Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii muhimu sana ya bajeti ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi ambazo anaendelea kutuletea Majimboni mwetu, kutatua kero za wananchi ikiweko suala zima la usambazaji wa nishati muhimu ya umeme, pia nipongeze sana Wizara ya Nishati chini ya Mheshimiwa Waziri Makamba na Naibu Waziri Byabato kwa kazi kubwa ambayo wanafanya ambayo inaonekana kwa wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na suala la umeme vijijini. Usambazaji wa umeme vijijini kwenye Jimbo langu unakwenda vizuri, nichuke nafasi hii kumpongeza Mkandarasi SILO Power ambaye anafanya kazi vizuri. Katika Jimbo langu lenye vijiji 81, vijiji vyote shughuli ya usambazaji wa umeme inafanyika isipokuwa kijiji kimoja tu cha Ikindwa na ambacho leo nilipokuwa kwenye banda la maonyesho pale, nilikutana na Mratibu wa REA na Mkandarasi SILO Power na wamenihakikishia kwamba wiki ijayo, kijiji cha Ikindwa kazi kwa sababu survey walishafanya, kazi ya kuchimba mashimo na kusima nguzo itaanza ili kukamilisha vijiji vyote 81 vya Jimbo la Bukene. Kwa hiyo kazi kubwa inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo ningependa kushauri ni kwamba haraka iwezekanavyo Wizara iende sasa kwenye mpango wake wa kuhakikisha sasa tunasambaza umeme kwenye ngazi ya vitongoji. Hesabu ya vijiji inaweza ikaku – mislead, kwa mfano mimi Jimbo langu lina vijiji 81 na almost vyote tayari umeme umefika lakini umeme umefika kwenye makao makuu ya kijiji. Mimi nina vijiji vingine ambavyo nitatoa mfano, Kijiji cha kakongwa, Kijiji cha Kagongwa kina vitongoji saba, lakini ni kitongoji kimoja tu kati ya saba ndicho kimepata umeme, vitongoji sita vyote havijapata lakini ukihesabu kijiji na Kagongwa unaihesabu kwamba imepata umeme lakini kumbe ni kitongoji kimoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina Kijiji cha Kayombo, Kijiji cha Kayombo kina vitongoji 11, katika vitongoji 11 ni kitongoji kimoja tu ndiyo kina umeme, makao makuu ya kijiji lakini ukihesabu kijiji unasema Kayombo imepata umeme ambayo Kayombo ina vitongoji 11 lakini ndani ya vitongoji 11 ni kimoja tu ndiyo kina umeme. Kwa hiyo, tuende sasa kwenye hatua ya vitongoji ili tuhakikishe sasa wananchi wetu wengi wanapata umeme lakini tuendane na malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ya Mwaka 2030 ambako lengo Namba Saba linasema ifikapo mwaka 2030 tuhakikishe wananchi wetu wanapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni usawa katika gharama za kuunganisha umeme maeneo ya vijijini. Mheshimiwa Ndulane amezungumza, ninafahamu mantiki ya kuwa na utofauti kati ya maeneo ya vijijini kuunganishiwa umeme kwa 27,000 na maeneo ya mijini kwa 320,000, lakini sasa kilichotokea ambayo sijui kwa sababu zipi, unakuta maeneo hayo hayo ya vijijini, kwa mfano Jimbo langu la Bukene lote ni vijiji lakini humo ndani ya vijiji kuna Kijiji cha Itobo na Kijiji cha Bukene eti vimewekwa kwenye group la Miji kwa hiyo kuunganisha umeme wateja wanatozwa shilingi 320,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Bukene na Itobo ni vijiji tu vina wenyeviti wa vijiji, vina Serikali ya vijiji, vinaendeshwa na kama vijiji tu. Kwa hiyo, kuvi - group kwenye group la Miji na kuwatoza 320,000 badala ya 27,000 hatuwatendei haki. Kijiji cha Itobo na kijiji jirani cha Lakui au Chamwabo vyote ni vijiji vinafanana, wote wanategemea kilimo, maisha yanafanana, lakini wananchi wa Itobo kwa sababu ni ka-center tu kidogo anatozwa 320,000 tofauti na mwananchi wa Lakui au Chamwabo ambao wanatozwa 27,000. Kwa hiyo, hii mimi naona siyo haki na ninashauri kwa kuwa eneo, kwa mfano Jimbo la Bukene lote ni vijijini kwa hiyo tusibague tena kwamba kijiji hiki kiwe mji, kijiji hiki siyo mji vyote ni vijiji vina wenyeviti wa vijiji vina Serikali ya vijiji, kwa hiyo kuwabagua kwamba wengine walipe 320,000, wengine 27,000 hatutendei haki baadhi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilipenda kuzungumza ni kuhusu mradi mkubwa wa bomba la mafuta. Nimeshazungumza pale kwenye Jimbo langu kuna coating yard, karakana kubwa ya kuyapaka special rangi maalum haya mabomba. Sasa juzi kwenye semia ya EACOP tuliambiwa kwamba mzigo wa kwanza wa mabomba unaingia Desemba mwaka huu na baada ya hapo utaanza kusafirishwa kutoka Bandarini Dar es Salaam kwenda Sojo Jimboni kwangu kwenye kituo cha kuyapaka rangi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kilipo pale ni rough road ukifika Nzega unaingia rough road kama kilometa 65, hata ukizungukia kule kwa Mheshimiwa Kishimba ukifika Kagongwa ni rough road tena mpaka kufika pale Sojo. Sasa siku zote nimekuwa nasema kwamba hiki kipande cha kilometa 65 kutokea Nzega kupita Itobo - Mwamala mpaka Sojo ni barabara nyembamba, madaraja membamba ni rough road, huo mzigo mkubwa wa mabomba hautaweza kupita. Juzi kwenye semina ya EACOP wale EACOP wenyewe walisema wako tayari na wameanza mazungumzo na Serikali ili kuchangia gharama ya kuimarisha kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami kutoka Nzega Mjini – Itobo – Mwamala mpaka kufika pale Sojo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Wizara ya Nishati kwamba pengine Wizara ya Ujenzi wao umuhimu wa hiyo coating yard hawauoni lakini pale ni uwekezaji wa bilioni 600 na mabomba yote yatakayolazwa kilometa 1,440 lazima yafikishwe pale kwanza, yapakwe special rangi hiyo ili yaweze ku – maintain temperature ili mafuta yasigande yaweze kutiririka. Sasa hayo mabomba yanafika port ya Dar es Salaam Desemba yataanza kusafirishwa, yatafikaje pale coating yard kama kipande cha barabara cha kilometa 65 hakitamudu kuyabeba hayo mabomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mabomba ni mazito sana karibu tani 240,000 mabomba saba tu yanajaza lori moja. Kwa hiyo kale kabarabara kaliko pale, hivi sasa hayataweza kupita, nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwa sababu wewe uzito na umuhimu wa ile coating yard unaufahamu ni vizuri ukakaa na Wizara ya Ujenzi kwa sababu wao pengine umuhimu wa coating yard hawauoni ndio maana priority ya kutengeneza ile barabara inakua haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika bajeti nimepata fedha kidogo tu kama kilometa chache tu za hiyo barabara, sasa mabomba hayatafika pale kama hicho nilichoshauri hakitafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa kifupi kwamba pamoja na kwamba bado tuna mahitaji makubwa sana ya umeme na nishati nyingine lakini niseme kazi kubwa sana imefanyika katika Wizara hii ya Nishati ikilinganishwa na hali ilivyokuwa hapo nyuma. Katika Bunge la 2010, Mheshimiwa Waziri Makamba tulikuwa naye Kamati moja ya Nishati na Madini alikuwa Mwenyekiti wangu, hali ilivyokuwa wakati huo, hali ya nishati ilivyokuwa wakati huo na sasa ni vitu viwili tofauti kubwa. Kuna kazi kubwa sana imefanyika. Uthubutu wa kupeleka umeme vijijini, ndani ya Tanzania tunaweza tukaona ni jambo dogo la kawaida lakini ni jambo kubwa sana, miongoni mwa nchi za SADC, nchi ambayo inafanya kazi kubwa sana kwenye Village Electrification Tanzania inaongoza na iko mbali mno, iko mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukajiona hatujafanya jambo kubwa lakini wenzetu wa nje wanavyoona namna ya uthubutu na uwekezaji mkubwa wa kupeleka umeme vijijini, wanashangaa na wanaona ni jambo kubwa sana. Kwa hiyo, baada ya maneno hayo, ninaunga mkono hoja na niwapongeze sana Mheshimiwa Makamba na Naibu Waziri pigeni kazi, kazi yenu inaonekana. Ahsanteni sana. (Makofi)