandarini, Afisa wa kutoza ushuru anakuja anamwambia kabisa, badala ya shilingi milioni 300, lipa shilingi milioni 70 nami unipe shilingi milioni 20. Watanzania walio wengi wanajikuta wakiingia huko. Mnaweka mazingira ya watu kutoa rushwa, lakini ukitoza bei ambayo ni reasonable, watu watakwenda kulipa na Serikali itapata fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tujitahidi kuongeza ukubwa wa vyanzo vya mapato ili wananchi wengi waweze kufanya kazi yao na Serikali ipate kodi nzuri. Kwa mfano, unaangalia changamoto iliyotokea Kariakoo, wananchi wengi kupiga kelele, lakini yote hii ni kwa sababu ya kodi kubwa. Mmeona jinsi ambavyo mkitekeleza hivyo wananchi wengi watapata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tozo zimekuwa kubwa. Mnatoza magari tozo kubwa. Kwa mfano, gari jipya ili lifike hapa, tozo yake ni kubwa sana. Kodi yake ni kubwa sana. Hata lori mnatoza. Kwa nini mnafanya hivyo? Kwa sababu wananchi wanashindwa ku-afford kununua magari mapya, ndiyo maana wanaingiza magari chakavu. Tumeona kabisa magari chakavu yanaingia, na yakiangia yanaharibu mazingira na Serikali vilevile inakosa kodi, kwa sababu magari yale yanakuwa chakavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini wasi-enjoy kuendesha magari mapya? Punguzeni kodi ili wananchi wanunue magari mapya. Kwa mfano, lori. Lori ni uchumi, linaweza likaajiri watu wengi sana; dereva, fundi, utingo na watu wengine ambao wanabeba mizigo. Sasa ukiweka ushuru ukawa mdogo, malori mengi yataingia, wananchi watakuwa wanawaletea kodi kila mwaka na mtapata magari mengi ambayo yatakuwa yanahudumia watu na wananchi wengi watapata ajira. Mkianza kuweka kodi kubwa, tunashindwa kupata hivyo. Kwa hiyo, naomba mpunguze kodi katika vitu hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, nitazungumzia ongezeko la bei ya mafuta. Bei ya mafuta itakapoongezeka, automatically vitu vyote vinapanda bei, na hii ni shida. Kwa nini inafika hapo? Kwa nini tusiwe na utaratibu mzuri wa kuweza kuangalia vyanzo gani vitatupa fedha? Napendekeza kwa mfano, matumizi badala ya mafuta, tuangalie namna tutavyotumia gesi. Tunayo gesi na tumekuwa na upungufu wa dola hapa ndani. Kwa sababu tuna upungufu wa dola, tuanze kutumia gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dangote anatumia gesi. Amekuja kuwekeza kwenye viwanda, lakini magari yake yanatumia gesi. Kwa nini Serikali tusianze na magari ya Serikali, mwendokasi tutumie gesi yetu? Kwanza tuta-save dola, tutatunza mazingira na vilevile ajira zitakuwa nyingi. Tukianzia hapo, na wananchi wataanza kutumia gesi katika magari yao, halafu tutakuwa tume-minimize kutumia dola yetu kwenda nje na tutabaki nayo hapa ndani. Kwa hiyo, badala ya ku-import mafuta kwa kutumia hiyo, tutakuwa tunatumia gesi yetu. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri tuangalie suala hili kwa umakini kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo, naomba nichangie pia kuhusu kutengeneza mabilionea. Yaani tutengeneze hata mabilionea kumi ambao ndio watakuja kutuletea mambo mengi katika nchi hii. Hayati Dkt. Magufuli aliweza kuwezesha Kiwanda cha Sukari cha Bakhresa, akatoa eneo, akaiamuru Benki ya Kilimo iweze kum-support, I think ilikuwa shilingi bilioni 100 kama sikosei. Sasa hivi tunaanza kuona sukari siyo shida kubwa vile. Kwa nini tusiende tukatengeneza watu kama hao hata kumi ili waweze kufanya vitu vikubwa kama hivyo vikaweza kusaidia nchi yetu kusonga mbele. Kwa hiyo, nashauri tufanye hivyo. Hii itatusaidia sana kuondoa tatizo la ajira, kuondoa umaskini na vilevile uchumi utakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ongezeko la fedha kwenye utoaji wa simu. Tunajua nia siyo mbaya, lakini mnawaonea wananchi wa chini. Kwa sababu unapoweka hiyo ina-cut across kwa mwananchi wa kipato cha chini na kipato cha juu. Sasa wote wanatoa, unapofanya hivyo, wale wananchi kule kijijini unakuta mtu anatumiwa shilingi 5,000; shilingi 10,000, au shilingi 6,000, unapokata, ujue wale wote inawakuta. Kwa nini tusiangalie kitu kingine kitakachowasaidia? Kwa sababu wananchi wetu wanapata shida. Unapoweka shilingi 10,000, unamkata tena, anakuwa hapati fedha inayotakiwa. Kwa hiyo, ina-cut across kwa wote. Nia ni nzuri, lakini tuangalie namna ambavyo inaweza ikafanya kazi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tozo ya pikipiki, sikatai, pia ni tozo nzuri, lakini mimi nilikuwa nadhani, utaratibu wa kupata kodi lazima uangalie economy, yaani usitumie hela nyingi kuchukua pesa kidogo. Nataka kujua kwa Mheshimiwa Waziri, anapokuja hapa atuambie, tuna pikipiki ngapi ambazo anatarajia kukusanya hizo kodi zake na ana staff wangapi wa kukusanya hizo pesa kutoka kwenye hizo pikipiki? Kwa sababu ni ngumu sana ukiangalia, lakini atakuja atatueleza, ni namna gani atafanya ili aweze kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi walio wengi kwa kweli unakuta wana kipato cha chini, wale vijana ndio wanaanza kutafuta maisha. Kwa hiyo, tuangalie namna ambavyo tunapona. Tuna vyanzo vingi vikubwa. Ukiangalia vyanzo ni vingi vikubwa ambavyo tunaweza tukapata fedha nyingi na kuweza kuendesha nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la kilimo. Nitajikita kwenye kilimo cha parachichi. Kule Iringa tunalima parachichi, Njombe na kwingineko wanalima parachichi. Tunapenda tuimarishe vituo vya tafiti. Kwa mfano, kuna kile kikonyo kinaitwa sayo. Kile kikonyo ni cha muda mrefu, tuangalie namna ya kuhuisha ili mbegu ile iendelee kuwa na ubora. Ikiendelea kuwa na ubora, wananchi wataweza kuzalisha parachichi nyingi zaidi. Kwa hiyo, hiyo imekuwa ni changamoto na tumeona kule kwetu, kile kikonyo kikiendelea kwa ile ile privet ya mwanzo inaleta shida katika uletaji wa mazao. Kwa hiyo, parachichi inapungua jinsi unavyoendelea kama kile kikonyo hakijawa kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iweke msamaha wa kodi ya magari ya baridi (cold trucks), zile cold containers. Mkiweka msamaha wa kodi, wananchi wanaweza wakafanikiwa sana, kwa sababu imekuwa ni gharama kubwa, wananchi wanashindwa kuhimili kumudu hayo magari na kusafirisha nje, na soko linataka uhifadhi katika chombo kama kile. Kwa hiyo, mkikitolea msamaha hapo, mtawezesha wananchi wangu wa Mkoa wa Iringa, wale wakulima wa parachichi na wengine katika mikoa mingine waweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)