Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye hoja iliyoko mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ninaunga hoja mkono asilimia 100 kabisa na kwa upekee kabisa nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Niseme wazi kabisa kwamba Mheshimiwa Rais kazi anayoifanya ni kubwa kwa kiwango ambacho tumetekeleza bajeti kwa Wizara zote kwa zaidi ya asilimia 50. Hii inaonyesha kwamba Wizara ya Fedha pia na Mamlaka ya Mapato Tanzania wanafanya makusanyo vizuri. Tuwapongeze sana; kwa sababu sehemu kubwa ya miradi ya maendeleo inatekelezwa vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nina hoja zangu mbili. Hoja ya kwanza ni kuhusiana na suala la unclaimed financial asset. Nilizungumza wakati ule na niliahidiwa kwamba litakuja kutolewa ufafanuzi mwaka huu; na niko hapa nikisubiria ufafanuzi kuhusu unclaimed financial assets kwenye Taifa letu. Hawajawahi kuzungumza popote ambapo hizi fedha ambazo zimekuwa unclaimed kwenye benki, kwenye mitandao ya simu na hata kwenye maliasili, kwenye vituo vya polisi. Ukisoma kwenye ripoti ya CAG anazungumzia bodaboda zipo kwenye vituo vya polisi zina miaka mitatu, minne zinauzwa hadi kwa shilingi 20,000 kwenye ripoti ya CAG. Kwa hiyo ni vyema Mheshimiwa Waziri wakatoa ufafanuzi fedha hizi zinaenda wapi, ambazo ni mali ya Watanzania na walituahidi kwamba watakwenda kulifanyia kazi kupitia Ofisi ya PST. Kwa hiyo ninaomba majibu Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nipende kupongeza, tulishauri kwenye Bunge kuhusu kupunguza msururu wa watendaji wa Serikali kuingia kwenye maduka ya Watanzania na wafanyabiashara wanaonzisha biashara zao. Tulizungumza hapa kwamba mtu anaanzisha biashara lakini kuanzisha kwake biashara ni kama anafanya kitu haramu kwa sababu akiamka asubuhi watu wa fire wameingia, watu wa NEMC wameingia, watu wa OSHA wameingia, watu wa TRA wameingia, watu wa service levy wameingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukashauri hapa Serikali itafute namna moja ya ku-centralize hii iwe ni moja tu. Mtu alipe tu hiyo Serikalini kwa mwezi kugawana. Na naona kuna mawazo yako kwenye bajeti hii umeyatoa; nikupongeze sana, kwamba kwa hili unakwenda kuilinda sekta binafsi, na kwamba ni nia ya dhati ya Mheshimiwa Rais kuona sekta binafsi nchini inalindwa ili mfanyabiashara apate muda wa kuhudumia zaidi wateja kuliko kuhudumia watumishi wa Serikali; na kwa kweli mnaenda kuandika historia. Ule mfumo, tulisema hata waleti mwanaume kujaa waleti mfukoni vimejaa vitambulisho sio jambo zuri tuwe na kitambulisho kimoja ambacho kinaweza kikasaidia. Kwa hiyo niseme hili unaloenda kulifanya unaenda kufanya jambo la kizalendo kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuzuia kamata kamata. waheshimiwa Wabunge walipiga kelele hapa wakati NEMC wamefungia na maeneo tofauti tofauti. Bado ni mwendelezo wa Mheshimiwa Rais kulea sekta binafsi kwenda kuzuia sasa kamata kamata tu-deal na muhusika ambaye amefanya hujuma yoyote ile ndiye tuhangaike naye. Hii itasaidia hata Kariakoo na maeneo mengine ya masoko na hata sekta ya biashara kukua ili tuli-deal na hawa wahusika ambao sioy kuliko ku-deal na biashara ambayo tunakuwa tunasababisha Serikali inakosa mapato. Kwa hiyo mimi nipongeze kwenye hayo mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo langu na agenda yangu ipo kwenye jambo moja; na hili ndio nililotumwa na Makete hili wamenituma watanzania, hili wamenituma wakulima wa ngano kwenye Taifa letu. Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako ukurasa namba 149 unasema una mpango wa kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kwa uratibu wa duty remission kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya 35 kwa mwaka mmoja kwenye ngano inayotambulika kwa HS Codes hizo hapo, lengo lake ni kupunguza gharama za maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri inawezekana una nia ya dhati kabisa lakini nia yako ya dhati inawezekana inaenda tofauti na mpango wa Mheshimiwa Rais, tofauti na Waziri wa Kilimo, tofauti na kile kinachofanyika field. Mimi ni Mbunge wa Makete, Mheshimiwa Rais ametupa ngano tani 80 kwa ajili ya wananchi wetu na amegawa bure Makate na inawezekana na mikoa mingine kama Arusha ameigawa bure. Lengo la Mheshimiwa Rais ni kumsaidia mkulima na ngano iweze kuoteshwa kwa wingi nchini ili soko la ndani la ngano liweze kufanya vizuri. Unapokuja na mpango huu Mheshimiwa Waziri unataka kutuambia ni kama mnataka kumuhujumu mkulima. Kwa nini? ukisoma ukurasa wa 257 kwenye hansard za Bunge za Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe anazungumza naomba Wabunge mnisikilize.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bashe anasema hivi; “Mheshimiwa Spika, niongelee hii issue ya ngano na alizeti. Sisi tuna-import ngano tani milioni moja kwa mwaka. Ili tujitosheleze ngano tunahitaji ngano tani 50,000 za mbegu za kwenda kumpa mkulima alime. Tumechukua hatua gani?” Akaendelea; “Mheshimiwa Spika, nataka niseme mbele ya Bunge lako tukufu niseme mbele ya Wabunge na mbele ya Watanzania kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu 2025/2026 tunaendelea kuzalisha ngano. Mwenye mamlaka ya kuwapa cheti cha ku-import ngano ndani ya nchi ni Waziri wa Kilimo. Kama nitakuwa kwenye kiti viwanda vitageuka chuma chakavu, hawataingiza hata kilo moja kama hawajanunua ngano ya Watanzania.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bashe anazidi kuongea, anasema; “Mheshimiwa Spika, Watanzania hawatakufa kwa kukosa ngano, haiwezekani unambembeleza. Mmefanya nao trial tumewapa mbegu wao wenyewe kwenye maabara zao wamesema inafaa halafu wakati wa ku-sign MOU wanasema hatutaki. Over my dead body wata-sign mkataba, wasipo-sign hatutawapa phyto sanitary ya kuingiza ngano, watajua watakachokifanya na viwanda vyao”. Huyu ni Waziri wa Kilimo analizungumza hilo, huyu ndiye aliyesambaza mbegu kwa wakulima, huyu ndiye aliyetuma hasa ikazalishe mbegu, huyu ndiye anakaa na Mheshimiwa Rais kwenye sekta ya kilimo, wanapanga ili ngano izalishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kila mwananchi wa Makete amezalisha ngano leo unakwenda kumwambia huyu mtu aingize ngano kwa ushuru wa kutoka 35 kuja kwenye 10 percent, hii ni sabotage kwa mkulima wetu, hii ni sabotage kwa wana-Makete, hii ni sabotage kwa mwananchi aliyeko Mbulu. Hii ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; mnazungumza jambo moja lakini kwa lugha tofauti. Tukimruhusu mfanyabiashara aingize ngano Mheshimiwa Waziri Bashe anasema hawa watu wamemkataa kwenye MOU manake unataka utuambie amezunguka nyuma, wamekutana na watumishi wako wa Wizara wamemwambia shusha kutoka asilimia 35 percent uje kwenye asilimia 10 percent. Kufanya hivyo ili Waziri wa Kilimo aendelee kubaki katika msisitizo wa kwamba hawa wanabaki na viwanda vyao kumbe wametengeneza lango lingine la kuingiza ngano kwa kupitia kushusha ushuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri Mwigulu una heshima kubwa kwenye Taifa letu, ninakuomba sana achana na hii biashara. Tumepita kwenye covid tukiwa kwenye asilimia 35, tumepita kwenye mtikisiko wa uchumi tukiwa na asilimia 35, unaendaje saa hizi angalau hali iweze kupoa tunaanza kushusha kwenye asilimia 10? Tunaua viwanda vya ndani. Mimi nitaenda kuwaambia nini wananchi wa Makete, Matamba na Ikuo ambao wameacha mazao yote nimewaambia limeni ngano? Leo hii mnaenda kuwaambia wafanyabiashara washushe ngano waingize kwa asilimia asilimi 10 waache 35.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Waziri wa Viwanda na Biashara; kweli inawezekana tuna upungufu wa ngano tafuteni utaratibu wa kuweka kibali maalum kwa ajili ya kuingiza huyo mtu lakini si kwa asilimia hii mliyoitaja, tunaenda kuua wakulima wetu. Yaani Mheshimiwa Anthony Mtaka pale Njombe amepambana kweli kuhakikisha ngano inaota. Mimi nimepambana kweli kuona ngano inaota. Mkuu wa Wilaya ya Makete Mheshimiwa Juma Sweda amepambana kweli kuona ngano inaota. Mkurugenzi wangu Ndugu William Makufwe amepambana kweli kuhakikisha ngano inaota. Na hata juzi Tume ya Mipango imekuja tumeanza kupima vijiji 41 na kuwapa hati kwa sababu ya zao la ngano. Leo tunakuja kusomewa hapa mfanyabiashara anaongezewa dirisha la kuingiza ngano nyingi ili ngano ya ndani izame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri, hili ni jambo la muhimu sana kwenye Taifa letu. Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Kilimo kaeni chini tusaidieni. Mheshimiwa Waziri najua una nia njema ninajua una nia njema lakini nia yako njema inaenda kuzamisha watoto wako wa ndani, unaenda kuzamisha familia yako Mheshimiwa Waziri. Nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha nikuombe…

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri anakuomba tu huyo utakuja kumjibu.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe unafanya vizuri sana kwenye Wizara yako, miradi iko kedekede umetupelekea fedha huku hatujawahi kuziona fedha nyingi kwa kiwango hicho…

MHE COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. FESTO R. SANGA: …hili kosa la kuruhusu ngano iingie lisiende kufanyika …

MWENYEKITI: Kuna taarifa Mheshimiwa Festo.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, unanizamisha mimi, unazamisha Wabunge, unazamisha Wabunge ambao kila siku…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Festo kuna taarifa yako, Mheshimiwa Cosato Chumi.

TAARIFA

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, mojawapo ya hatua ambazo tunatakiwa kuzifanya ni kuhakikisha kwamba tunapunguza kuagiza bidhaa muhimu kutoka nje ili kujijengea uwezo wa ndani. Sasa basi analolisema la kibali ni muhimu, tumefanya hivyo katika sukari matokeo yake tulikuwa tunaagiza tani 300,000 leo hii tunaagiza tani 15,000 na viwanda ndani vimeshamiri na wananchi wetu wanapata ajira. Kwa hiyo anachokitetea siyo kwa wananchi tu wa Njombe, wa Makete, ni wa Tanzania nzima na Taifa kwa ujumla. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Festo, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hii taarifa, kwa sababu tunaenda kulinda viwanda vya ndani, tunaenda kulinda wakulima wetu napokea kabisa. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, aachane na hii biashara, huu ni mchezo, wamemzunguka Mheshimiwa Bashe kule kwenye MoU, mbegu wameenda nayo maabara wao wenyewe, wamepima wakasema Waziri hapa tutaingia pamoja kwenye hii. Walivyofika kwenye kusaini mezani wakamgeuka kumbe wameona dirisha nyuma ya Waziri, wamepita huko, wameenda kushusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri aachane na hii biashara, amsaidie Mheshimiwa Bashe, awasaidie wakulima wa Makete, Njombe, Iramba, Kisasatu na awasaidie wakulima wa kila eneo la Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, hoja yangu ni ngano na nitakufa nayo, kwa sababu hizi ndiyo kura za CCM, hizi ndiyo kura za Mheshimiwa Rais, hizi ndiyo kura za Taifa langu, lazima niwapiganie, ahsante. (Makofi)