Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo ameanza kutekeleza, vilevile niwapongeze Mawaziri wetu wote wa Wizara zote. Kazi mnazozifanya tunaziona, tunazidi kuwatia nguvu ili muendelee kufanya kazi zaidi. Nimpongeze pia Waziri Mkuu kwa usimamizi mzuri na kazi nzuri anayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijikite moja kwa moja kuzungumzia maendeleo ya Mkoa wa Njombe. Kwa kuwa hotuba tunayoijadili sasa hivi ni ya TAMISEMI, Mkoa wa Njombe ni Mkoa mpya na katika Mkoa huu mpya wa Njombe kuna Wilaya mpya ya Wanging‟ombe. Wilaya hii ya Wanging„ombe tuna uhaba wa hospitali hatuna hospitali ya Serikali tuna hospitali moja tu ya Ilembula ambayo ni ya binafisi, ya Kanisa hivyo basi wananchi wa Wilaya ya Wanging‟ombe wanatumia gharama kubwa sana katika matibabu. Naiomba Wizara hii ya TAMISEMI ione umuhimu wa kujenga hospitali ya Serikali ili kuweza kuwasaidia Wabena wenzangu wa kule Wanging‟ombe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati zetu katika Wilaya Wanging‟ombe hazina wahudumu wa kutosha, madaktari ni pungufu kabisa hakuna madaktari, utakuta nesi anafanya kazi ya daktari naomba pia Wizara hii ya TAMISEMI iangalie umuhumu wa kuongeza wauguzi kwa maana ya madaktari katika zahanati zetu za Wilaya ya Wanging‟ombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzungumzia suala hili la afya nataka niguse Halmashauri zote za Mkoa wa Njombe. Halmashauri ya Mji wa Njombe ambayo ni Jimbo la Lupembe, pia kuna changamoto ya hospitali, hospitali hatuna kule katika ile Halmashauri. Kuna zahanati mbili tu, vituo vya afya viwili na vituo vya afya hivyo viwili havina huduma ya upasuaji. Naiomba Wizara iangalie umuhimu wa kuendelea kuboresha na kujenga zahanati zingine ndani ya Halmashauri ya Mji katika Jimbo la Lupembe. Najua wao wakiongeza zahanati nyingi basi Wizara Afya Mheshimiwa Waziri wa Afya Dada yangu Ummy Mwalimu ataleta dawa za kutosha na kuweza kuwahudumia Wabena wetu kule wa Lupembe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto pia hii ya afya ipo pia katika Halmashauri ya Makete, hospitali ni chakavu tunaomba hospitali ile ikarabatiwe, vilevile na waaguzi ni wachache katika hospitali ile ya Makete. Tunaomba sasa tuongezewe wauguzi ili wananchi wa kule Makete waweze kupata huduma vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende sasa Halmashauri ya Mji ya Njombe Mjini. Pale kuna Hospitali ya Kibena, hospitali ile ya Kibena sasa hivi inatumika kama hospitali ya Mkoa kwa sababu Wilaya zote zinategemea hospitali ile. Ninaiomba Serikali sasa ikarabati kwa haraka ile hospitali, iongeze wahudumu kwa sababu tuna changamoto bado za madaktari na baadhi ya manesi. Kwa kuwa hospitali ile inahudumia watu wengi sana tunaomba waongezeke madakitari pamoja na manesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia miundombinu ya maji katika hospitali ile ya Kibena ni chakavu, umeme ni shida, naomba Serikali iangalie kwa karibu kwa sababu hospitali ile sasa hivi ndiyo inatumika kama Hospitali ya Mkoa ukizingatia kwamba Mkoa wetu wa Njombe ni mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wanatoka umbali mrefu sana karibia kilometa 147, wale akina mama wanaotoka Lupembe kwenda kufuata huduma ya upasuaji. Ni vema basi tukaona sasa na madaktari wa upasuaji waongezeka wawe wengi ili akina mama wale wanapokwenda wasikae kwa muda mrefu pale hospitali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niende kwenye suala la elimu; tunaishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa elimu na kuweza kutoa elimu bure kuanzia chekechea mpaka elimu ya sekondari. (Mkofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii kulipongeza Bunge kwa kutambua umuhimu wa elimu na kuweza kuchangia shilingi bilioni sita iende kununua madawati. Ina maana kila Jimbo litapata madawati 600; tunatambua umuhimu wa elimu na ndiyo maana tumeweza kufanya hivyo, nipongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kule kwetu katika hizi Halmashauri zote nilizozitaja kwa maana ya Wanging‟ombe bado tuna tatizo la wafanyakazi katika shule, pia shule zilizokuwepo majengo yake ni chakavu sana yanatakiwa kukarabatiwa, miundombinu ya vyoo ni mibovu inatakiwa kukarabatiwa. Kwa mfano kule Wanging‟ombe kuna shule moja inaitwa shule ya msingi ya Mjenga ina walimu wawili tu. Kwa hiyo, bado uhaba wa walimu katika shule za msingi na sekondari bado ni changamoto kubwa sana katika Halmashauri ya Wanging‟ombe, vilevile ukienda kwenye Halmashuri ya Ludewa changamoto hii ipo katika shule 108 ni shule nne tu, ambazo zina walimu wa uhakika, lakini shule 104 zote hazina walimu wa kutosha katika Halmashauri ya Ludewa. Tunaomba pia Serikali iangalie na iweze kutatua tatizo hili. Tatizo hili vilevile liko Halmashauri ya Mji kule Jimbo la Lupembe pia kuna changamoto hiyo shule haziko za kutosha na zilizopo zipo katika hali mbaya, zinahitaji kukarabatiwa, hali kadhalika katika Wilaya ya Makete na Wilaya ya Njombe kwa ujumla. Natumaini Mawaziri wetu wa TAMISEMI watazichukua changamoto hizi kwa haraka zaidi ili kuweza kutatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie barabara ambazo ziko katika Halmashauri zote za Mkoa wa Njombe. Zile barabara za Halmshauri, nilikuwa naiomba sasa Serikali iweze kutenga pesa nyingi ili ziweze kukarabatiwa katika kiwango kizuri ili ikifika msimu h wa mvua zile barabara zisiwe zinaharibika kwa urahisi. Kwa sababu Mkoa wetu wa Njombe ni Mkoa wenye neema kama jina langu, tunalima sana kule kwa hiyo, wananchi wa Mkoa wa Njombe wanashindwa kutoa yale mazao kutoka ndani kule vijijini kwa kutumia zile barabara za Halmashauri ili kukutana na zile barabara za TANROADS. Naomba Serikali izingatie hilo na iweze kutoa pesa ya kutosha katika suala zima la barabara za Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wazungumzaji wengi waliopita wamezungumzia suala la asilimia kumi. Labda tu niwambie Wabunge wenzangu na wale waliokuwa kwenye Halmashauri Madiwani wenzetu ni kwamba asilimia kumi ni lazima iende kwa wanawake na vijana kwa sababu hiyo asilimia kumi inatokana na mapato ya Halmashauri, ina maana kama hiyo asilimia kumi haijaenda kwa wanawake na vijana hiyo Halmashauri haijakusanya mapato yoyote? Hili ni jipu, Mheshimiwa Waziri hili ni jipu lazima mliangaliye kama Halmashauri inaweza kukusanya mapato lazima ile ten percent ambayo asilimia tano inaenda kwa vijana na asilimia Tano inaenda kwa wanawake lazima zipelekwe ili ziweze kusaidia akina mama pamoja na vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru kwa kunipa nafasi.