Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Awali ya yote kwanza nitumie fursa hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo langu la Bukene. Nimshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi za maendeleo ambazo zinaletwa kwenye Jimbo letu la Bukene ukilinganisha na kipindi kingine chochote kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mambo kadhaa, lakini la kwanza nitaanza na Hifadhi ya Taifa ya Chakula. Nimeona kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri, ambalo ni jambo jema, kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kununua chakula kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa ya Chakula, na makadirio mwaka huu ni kununua tani 400,000 hadi 500,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ushauri wangu ni kwamba tani hizi hazitoshi na kama kuna uwezekano basi fedha zitafutwe ili angalau, najua hatuwezi kuwa na fedha za kutosha kununua tani nyingi kwa wakati mmoja lakini angalau hata tufike tani 700,000 kwa mwaka huu itapendeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa hifadhi ya chakula unajulikana, hasa pale ambako hifadhi hii ya chakula inatumika ku-stabilize price kupunguza makali ya bei pale ambapo kunakuwa na uhaba mkubwa wa chakula. Hapa juzi juzi sisi tumepita kipindi kigumu sana, pale Jimbo langu la Bukene kuna wakati debe la mahindi lilifika mpaka 23,000. Lakini nipongeze Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, niliomba Serikali na walileta mahindi, kwa maana ya Hifadhi ya Taifa ya Chakula na tukapunguza bei ya mahindi kutoka debe 23,000 mpaka 14,000 ambayo ikasaidia kuwavusha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito kwa Hifadhi ya Taifa ya Chakula, mara zote imekuwa ikitumia pale Bukene kama kituo cha kununua na kwa sababu kuna ma-godown makubwa yanayomilikiwa na Chama cha Ushirika cha Igembensabo. Kwa hiyo Hifadhi ya Taifa ya Chakula tunawakaribisha pale waje wakodi hayo ma-godown kutoka Chama cha Ushirika cha Igembensabo waweze kununua mahindi na kuhifadhi pale, yatatusaidia sana kwa sababu mwaka huu pia siyo mzuri sana kihivyo. Kwa hiyo tunahitaji kuwa na hifadhi ya chakula kwa ajili ya usalama wa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni kwamba ukiangalia ukurasa wa 147 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye hatua za kikodi ambazo Serikali inapendekeza. Waziri wa Fedha amependekeza mojawapo ya hatua za kikodi ni kupunguza ushuru wa forodha kwa mafuta ya kula yanayotoka nje ya nchi kutoka asilimia 35 mpaka asilimia 25. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, hatua hii ya kikodi ya kupunguza ushuru wa mafuta yanayotoka nje ya nchi ita-discourage, itavunja moyo wakulima wetu wa ndani hasa kwenye maeneo ya mazao ambayo yanazalisha mafuta ya kula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukitumia jitihada kubwa sana mwaka uliopita kuhamasisha wakulima wetu walime alizeti kwa ajili ya kuzalisha mafuta ya kula ili kupunguza upungufu wa mafuta ya kula. Tunajua tuna gap kwamba mafuta ya kula tunayozalisha hayatoshi kwa matumizi yetu na kutokana na hilo kumekuwa na mkakati wa makusudi wa kuhamasisha kilimo cha mazao mbalimbali yanayozalisha mafuta ikiwemo alizeti. Sasa pendekezo hili la Serikali la kupunguza kodi, ushuru wa forodha kwa mafuta ya kula yanayotoka nje, litafanya mafuta hayo ya kula sasa ya kutoka nje yawe bei ndogo/bei nafuu na mafuta yetu ya alizeti yatakuwa ya bei kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili jambo litafanya kwanza wananchi ambao tunawahimiza walime alizeti watavunjika moyo, lakini tumehamasisha sana viwanda vidogo vidogo vya kusindika mafuta ya alizeti na vyenyewe vitavunjika moyo na hatimaye vitakufa. Kwa hiyo ushauri wangu, Mheshimiwa Waziri wa Fedha pendekezo hili la kushusha ushuru wa forodha tubakie pale pale badala ya kushusha kutoka thelathini na tano mpaka asilimia ishirini na tano tubakie na asilimia thelathini na tano hiyo hiyo ili kulinda viwanda vya ndani vya kusindika mafuta ya alizeti na wakulima wetu wadogo wadogo waweze kuendelea kulima alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, naunga mkono ongezeko la bajeti kwenye Wizara ya Kilimo. Sisi ambao tunatoka majimbo ya vijijini asilimia kubwa wananchi wetu shughuli yao kubwa ni kilimo. Tunataka wananchi wetu waendelee kupata mbolea ya ruzuku, lakini tunataka tuendelee kuona skimu za umwagiliaji zikiendelea kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii na naunga mkono bajeti kwa sababu nahitaji fedha kwenye skimu yangu kubwa ya umwagiliaji. Serikali imenipa skimu kubwa sana hekta 4,000, yenye thamani ya zaidi ya bilioni 40 kwenye Kata ya Sigili pale kijiji Lyamalagwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuendelea na skimu kubwa niishauri Serikali isiyaache kabisa mabwawa madogo madogo au skimu ndogo ndogo ambazo zimekuwepo kwa muda na ambazo sasa hivi zimejaa mchanga na hazifanyi kazi vizuri. Kwa mfano, kwangu pale kuna Bwawa la Ikindwa, Bwawa la Malolo, Bwawa la Ng’indo, Bwawa la Chamipulu maeneo ya Mambali kule ambako kuna mabwawa madogo madogo ambayo zamani tulikuwa tunayatumia sana kwa umwagiliaji, lakini muda umekuwa mrefu yamejaa mchanga na sasa hivi hayafanyi kwa ufanisi tunao utarajia. Kwa hiyo pamoja na kujikita kwenye skimu kubwa za umwagiliaji, lakini tusisahau hizi ndogo ndogo ikiwemo na Skimu ya Kamahalanga kwa maana ya kuzifufua na zifanye kazi kadri inavyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti hii kwa sababu bado nahitaji fedha kwa ajili ya kuendelea kuboresha barabara za vijijini. Kazi kubwa sana imefanyika ukilinganisha na hapo nyuma. Barabara zetu za vijijini, TARURA wamefanya kazi kubwa sana, wamepasua maeneo ambayo hata hayakuwa na barabara kabisa, lakini kwa sababu hali haikuwa nzuri kazi ya kupasua barabara na kuimarisha barabara za vijijini bado inahitajika. Kwa hiyo, naunga mkono bajeti hii. Kwa sababu inaendelea kupeleka fedha kwa ajili ya eneo la uimarishaji wa barabara vijijini na huko vijijini ndiko uzalishaji uliko. Unaposema barabara za vijijini maana yake ni kwamba bei ya mazao kwa wananchi wa maeneo ya vijijini itaimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti hii kwa sababu inaendelea kupeleka fedha kwenye Miradi ya Maji, kazi kubwa sana imefanyika pale kwangu sasa hivi kuna kazi kubwa sana ya kuyatoa maji ya Ziwa Victoria, Nzega Mjini kuyapeleka Bukene, vijiji ishirini karibu 21 vinakwenda kufaidika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Zedi.

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono bajeti hii kwa sababu bado nahitaji fedha zipelekwe ili maji yafike kwenye vijiji vyote katika Jimbo la Bukene.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono bajeti. (Makofi)