Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niseme machache. Kwanza namshukuru Mungu kunisaidia kusimama hapa mbele na kuchangia hotuba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu JPM, maarufu sana mzee wa kutumbua majipu. Mheshimiwa Magufuli amefanya mambo mengi na lazima tumuunge mkono. Nataka niseme leo hili, mimi namuombea kwa Mungu na namuombea kwa sababu anakutana na changamoto nyingi ambazo kimsingi sisi Wabunge tunaziona. Kutumbua majipu siyo kazi rahisi, anapotumbua majipu kuna wengine wanaumia, wengine wanalia lakini wengine tunafurahi hasa sisi ambao tunatoka katika mazingira duni, sasa tunaanza kuona ukweli na uhalisia wa Serikali inavyozidi kuwajibika. Kwa nini nimeshukuru haya. Nimeshukuru haya kwa sababu tunaona sasa walau Serikali inaanza kuchukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi na kumshukuru Rais, namwambia aendelee. Inawezekana wapo wengine wanabeza hali hii, tulitaka Rais mkali, tulisema yule mpole, sasa amekuja mkali tumuungeni mkono jamani! Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Mimi namuombea kwa Mungu na kila siku nitasali kwa ajili hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, katika Wizara hii ya Miundombinu, napenda kuchangia eneo moja kubwa na kwa kweli hili nimetumwa na wananchi wangu. Kwa kuwa tunakuja huku kwa kura, naomba niseme hili kwamba katika swali namba 76 lililoulizwa kwenye Mkutano wa Pili wa mwezi Februari, Mheshimiwa Waziri alinijibu akasema barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom - Singida itajengwa na walau itawekwa kwenye mpango wa upembuzi yakinifu kwenye bajeti hii ya 2016/2017.
Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu nimeiona kwenye ukurasa wa 152 na ndiyo maana naona kweli walau Serikali inafanya kazi. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, huu upembuzi yakinifu basi usiendelee kwa muda mrefu sana kwamba mwaka huu mpaka mwakani upembuzi bado unaendelea. Barabara hii ni muhimu sana kwani pia imeahidiwa na Rais aliyetangulia. Juzi wakati anaomba kura Mheshimiwa Magufuli ameahidi tena barabara hii na wananchi wamempa kura na tuna imani kwamba barabara hii itaanza kufanyiwa upembuzi yakinifu halafu baadaye iweze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu Mbulu na Mbulu Vijijini ni wilaya ya siku nyingi sana, nimeshawahi kusema hapa imezaliwa 1905. Tukifanya kitu kinachoitwa research hapa tutakuta kuna Wilaya nyingine ambazo zimezaliwa hivi karibuni, kimsingi naamini Mbulu inapaswa kupata haki hii. Mbulu imeweza kuizaa Hanang, leo Hanang kuna kaafadhali kidogo, imezaa Babati na imezaa Karatu. Kwa hiyo, naomba niseme leo wilaya hii imekuwa bibi na kwa kuwa imekuwa bibi hebu muoneni huyu bibi basi awe kama kijana aweze kupatiwa hii miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi huwezi kutoka Mbulu ukafika makao makuu ya mkoa ambayo ni Babati, uko mlima unaitwa Magara, wakati Mkapa amekuja miaka 11 iliyopita kwenye kona za Magara alishaanza kusema mke wangu mnampeleka wapi kwa sababu zile kona zinaonyesha kama zinarudi. Kuna daraja pale linaitwa daraja la Magara, ukiitwa kikao kama unatokea Mbulu, Mheshimiwa Lukuvi naona unacheka, ina shida ile barabara, nafikiri ulipata kizunguzungu ulipopita pale, kufika Babati kuna daraja kubwa pale. Kwa hiyo, naomba ndugu zangu wapendwa muone na Wizara iangalie daraja hili ili liweze kuwekwa kwenye mpango ujao, daraja litengenezwe na ule mlima urekebishwe ili tuweze kufika makao makuu ya mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutoka pale kuna barabara ya kutoka Dareda - Dongobesh, hii barabara imewekwa kwenye Ilani ya CCM na mimi naamini huu ndiyo wakati mzuri wa kusemea sasa. Barabara nyingine ni kutoka Haydom – Katesh. Barabara hizi zinasaidia sana wananchi wetu kutoka katika maeneo yao kwenda kwenye Hospitali ya Haydom. Barabara hii haishii hapa inakwenda mpaka Sibiti inapitia Mkalama na Kidarafa inafungua Mkoa wote wa Manyara kwenda Singida, itahudumia maeneo yote mpaka Simiyu kule. Kwa hiyo, ndugu zangu Wabunge wa maeneo haya niliyoyataja, nafikiri ndiyo wakati wa kuieleza Serikali sasa kuifanya barabara hii ipitike na iweze kuleta kitu kinachoitwa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri sisi tunalima vitunguu saumu kule, mpunga na mazao mengi ambayo kimsingi sisi ndiyo tunaolisha viwanda. Ukieleza habari ya uchumi wa viwanda, Arusha hawawezi kuendelea bila kuwa na barabara iweze kupeleka mazao ghafi au malighafi katika viwanda vya Arusha. Kwa hiyo, barabara hii ikitengamaa na mkaijalia kuipangia bajeti katika mwaka wa fedha ujao baada ya huo upembuzi, hakika mambo yatakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Mungu kwamba Waziri kwenye majibu yake ya mwanzo amesema kwamba Benki ya KfW, Benki ya Ujerumani imekubali kufadhili barabara hii. Niombe sana, Mheshimiwa Waziri siku akiwa na kikao na hao wanaoitwa KfW tuite basi na sisi tuweze kushauriana nao tuweze kuweka hoja zetu ili barabara hii itoke Karatu – Mbulu - Sibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu najua muda ni mdogo sana, naomba nishauri mambo machache kwenye mawasiliano. Mawasiliano ni taabu katika maeneo yetu mengi sana hasa kwenye kata za Ari, Tumati, Mangisa, Yaeda Ampa, kule sisi tuna shida hiyo na ninaamini hii inasikika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala kubwa sana la kitu kinachoitwa barabara za Wilaya kupandishwa hadhi kufikia kuwa barabara za TANROADS. Manyara tuna miaka minne barabara hazijapanda hadhi. Kwa hiyo, niombe Wizara iiangalie Manyara kwa jicho la pekee na kuipandisha ile barabara hadhi maana sasa hivi Mkoa wa Manyara barabara zake zimekuwa scattered, hatuwezi kutoka wilaya kwa wilaya. Ukitoka Kiteto kuja Babati ni tatizo, ukitoka Babati kwenda Hanang ni shida hasa kutoka Mbulu kwenda pia Babati, niombe haya, naamini Wizara inasikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine kubwa katika Sheria ya Manunizi, naomba Mheshimiwa Waziri anayehusika alete mabadiliko ya Sheria hii ya Manunuzi, tufanye mabadiliko ya sheria hii hapa ili walau tuweze kujenga barabara zetu sisi wenyewe.
Halmashauri ziwezeshwe kununua vitu vinavyoitwa caterpillar, grader ili tuweze kujenga barabara zetu wenyewe. Niombe Mheshimiwa Waziri anayehusika, hizi caterpillar zinapoingia hapa zisamehewe kodi hasa sisi tukileta maombi kama wa halmashauri ili tuweze kujitengenezea barabara zetu wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nimshukuru sana Waziri na Naibu wake kwa hotuba nzuri na kuweka barabara zetu hapa. Nachoamini ni kwamba barabara zilizoko kwenye Ilani zitakuwa za kwanza kutengewa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipenda kuchangia haya tu, nasema naunga mkono haja. Ahsante sana.