Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE.JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, namshukuru Mungu kwa kunijalia afya kwa mara nyingine kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Hasna Mwilima kwa kushinda kesi ya uchaguzi katika Jimbo la Uvinza. Kwa niaba ya wanawake wa mkoa wa Kigoma ninampongeza sana na ninamshukuru Mungu kwa kuweza kutenda maajabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana CCM tulikuwa tunaitwa wapinzani, lakini kwa utekelezaji mzuri wa Sera za CCM Mkoa wa Kigoma waliamua kuachana na upinzani wakarudi kukitendea haki Chama cha Mapinduzi. NCCR Mageuzi wakati ule walikuwa wanasema wao ndio Chama Tawala sasa Kigoma Chama cha NCCR Mageuzi kwisha kabisa, chali cha mende, nyang‟anyang‟a. Tumebaki na …
Mheshimiwa Mwenyekiti baada ya kuzungumza hayo…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Genzabuke, endelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti niliwahi kuwaambia, kwa mambo makubwa yaliyofanyika Kigoma..
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mambo yalifanyika Kigoma wananchi wa Kigoma waliamua wakasema, sasa NCCR basi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukurani hizo za kumpongeza Hasna, naomba nianze kuchangia. Mkoa wa Kigoma tutaendelea kumkumbuka Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuweza kuufungua mkoa wa Kigoma akiwa na Waziri wa Ujenzi ambaye ndiye Rais wetu, Mheshimiwa John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya matendo makubwa sana, amejenga barabara za lami tunazopita, wana CCM na wapinzani wote ni mashahidi, zilijengwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanasema barabara zimeharibika. Kumbukeni mvua zikinyesha barabara zinaharibika, magari makubwa yakipita barabara zinaharibika, kwa hiyo ndugu zangu ambao mnasema Mheshimiwa Rais hajafanya chochote; mwaka jana wakati anawasilisha bajeti yake akiwa Waziri wa Ujenzi kwa kumbukumbu zangu nakumbuka kabisa Wabunge wote tuliipitisha bajeti ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli, kwa kura za ndiyo bila kupinga bajeti ile, wote tunaamini ni mchapakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana mwaka wa jana tulipokwenda kwenye uchaguzi hatukuhangaika kumnadi Mheshimiwa John Pombe Magufuli, alijiuza mwenyewe kwa sababu ya utendaji wake uliotukuka.
Ninaomba kusema, kwa barabara ambazo tayari zimeshafunguka, naomba sasa barabara ya Kigoma – Nyakazi, Kigoma – Kasulu kilometa 50, Nyakanazi – Kibondo, kilometa 50, nashukuru kwa kutengewa pesa. Ninaomba sasa barabara ya kutoka Kibondo – Kasulu mpaka Manyovu nayo iweze kutengewa pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumekuwa tukisifika kwa kuwapokea wakimbizi, lakini watu wanaobeba mzigo mkubwa wa kuwapokea na kuwabeba wakimbizi ni watu wa Kigoma. Kwa hiyo, ninakuomba Mheshimiwa Waziri ambaye mwaka huu kabla ya bajeti hii ulitoka Kibondo, Kasulu mpaka Kigoma ukaone kile kipande cha kilometa 258 ambacho ndicho kimebaki hakijatengewa pesa. Kipande kile ndicho kinachotumika kupitisha wakimbizi wanapotokea Burundi kupita Manyovu, kuja Kasulu kwenda mpaka Kibondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kipande hicho kitengewe pesa mara moja ili na chenyewe kiweze kukamilika.
Ninaomba kipande cha kutoka Uvinza mpaka daraja la Kikwete kiweze kutengewa pesa ili kikamilike ikiwa ni pamoja na kipande cha Chagu mpaka Kazilambwa na chenyewe kiweze kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie kwenye reli. Huu ni mwaka wangu wa 11 nikiwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muhuri ya Muungano wa Tanzani. Mimi kwa kushirikiana na Wabunge wa mkoa wa Kigoma, Shinyanga, Mwanza, Tabora, Mara, Rukwa Katavi na Kagera kilio chetu kikubwa kimekuwa ni reli. Tunaomba basi mipango ya ujenzi wa reli inayowekwa iwe ni ahadi inayotekelezeka, isije kuwa ni ahadi isiyotekelezeka. Ipangwe kujenga kwa standard gauge ili wananchi waweze kunufaika na matunda ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa mkoa wa Kigoma, na mikoa yote hiyo niliyoitaja wanapata shida sana kutokana na ukosefu wa usafiri wa uhakika wa reli. Akina mama wanapata shida, wanateseka, wanafunzi wanapokwenda shuleni wanapata shida sana. Tunaiomba Serikali, iweze kutekeleza ahadi ya kujenga reli ili kuwaondolea shida wananchi wanaoishi ukanda huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nimeangalia katika kitabu hiki sijaona kama imetengewa pesa kwaajili ya ukarabati wa bandari ya Kigoma. Ninaomba tunapokwenda kujenga reli na bandari ya Kigoma nayo itengewe pesa kwa ajili ya kutengenezwa. Kwa sababu mizigo ikisafiri kupitia reli ni lazima itafika bandarini, ikifika bandarini itasafirishwa kwenda DRC na Burundi. Kwa hiyo sambamba na kutengeneza reli tunaomba na bandari nayo iweze kuangaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, meli ya Liemba ina miaka 100; meli ile ipo kabla ya uhuru, naomba iwekwe meli nyingine ya kusaidia meli ile. Tunapoteza mapato mengi sana kwa sababu meli tuliyonayo imechoka, imezeeka, kwa hiyo tunaomba tupatiwe meli nyingine. Lakini vilevile tunaweza hata tukapewa boti hizi za fiber boat kusudi ziweze kusaidia kusafirisha mizigo kutoka Kigoma kupeleka Burundi na DRC. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kiwanja cha ndege cha Kigoma. Ninaomba kiwanja hicho kiweze kutengewa pesa, kipanuliwe ili ndege ziweze kutua na kuruka. Ndege kubwa haziwezi kuruka kwa sababu uwanja ule maeneo ya kuruka ni kidogo. Naomba kipanuliwe ili ndege kubwa ziweze kuruka. Kwa sababu kiwanja kile kikiweza kutengenezwa kikawa na maeneo ya kuruka na kutua ndege kubwa watu wataweza kufanya biashara muda wote, tofauti na ilivyo sasa ndege ikienda asubuhi ikifika kule mchana hakuna ndege nyingine inayoweza kutua jioni au usiku.
Kwa hiyo, naomba kiwanja kile kiweze kutengenezwa. Lakini vile vile kule kwetu kuna hifadhi ya Gombe watalii wataweza kuja kwa wingi kutoka maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma naomba kitengewe hela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.